Thursday, 23 July 2015

PONDA APUNGUZIWA MASHTAKA

By    
 Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, jana ilimfutia shtaka moja kati ya matatu Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda.

Baada ya Mahakama kufuta shtaka hilo la kwanza, sasa Ponda atatakiwa kujitetea mashtaka mawili yaliyobaki.

Mahakama hiyo iliridhika na upande wa mashtaka uliowasilisha ushahidi, hivyo Ponda atajibu shtaka la pili na tatu.

Akitoa uamuzi mdogo kama mshtakiwa ana kesi ya kujibu au la, Hakimu Mary Moyo alisema Ponda ana mashtaka mawili ya kujibu.
Mashtaka yaliyokuwa yakimkabili Ponda baada ya kufikishwa mahakamani hapo Agosti 18, mwaka 2013 ni pamoja na kutoa kauli za kuwataka Waislamu kutokubali kuundwa kwa kamati za ulinzi na usalama za misikiti kwa vile ziko chini ya Bakwata, ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali.

Hakimu Moyo alisema shtaka analotakiwa kujitetea ni lile alilotenda Uwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro, ambapo anadaiwa kuituhumu Serikali kupeleka wanajeshi Mtwara kuzima vurugu za kupinga gesi kuletwa Dar es Salaam, lakini wananchi wa huko wakaishia kuuawa, kubakwa na kuteswa kwa vile asilimia 90 ya wakazi wake ni waislamu.

Ilidaiwa pia kuwa Ponda aliituhumu Serikali kutopeleka polisi Loliondo baada ya wananchi kupinga Mwarabu kupewa kipande cha ardhi ya uwindaji na hiyo ni kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo.

Katika shtaka la tatu, Ponda anadaiwa kuwa kauli alizotoa kuhusu wanajeshi walioua, kubaka na kutesa wananchi na madai kuwa asilimia 90 ya wananchi wa Mtwara ni Waislamu, zililenga kuumiza dini ya watu wengine, jambo ambalo ni kinyume na Kifungu cha Sheria Namba 390 na Kanuni ya Adhabu Namba 35 cha mwaka 2002.

Akifafanua, Hakimu Moyo alisema kuwa katika kosa la kwanza, mahakama hiyo imeona Ponda hana kesi ya kujibu kwa vile tayari shtaka hilo lilishatolewa uamuzi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kwamba mahakama ya chini haina uwezo wa kupinga.

Baada ya hakimu huyo kutoa uamuzi huo, upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Juma Nassoro uliridhika na uamuzi huo na kwamba wako tayari kuleta mashahidi katika kesi hiyo.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Sunday Hyera, uliomba kupangiwa tarehe nyingine ya kuwasilisha ushahidi wa upande wa utetezi kwa vile Wakili Kiongozi, Bernard Kongola alishindwa kufika mahakamani kwa sababu zilizo nje ya uwezo. Kesi hiyo itaendelea tena Agosti 7.

Chanzo: mwananchi

0 comments