Mraribu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Alvaro Rodriguez |
Alvaro amesisitiza kuwa UN itaendelea kushirikiana kikamilifu na Serikali ya Tanzania na wananchi wake.
Amesema hajawahi kukutana wala kuzungumza na Jarida la Indian Ocean na kutoa tuhuma na madai yaliyotolewa na jarida hilo, wala yale yaliyochapishwa na mtandao wa Jamii Forum.
Jarida hilo la Indian Ocean la Julai 10, mwaka huu, lilichapisha habari inayodai kuwa Serikali ya Tanzania ilikuwa inakabiliwa na uzembe wa taasisi zinazosimamia uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Habari hiyo ilidai pia kuwa Alvaro alikuwa hafurahishwi na maandalizi ya uchaguzi huo mkuu.
Katika taarifa yake iliyotolewa na UN jijini Dar es Salaam jana, Alvaro alieleza kuwa uhusiano kati ya UN na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na Jumuiya ya Kimataifa inayofadhili uchaguzi mkuu ni mzuri na umelenga kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka huu unakuwa wa amani na kushirikisha wananchi wote.
Alisema uchaguzi huo unaendeshwa kwa ubia baina ya wadau hao, na kwamba kwenye kilele cha ubia huo kuna Kamati inayoshughulikia Uchaguzi Mkuu, inajumuisha wadau wote hao.
Maamuzi yote makubwa kuhusu masuala ya uchaguzi yanafanywa na Kamati ya Mradi wa Uchaguzi na Kamati za Ufundi za mradi huo, zilizopo Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
“UN inaomba vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa, kuripoti kwa usahihi kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu pamoja na uchaguzi wenyewe” alisema.
Chanzo: Habari leo
0 comments