Saturday, 16 January 2016

BANDARI YADAIWA KUPITISHA SILAHA

By    

Mjadala wa wazi wa kujadili mgogoro wa Burundi unaoendelea makao makuu ya jumuiya ya Afrika mashariki umezidi kurindima  jijini Arusha ambapo wajumbe kutoka asasi za kiraia wameeleza kuwepo kwa taarifa kuwa  bandari za hapa nchini zinahusika kupitisha silaha zinazokwenda nchini Burundi   hivyo wameitaka jumiya ya Afrika mashariki kuchunguza jambo hilo ili kubaini ukweli wake.

Madai hayo yamekuja  ikiwa ni siku ya tatu ya mijadala inayohusisha wadau wanaohusika na mgogoro wa Burundi kwa lengo la kutafuta suluhu nchini humo.

Katika mjadala wa leo uliohusisha makundi ya asasi za kiraia kutoka nchi za jumuiya ya Afrika mashariki ,wajumbe wameonesha kutoridhishwa na kuendelea kuwepo kwa mijadala ya muda mrefu katika kutafuta amani ya nchi ya Burundi  ili hali serikali ya nchi hiyo bado haijaonesha nia ya dhati katika kutafuta  suluhu.

Vital Nshimirimana ni mmoja wa wajumbe kutoka asasi za kiraia , wakati akitoa mapendekezo katika mjadala  amesema kumekuwepo na taarifa kuwa bandari ya Dar es salaam  ya nchini hapa imekuwa ikihusika kupitisha silaha zinazokwenda katika baadhi ya nchi za jumuiya ikiwemo nchi ya Burundi hivyo wameitaka kamati ya utatuzi wa migogoro kuchunguza ili kubaini ukweli wa mambo.

Akielezea tuhuma hiyo mwenyekiti wa kamati ya  masuala ya ndani ya utatuzi wa migogoro katika nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika mashariki Abdulah Mwinyi amesema  jambo hilo ni lazima litafutiwe ushahidi wa kutosha kwa kuwa si jambo jepesi.

Maria Baricako kutoka taasisi ya utetezi ya wasichana na wanawake, kuhakikisha wanapata ulinzi na usalama katika nchi ya Burundi amesema wamejitokeza kuhakikisha wanapaza sauti kwa ajili watu wa Burundi wanaohitaji kupata haki ya kuishi katika nchi yao.

Kumekuwepo na mijadala kwa siku tatu mfululizo ambapo baadae mapendekezo yanayotolewa yanategemewa kupelekwa katika bunge la Afrika mashariki kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi.

CHANZO: startvtz.com

0 comments