Viongozi wote kuanzia ngazi ya vijiji hadi mkoa wametakiwa kushiriki kikamilifu katika kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu hadi kufikia Machi, 30 mwaka huu.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu akiongea na kikosi kazi cha udhibiti wa ugonjwa wa kipindupindu, kulia nina Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dkt.Nassoro Mzee.
Wito huo umetolewa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu wakati alipokutana na kikosi kazi cha cha udhibiti wa kipindupindu mkoani Dodoma
"Kipindupindu siyo suala ya afya peke yake, bali ni suala mtambuka hivyo sekta zote zinapaswa kujumuika katika kupambana na kutokomezwa ugonjwa huu.
Ummy alisema kipindupindu bado ni changamoto na janga hivyo kila mkoa unatakiwa kuliwekea kipaumbele kwakuwa ugonjwa huo unaua kwa haraka hivyo viongozi wote washiriki kikamilifu na si kuwaachia waganga wakuu wa mikoa au wilaya.
Aidha alisema licha ya kuwa na sheria ndogo za kila halmashauri za kusimamia usafi na mazingira lakini katika kudhibiti kuenea kwa kipindupindu lazima litakuja suala la kufungia biashara hususani za mbogamboga, matunda pamoja na chakula.
"Suala la kukusanya mapato lipo na litaendelea kuwepo lakini suala la kipindupindu linapoteza maisha,maisha hayatafutwi lakini pesa zinatafutwa lakini ukikosea utapoteza maisha ya watu wengi,” alisema Waziri Mwalimu.
Kaimu mganga mkuu mkoa wa Dodoma Dkt.Nassoro Mzee akisoma taarifa ya hali ya kipindupindu ya mkoa.
Ummy alisema tangu kipindupindu kiingie nchini Agosti mwaka jana, halmashauri zimetumia pesa nyingi katika kutokomeza ugonjwa huo, lakini wangeweza kuzuia mapema, pesa hizo zingeenda kutatua tatizo la madawati katika shule za msingi nchini.
"Mnapoona hamjaridhika na uendeshaji wa migahawa, msisite kuzifungia mara moja, mapato mtakusanya haraka kwa kuwa na nguvu za pamoja baada ya kutokomeza ugonjwa na kuweza kuingiza mapato mengi na kwa haraka tofauti na kuwa na hilo tatizo,” alieleza.
Hata hivyo alivitaka vikosi vyote vya mikoa nchi, kuwashirikisha wadau wote wakiwemo viongozi wa dini zote kuweza kuelimisha kuweza kutoa elimu ya jinsi gani ya kujikinga na ugonjwa wa kipindupindu kwa waumini wao.
Mkoa wa Dodoma umetumia takribani Shilingi Milioni 124 toka kipindupindu kimeingia mkoani humo na hadi leo kuna wagonjwa wanne katika kambi ya kipindupindu wilaya ya Bahi, jumla ya wagonjwa 450 waliugua na vifo12, wilaya zilizoathirika ni Bahi, Dodoma mjini na Chamwino.
0 comments