Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imevipa siku saba vyama 14 vya siasa kuthibitisha kama vitashiriki uchaguzi wa marudio utakaofanyika Machi 20 mwaka huu.
Vyama hivyo, kikiwamo cha CUF, ndivyo vilivyosimamisha wagombea wa nafasi za urais, uwakilishi na udiwani katika majimbo 54 Unguja na Pemba katika Uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana, kabla ya matokeo kufutwa na ZEC.
Uchunguzi wa Nipashe mjini Zanzibar umebaini kuwa wagombea wote tayari wamepewa mwongozo kupitia barua ya Januari 25, mwaka huu, na kutakiwa kuthibitisha kama vitashiriki uchaguzi wa marudio kuanzia kesho hadi Februari 11, mwaka huu.
Mwongozo huo umetolewa na Mkurugenzi wa ZEC, Salum Kassim Ali, na unavitaka vyama hivyo kuthibitisha ushiriki wao kwa maandishi.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa tarehe ya kufanyika uchaguzi imetangazwa rasimi katika gazeti la serikali tangu Januari 29, mwaka huu.
Mbali na wagombea katika majimbo, ZEC imewataka pia wagombea wa viti maalumu kukamilisha kuthibitisha kama watashiriki hadi ifikiapo Febuari 11 lakini hakutakuwa na kampeni kwa wagombea.
Salum katika barua yake hiyo alisema kazi ya kupiga kura na kuhesabu pamoja na kutangaza matokeo hitakamilika ndani ya siku tatu.
“Kazi ya kutangaza matokeo itafanyika Machi 23, mwaka huu,” imeeleza sehemu ya waraka huo.
Akizungumza na Nipashe mjini hapa jana, Mkurugenzi huyo wa ZEC, alithibitisha kutolewa mwongozo wa kushiriki uchaguzi wa marudio visiwani humo.
Wakati ZEC ikitoa mwongozo huo, kumetokea mgawanyiko mkubwa miongoni mwa vyama vilivyosimamisha wagombea katika uchaguzi uliyofutwa matokeo yake.
Vyama 10 vimeunda ushirikiano na Mwenyekiti wake ni Kassim Ali Bakar Ali ambaye ni mgombea urais kupitia chama cha Jahazi Asilia. Alisema wanatarajia kukutana leo kujadili na kutoa msimamo kama watashiriki uchaguzi huo wa marudio au la.
Alisema ajenda kubwa ya kikao hicho ni kujadili waraka wa tume wa kuwaarifu kurudiwa kwa uchaguzi lakini baadhi ya viongozi wa vyama vitatu ambao ni wagombea, walikanusha kuhusika katika mpango huo. Vyama hivyo ni TLP, SAU na CCK.
Vyama 10 vinavyounda umoja huo ni Jahazi Asilia, NRA, Chauma, TLP, SAU, CCK, ACT- Wazalendo, DP, CCK na Demokrasia Makini.
Viongozi waliokanusha kuwemo katika ushirikiano huo Naibu Katibu Mkuu wa CCK, Ali Khatibu Ali; Makamu Mwenyekiti wa SAU, Issa Mohamed Zonga, na Makamu Mwenyekiti wa TLP Zanzibar, Hafidh Hassan Suleiman, ambao pia ni wagombea wa urais wa Zanzibar
Hata hivyo wagombea urais, Juma Ali Khatib (TADEA) na Soud Said Soud (AFP) walisema kuwa wametengwa katika umoja huo.
“Sifahamu kwa nini tumetegwa katika umoja huo wa vyama lakini sisi tutatoa msimamo wa kushiriki baada ya kufanyika kikao cha Halmashauri Kuu ya TADEA mwezi huu,” alisema Khatib.
Soud alisema chama chake kinajipanga kuingia katika uchaguzi baada ya kupokea rasmi barua ya tume ya kutakiwa kuthibisha ushiriki kabla ya Febuari 11, mwaka huu.
Taarifa za uchunguzi zilizopatikana mjini Zanzibar zinasema Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, ameanza kukutana na viongozi wa vyama kwa mafungu baada ya kuwepo tishio la kususia uchaguzi kama ilivyotangaza CUF.
Viongozi wa vyama vitatu, CCK, Jahazi na SAU wanadaiwa kukutana na Msajili na kuzungumza kwa kina juu ya ushiriki wao katika uchaguzi huo.
Katika hatua nyingine, wagombea watatu wametangaza kushiriki uchaguzi wa marudio. Wagombea hao ni Ali Khatib Ali (CCK) Issa Mohamed Zonga (SAU) na Hafidh Hassan Suleiman ambao walitangaza hatua hiyo jana.
“Sisi wagombea wa urais wa vyama vya CCK, SAU na TLP tunatoa tamko rasmi kuwa tutashiriki uchaguzi wa marudio,” alisema Ali wakati akisoma tamko la pamoja.
Aliwataka wananchi wa Zanzibar kudumisha amani na utulivu pamoja na kujitokeza kwa wingi wakati wa kupiga kura na baada ya kukamilisha kazi hiyo, warudi nyumbani kusubiri matokeo.
Upande wake, CUF imesema imeanza kutengwa na tume tangu kutangaza kutoshiriki uchaguzi wa marudio.
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe, alisema barua za mwongozo wa uchaguzi wa marudio zilizotolewa na ZEC ilikuwa haijawafikia hadi jana.
Alisema pamoja na CUF kutoshiriki uchaguzi huo, kama chama hawatakiwi kukatiwa mawasiliano ili wafahamu kinachoendelea katika uchaguzi huo.
Alisema kutokana na hali hiyo, wamewasilisha rasmi malalamiko kwa mkurugenzi wa uchaguzi juu ya kunyimwa taarifa ya mchakato wa uchaguzi.
Wagombea wa urais wa Zanzibar walikuwa 14 ambao ni Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein (CCM), Khamisi Iddi Lila (ACT-Wazalendo) Juma Ali Khatib (TADEA), Hamad Rashid Mohamed (ADC), Said Soud Said (AFP), Ali Khatib Ali (CCK) na Mohamed Masoud Rashid (Chauma).
Wengine ni Maalim Seif Sharif Hamad (CUF), Tabu Mussa Juma (Demokrasia Makini), Abdalla Kombo Khamis (DP), Kassim Bakar Ali (Jahazi Asilia), Seif Ali Iddi (NRA), Issa Mohamed Zonga (SAU) na Hafidh Hassan Suleiman (TLP).
CHANZO: NIPASHE
0 comments