Friday, 15 April 2016

Deni la MSD laiponza Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo

HOSPITALI ya Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani, haina dawa kutokana na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kuidai Sh. milioni 210.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Tumaini Bailon, amesema ukosefu huo wa dawa umedumu kwa zaidi ya miezi minne sasa.

Akizungumza mjini hapa jana, Dk. Bailon alisema licha ya kuandika maombi mara kadhaa kwa MSD kuomba wapelekewe dawa kwa ajili ya wagonjwa tangu Januari, mwaka huu, bado jitihada hizo hazijaazaa matunda kutokana na kudaiwa deni hilo.

Alisema hospitali hiyo inakabiliwa na uhaba wa vifaa tiba na vipimo, kikiwamo cha kupimia wingi wa damu na kuwa wanaitegemea MSD ili kuondokana na matatizo hayo.

“Changamoto ni nyingi sana katika hospitali yetu, jenereta tunalolitumia ni dogo lenye kilowati 170 pekee, wakati linahitajika lenye uwezo wa kilowati 312 litakaloweza kukidhi mahitaji yetu”, aliongeza kusema Dk. Bailon.

Mfamasia wa Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, Mohammed Makalai, alipoulizwa sababu za ukosefu wa dawa katika hospitali hiyo, alikiri kuwapo kwa tatizo hilo tangu Oktoba, mwaka jana.

Alisema awali walipokuwa wakikosa dawa walikuwa wakinunua kwa wazabuni, lakini kwasasa wizara husika imebadili utaratibu huo wa manunuzi.

Alisema mfumo huo umebadilishwa na serikali tangu Agosti, mwaka jana, ambayo imepiga marufuku kununua dawa nje ya MSD.

Makalai alisema changamoto nyingine zinazoikabili hosptali hiyo ni uhaba wa maji, upungufu wa watumishi 157, vyandarua, baadhi ya vipimo na mashine ya kufulia ipo moja .

Chanzo: Nipashe

0 comments