Sunday 23 June 2013

Mizengo Pinda hizi ni mbio za mchangani



Na Nova Kambota,

Si rahisi  kumwelezea kwa undani wake waziri mkuu wa Tanzania Mizengo
Pinda ni mtu wa namna gani? huyu ni “mtoto wa mkulima”, huyu ni
mwanasheria, huyu ni kada wa CCM, huyu ana sauti ya upole, huyu ana
sauti ya ukali , huyu ni mzee wetu mwisho wa yote Mizengo Pinda ni
“mtatuzi” mkuu wa migogoro iwe ya madaktari, kisiasa ama ya
wanamtwara. Nitajadili hili la mwisho leo!

Ukimwona uso wake utaamini Pinda ni mwerevu kweli, ukisikia sauti yake
utajua hakika ni mtu mwenye weledi mkubwa na ukimwona mavazi yake
utatikisa kichwa kumkubali lakini usiombe Mungu ukamwona Mizengo Pinda
akizungumza huku akizungushazungusha mikono yake na kuchezeshachezesha
paji lake la uso akijibu hoja za CHADEMA , hapo matumaini yako yote
yataingia nyongo utajua hakika mgogoro wa Arusha ni msalaba mzito
mno kwa Pinda kuubeba.


Ukimwona mzee huyu akiwapa matumaini walalahoi kwa kauli zake za
“serikali tumejipanga kuzungumza na wananchi wa Mtwara” ghafla
anakunja sura na kusema “wabishi wote watapigwa” hakika utashtuka sana
na kubaki kinywa wazi  juu ya busara ya kiongozi huyu ambaye kule
“site” wameanza kusema
amepwaya mno kiasi cha kubaki mshauri tu wa Rais Kikwete badala ya
mtendaji mkuu wa serikali.

Pinda aliposhindwa kueleza iwapo Zanzibar ni nchi ama la binafsi
sikushangaa, alipotoa kauli za jino kwa jino kuhusu wanaoua maalbino
sikushtushwa na hata aliposhindwa kutumia madaraka yake ya uwaziri
mkuu kumshughulikia David Jairo niliona kawaida lakini watanzania
wanazidi kulia na kumwaga machozi jinsi Pinda anavyoshindwa kutatua
mgogoro wa kisiasa unaondelea kutokota na kuteketeza maisha ya watu
mkoani Arusha.

Ni kweli kuwa polisi wanapaswa kutii amri halali inayotolewa na
serikali, hawapaswi kuhoji wala kubisha lakini ni aibu kwa serikali ya
CCM kulea matatizo ati kwa kisingizio cha kuomba msaada wa jeshi la
polisi kudhibiti washindani wake wa kisiasa na wananchi wenye uthubutu
wa kuhoji. Inauma sana waziri mkuu Pinda kushindwa kutumia uzoefu wake
serikalini kwa miaka mingi  kutatua migogoro inayoiandama nchi, hili
nitalilaani milele!
Pasi na shaka Pinda anafahamu kuwa CHADEMA ni chama kilichosajiliwa
kama CCM, kina wafuasi ambao ni watanzania wakiwepo baadhi ya wananchi
wa mkoani Katavi ambao wanapaswa kuongozwa kwa sheria na kanuni za
nchi si maguvu ya vyombo vya dola wala “pigapiga” ambazo Pinda anadai
zitawashukia wakileta ubishi, ubishi wa nini? Kauli ya kidikteta sana
hii!

Alipoteuliwa kuwa waziri mkuu ukichanganya na sura yake ya upole na
uzee ulioanza kumnyemelea kila mtanzania aliamini kuwa Rais Kikwete
amepata msaidizi makini na zaidi ya yote mbadala wa Edward Lowassa
lakini sasa hakuna ubishi kuwa anahitajika “mwendawazimu” mmoja wa
kumweleza Kikwete kuwa afanye uamuzi mgumu wa kufikiria kumng’oa Pinda
ili kunusuru taifa. Busara ya kawaida inashawishi “yapasa mmoja afe
kwaajili ya wengi”Pinda aondolewe uwaziri mkuu ili taifa litue “mzigo”
huu mzito wa uongozi legelege unaolilemea.

Ni vigumu kuamini kuwa Pinda ataweza kutatua hata mgogoro ndani ya CCM
sembuse huu mgogoro aliouanzisha wa polisi dhidi ya raia! Labda
nimuulize Pinda na serikali ya CCManayoitumikia anategemea nani
ataacha ubishi katika mazingira ambayo serikali yenyewe inafanya
ubishi? Watu wanategemea serikali iwe ya
mwisho kufanya ubishi lakini inapogeuka ya kwanza kubisha ujue uhai wa
nchi upo hatarini, ona serikali inabishia kuboresha huduma za elimu,
inabisha kuboresha huduma za afya. Hivi kulikuwa na haja gani ya Nape
kuituhumu CHADEMA  kujilipua bomu?, hivi nani kamteua Nape kuwa IGP?
Katika mazingira haya ni vigumu kuamini kuwa ama Pinda au serikali ya
CCM wana nia ya dhati ya
kukomesha “haya mauaji” ya walalahoi wasio na hatia kwa kigezo cha
kudhibiti maandamano.



Kwa mtu kama Pinda kuiambia dunia kuwa serikali inajipanga kudhibiti
wabishi kwa kuwapa mkong’oto basi! ili “kuwafunga midomo” kunatoa
kiashiria kibaya kuwa matatizo yanayofanya watu waandamane hayawagusi
“wakubwa” ndiyo maana hata utatuzi wake unafanyika kwa staili ya
kibabe. Hivi Pinda hajui kwanini wanamtwara ama CHADEMA wanaandamana?
Hajui kuwa watu wanaandamana kupinga unyonyaji?
Hivi Pinda hajui kuwa Tanzania kuna umasikini wa kutengenezwa na
mfumo? Lakini kwanini Pinda asikubali kuwa siyo kila sehemu inahitaji
nguvu bali kuna sehemu zinahitaji busara kuliko nguvu. Akilijua hili
basi tungependa tuone
ukomavu wake katika hili atambue kuwa “makali ya panga hayaribiwi
shingoni”.

Kwa mara ya kwanza tatizo la Mtwara lilipojitokeza miezi kadhaa
iliyopita mwaka huu tulidhani serikali imejifunza wenye “imani
dhaifu”wakajipa moyo kuwa Pinda sasa ameiva katika tasnia ya utatuzi
wamigogoro  kumbe wapi bwana! Kumbebesha Pinda  jukumu kubwa kama hili
la Arusha hakuna tofauti na kujaribu kubeba tembo kwa kutumia pick up!
Kila akikunja “ndita” na paji lake la uso kutengeneza namba 11 huku
sautiyake ikitetema kwa mawimbi dhaifu utabaini kuwa mgomo wa
madaktari si saizi yake hata kidogo. Inatia ukakasi na kuongeza chuki
dhidi ya CCM kwa kumtumia Pinda kutatua mgogoro ambao ni “maji marefu”
kwake.

Kila nikijenga picha ya hiyo siku isiyo na jina ambapo walimu nao
wataingia kwenye mgomo moto kwa maana kwa sasa kuna kila dalili ya
kuwepo mgomo baridi ukitaka kuamini angalia matokeo ya shule zetu,
naomba Mungu mgomo wa walimu umkute mtoto wa mkulima akiwa
amepumzika na wajukuu wa mkulima akifaidi posho yake ya uzeeni.

Kuahidi kutoa milioni kumi kwa timu ya taifa ni jambo moja na kuwa
kiongozi makini ni jambo lingine, kuna utofauti mkubwa kati ya kuitwa
waziri mkuu na kutimiza majukumu ya uwaziri mkuu kikamilifu. Siku ya
kuteuliwa kwake Pinda aliwahi kujikweza kwa kusema “kuwa karibu ya
uwaridi kunamfanya mtu kunukia uwaridi” akitaka kutuaminisha kuwa
kufanya kwake kazi chini ya serikali ya Kambarage basi na yeye
atanukia “Unyerere” lakini sasa si ya chumbani tena bali bararani kila
mtu ni shahidi kuwa Pinda hafanani na Nyerere kwa nywele wala ukucha.

Haina maana yoyote kwa Pinda kuendelea kuzungukazunguka kwenye kitu
cha matairi bungeni huku wananchi wakiendelea kuteswa kila wanapotumia
haki yao ya kuandamana! Ni dhambi isiyosameheka kwa kiongozi huyu
kuingia
bungeni na kusaini posho huku masikini wa nchi hii wakihaha kulinda
uhai wao kila wanapoamua kuchagua mbadala wa CCM au kuhoji kile
wanachoamini ni haki yao  .
Alihitajika kiongozi imara anayejuakuwa pasipo watanzania hakuna
waziri mkuu, alihitajika “mpambanaji”anayejua kuwa uhai ni haki ya
kila mtu, alihitajika “mpiganaji” anayejua utawala wa kibabe si urithi
aliotuachia baba wa taifa Mwl Nyerere, alihitajika mzalendo ambaye
angeacha hata posho za Dodoma na kurejea Magogoni Dar es salaam mara
moja ili kuwasilisha barua ya kujiuzulu kwa rais na kuomba msamaha kwa
watanzania .

Uongozi ni utumishi ni zaidi ya hotuba na uheshimiwa. Waziri mkuu
anayeshindwa kutatua migogoro iwe ya kisiasa au kijamii “anapoteza uhalali” wa
kuendelea kuongoza inampasa Pinda kuongozwa na hekima kuchukua uamuzi
mgumu kuachia ngazi. Naamini Pinda atalinda zaidi heshima yake kwa
kujiuzulu kuliko kuendelea kujichumia dhambi kwa kupokea hela za
walipa kodi masikini wa Tanzania huku akishindwa kufanya hata
“theluthi moja” ya kazi anazopaswa kuzifanya.

Ili kuwa mwanariadha mzuri kuna mbinu nyingi sana unazopaswa kuzijua
ndiyo maana wapenda mchezo huo wameupachika jina la “kukata upepo” hii
ina akisi kilicho nyuma ya tasnia hiyo. Siyo kila ukimbiaji unafaa
kila sehemu halikadhalika siyo kila mahala panafaa kukimbia. Mkimbiaji
mzuri anajua wapi afanye mazoezi ili awe imara kwaajili ya mashindano
na anafahamu maeneo yapi akifanyia mazoezi yatamfanya atoe ulimi nje
siku ya mashindano huku miguu ikigoma kusonga mbele.

Natofautiana kwa kiasi kikubwa na Pinda mwenyewe, wana CCM na baadhi
ya watanzania wanaomwita Pinda mtoto wa mkulima, nalikataa hili
kwasababu mtoto wa mkulima anafahamu vema mazingira ya vijiji. Mtoto
wa mkulima sharti ajue hatari ya kupanda mbegu mchangani tena juu
lazima mtoto wa kulima ajue mafuriko yanavyoweza kusomba mbegu
zilizopandwa juu mchangani. Pinda si wa aina hii hajui mlima wala
mchanga huyu ni sawa na mwanariadha aliyefanyia mazoezi mjini kisha
akaenda kushiriki mashindano kijijini.

Ataniwia radhi Pinda kwa kumfanisha na mwanariadha wa mjini
aliyefanyia mazoezi kwenye barabara nzuri za mjini kisha akajiona
imara na kuamua kwenda kijijini kushiriki mashindano huko kuna milima
na mchanga hakuna barabara nzuri za lami katika mkanganyiko huu
mwanariadha Pinda amekimbia mlima na kukimbia mchangani pasipo kujua
hatari ya uamuzi huo. Pinda alipaswa kujifunza kukimbia mchangani
kabla ya siku ya mashindano tofauti na huu mzaha wake wa  hivi sasa wa
kuanza mbio za mchangani siku ya mashindano ni ndoto kushinda!

www.novakambota.wordpress.com

0 comments