Monday, 28 October 2013

KATOLIKI WAMKUNA LOWASA

 WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, amelipongeza Kanisa Katoliki kwa huduma bora na nzuri wanazotoa kwenye sekta ya elimu na afya hapa nchini.

Aidha, alisema kuwa hata kwenye nchi zilizoendelea makanisa hutoa huduma kwa jamii kama ilivyo hapa nchini jambo alilosema kuwa serikali itaendelea kuutambua na kuudhamini mchango wao.

Lowassa aliyasema hayo jana jijini hapa wakati alipoongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa nyumba ya mapadri wa Kanisa la Watakatifu Petro na Paulo, Parokia ya Kijenge ambapo zaidi ya sh milioni 192 zilipatikana.

Alisema kuwa shule za kanisa hilo ndizo zinazoongoza kwa kufanya vizuri kitaaluma hapa nchini sanjari na hospitali zao zinatoa huduma nzuri jambo alilowatia moyo waendelee nalo kwani serikali inatambua na kuthamini mchango wao huo na itaendelea kushirikiana nao.

“Zamani nilidhani makanisa yanasaidia kujenga shule na hospitali kutokana na serikali kuwa na uwezo mdogo, lakini baada ya kutembelea nchi zilizoendelea ikiwemo Ujerumani nimekuta hospitali nyingi ni za makanisa,” alisema Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli.

Naye Mwakilishi wa Askofu wa Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lobulu, alisema kuwa mwanadamu akikosa huduma ya afya na elimu hawezi kuwa na amani hata kama ameshiba.

Padre Christian Tarimo ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Njiro, alisema kuwa jukumu la kulinda amani na utulivu nchini liko mikononi mwa viongozi waliopewa dhamana hiyo na wananchi, hivyo wasichoke kulinda amani hiyo.

Alisema kuwa ujenzi wa nyumba hiyo ya mapadri unatazamiwa kugharimu sh milioni 315, na kwamba kukamilika kwake kutawezesha upanuzi wa kanisa hilo kwa kubomoa nyumba zinazotumiwa na mapadri kwa sasa, na eneo hilo likatumika kwa ajili ya upanuzi huo.

  Katika hatua nyingine, Lowassa na marafiki zake walichangiash milioni 20 huku akiwataja marafiki hao kuwa ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo ole Nangole pamoja na mmiliki wa vituo vya mafuta aliyemtaja kwa jina moja la Lalaa.

“Mimi na marafiki zangu tunachangia sh milioni 20, huwa nasakamwa kuhusu marafiki zangu wanaonichangia, leo niko nao hapa, Ole Nangole na Lalaa,” alisema Lowassa.

Wengine walioambatana naye ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck ole Medeye, Meya wa Jiji la Arusha, Gaudency Lyimo na Mjumbe wa Halmashauri Kuu, Mathias Manga aliyechangia sh milioni 5.


CHANZO: TANZANIA DAIMA

0 comments