Monday, 4 November 2013

TEC WAPINGA MFUMO MPYA WA MATOKEO

RAIS wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcius Ngalalekumtwa, amepinga mfumo mpya wa upangaji wa madaraja ya ufaulu kwa wanafunzi wa sekondani yaliyotangazwa na Wizara ya Elimu hivi karibuni, akisema ni upungufu na kuporomoka kwa siasa.

Askofu Ngalelekumtwa ambaye pia ni askofu wa Jimbo la Iringa, alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza katika mahafali ya sita ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mwenge (Mwuce) kilichopo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Alisema kuwa uamuzi huo wa serikali unaishangaza dunia kutokana na wenye dhamana kubadili maneno katika kushughulikia elimu huku wakijua hali si nzuri katika sekta hiyo.

“Kufuta daraja sifuri ni sawa na kuongeza sifuri nyingine kwa vile utazalisha wahitimu wengi wasio na sifa hata kama utabadili maneno.

“Hatutaki kutafuta ni wapi tulipojikwaa na kutufikisha hapo tulipo kwa kuwa kipimo hicho kinaweza kuitumbukiza elimu yetu shimoni na kuliweka taifa pabaya hasa katika taaluma duniani,” alisema.

Naye Askofu wa Jimbo la Moshi, Isack Amani, akizungumza katika mahafali hayo, alisema taifa limeachwa katika mshangao ambao jamii inatakaiwa ipitie upya uamuzi huo kwa sababu mawazo yanaweza kufutika usoni, lakini si kichwani.

Akizungumzia mustakabali wa elimu, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) cha jijini Mwanza, Padri Pius Mgeni, alisema hali ni mbaya katika baadhi ya vyuo vya elimu ya juu.

Alisema kuwa hatua hiyo ni kutokana na idara nyingi ikiwemo inayoshughulikia lugha ya Kiswahili kuongozwa na wageni kwa vile wazawa hawana sifa.


CHANZO: TANZANIA DAIMA

0 comments