SERIKALI imeahidi kulifanyia kazi suala la stika za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwenye kazi mbalimbali za wasanii na kumaliza changamoto zilizojitokeza.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alipokuwa akifanya majumuisho wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia Muswada wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2015.
Muswada huo wenye lengo la kuzifanyia marekebisho sheria 16 zinazohusu masuala ya fedha, kodi, ushuru na tozo mbalimbali nchini uliwasilishwa juzi na kupitishwa na Bunge hilo.
Akifafanua hoja mbalimbali, Salum alisema ameagiza watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wafanyie kazi malalamiko ya wasanii nchini kuhusu suala la stika zinazohusu kazi zao.
Kuhusu kazi za wasanii wa nje zinazoletwa nchini ambazo hazina stika za TRA, Waziri wa Fedha, alisema hiyo ni changamoto nyingine ambayo pia wameigundua na kwamba wanaifanyia kazi.
Wakati akichangia muswada huo, Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata (CCM), alisema filamu zinazotoka nje ya Tanzania zinaua soko la filamu za ndani kwa sababu zenyewe zinaingizwa kwa wingi na hazina stika yoyote ya TRA.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments