Saturday, 25 May 2013

Mtwara: Hatujazuia gesi, tunataka haki

Na  Charles Misango, Tanzania Daima

VURUGU kubwa zilizozuka mwanzoni mwa wiki hii mkoani Mtwara, zimepoka maisha ya Watanzania wenzetu sita, na wengine wengi wakiachwa na majeraha ya maumivu kama sio vilema vya kudumu.

Waliopoteza maisha ni raia wawili, akiwemo mama mmoja aliyetwanga risasi akiwa ni mjamzito, pamoja na askari wanne wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, (JWTZ) ambao walifariki katika ajali ya gari wakielekea mjini Mtwara kuwasaidia askari polisi kukabiliana na mashambulizi ya raia.

Mali kadhaa za serikali, vyama vya siasa lakini kubwa zaidi hata nyumba na magari ya watu binafsi walizopata kwa shida na tabu kubwa zikiteketezwa na kuwaachia wahusika umasikini wa kutupwa.

Hali katika mji wa Mtwara na vitongoji vyake inatisha, inasikitisha na kuumiza mioyo kwa wakazi wengi, hususan akina mama na watoto ambao kwa siku kadhaa kabla ya tukio hili, maisha yao yamekuwa ya hofu tupu.

Tangu kuzuka kwa vurugu hizo, wapo watu hususan wanawake na watoto ambao wamekimbilia msituni na wanaishi maisha ya mateso makubwa kwa kukosa maji na chakula.

Hata huko, pamoja na mateso hayo, bado wana wasiwasi wa kukamatwa, kupigwa na askari polisi kwa madai ya kushiriki katika vurugu. Hakuna amani, hakuna usalama, hakuna chakula wala maji.

Mambo makubwa mawili mazito yametokea katika vurugu hizi. Kwanza ni kusitishwa kwa shughuli za Bunge kwa siku mbili, kwa hofu ya kuzuka kwa machafuko zaidi kutokana na kauli za wabunge ambazo zingetolewa wakati wa kuchangia Wizara ya Nishati na Madini ambayo hotuba yake ilikuwa kiini cha vurugu hizo.

La pili, ni hotuba kali ya serikali bungeni iliyosomwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi ambaye pamoja na Rais Jakaya Kikwete, walilaani vikali vurugu hizo na kutangaza rasmi kuchukua hatua kali na kwa nguvu zote dhidi ya waliowaita vinara wa kuchochea vurugu hizo popote walipo ndani ama nje ya nchi.

Serikali ikaenda mbali zaidi ikidai kwamba vurugu hizo zinachochewa na makundi ya watu wasioitakia mema nchi hii, vikiwemo baadhi ya vyama vya siasa.

Inawasukumia lawama wananchi wa Mtwara kwa kugomea usafirishaji wa gesi kutoka mkoani humo na kusambazwa nchini kote.

Juzi akitoa tamko la serikali, Waziri Nchimbi alisema wazi kuwa wananchi wa Mtwara sharti wajue kuwa rasilimali ya gesi ni ya Watanzania wote na sio ya watu wa eneo moja tu, na kwamba mtindo wa aina hiyo unaoanza kuenea kote nchini, ni wa hatari na usiokuwa na uzalendo.

Wakati serikali ikiwashambulia wananchi hawa, na kwa bahati mbaya kudakwa kwa nguvu na wanasiasa hususan wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakazi hao wanapinga vikali shutuma hizo.

Wananchi wengi wa Mtwara si tu wanaikana kwa nguvu, bali pia wanachukizwa na kile wanachoita, ‘kubambikizwa’ maneno yasiyo yao na watawala.

Mathias Malambo ni mmoja wa wakazi wa mjini Mtwara anayekerwa na kukana madai haya.
“Tunaumia sana kusingiziwa mambo haya na hawa wanasiasa na waandishi wa habari, kwamba tunazuia gesi isitoke. Hatujazuia, ila tunataka watawala watimize ahadi yao waliyotoa wakati wa kampeni kwenye uchaguzi mkuu uliokwisha.

“Shida yetu tunataka mtambo wa kuchakata gesi badala ya kujengwa huko wanakotaka (Dar es Salaam), ujengwe hapa hapa, na ndipo gesi isafirishwe kwenda kwengine.
“Hiki kinu kikijengwa hapa, kitasaidia kutoa ajira nyingi kwa walalahoi, kujengwa kwa viwanda vingi na kuimarika kwa bandari yetu, mambo tunayoamini yataleta maendeleo makubwa ya kiuchumi kwa watu,” anasema Mathias.

Ramadhan Nassoro Juma anakwenda mbali zaidi na kudai kwamba, serikali ndio kiini cha mgogoro huo na wala sio wao kama wananchi wa kawaida.
“Kwanini mawaziri hawasemi ukweli? Badala yake wanalindana kwa kutusukumia lawama ili Watanzania wenzetu watuone ni wajinga, wabinafsi na tusiopenda maendeleo ya wenzetu.
“Nani kasema Wamakonde hawataki gesi isambazwe? Mawaziri wanalindana, wanatukosea, wanatukandamiza kwa siasa zao, na tukidai tunaonekana eti tunatumiwa na wanasiasa, kwani sisi hatuoni umasikini wetu hadi mwingine atuambie?” anasema Nassoro.

Kauli yake inaungwa mkono na Rehema Salum ambaye anaeleza kukerwa kwake na kile alichokiita upotoshaji wa makusudi unaofanywa na watendaji wa serikali na wanasiasa wa CCM kuficha madhambi yao.

Rehema anasukuma lawama kwa serikali akidai imekuwa ikipotosha ukweli kwa maslahi binafsi, na hivyo kuwafanya waonekane ni wakorofi.
“Matatizo yote haya yamesababishwa na uongozi mbovu wa serikali, halafu wanataka kufunika uovu wao kwa kutusingizia. Watuombe radhi kwa kutulisha maneno ya uongo na iwawajibishe watendaji na wanasiasa walioshiriki kutoa matamshi haya.
“Wasituone wajinga na tusiojua kufikiri. Sisi ni wapole na wakimya, lakini haina maana kuwa hatuna akili. Wasitubambikie maneno midomoni, waseme kile tunachokipigania,” anasema Rehema.


Uchunguzi wa Tanzania Daima Jumamosi, umebaini kuwa kwa kiasi kikubwa vurugu hizi zimechangiwa kwa kiwango kikubwa na utendaji kazi mbovu wa baadhi ya mawaziri na kukuzwa na wanasiasa wa pande zote mbili.

Tangu kugunduliwa kwa gesi, watendaji kadhaa wa serikali kwa nyakati tofauti wamehusika kutoa kauli nono zilizojaa matumaini kwa wakazi hawa juu ya namna watakavyonufaika na uchimbaji wa gesi.
Upo ushahidi wa kutosha na usio na shaka unaoonesha namna wanasiasa hususan wa CCM walivyotoa ahadi wakati wa kampeni, kwamba upatikanaji wa gesi utakwenda sambamba na ujenzi wa kinu cha kuchakata gesi ambayo kutoka hapo ndipo itakaposambazwa nchini kote.

Wananchi hao wakaambiwa kuwa kuwekwa kwa kinu hicho mkoani Mtwara, kutawezesha kujengwa kwa viwanda kadhaa vikiwemo vile vya saruji na plastiki ambavyo vitatumia malighafi zitakazotokana na gesi hiyo, na hivyo kuongeza ajira kwa wananchi wengi.

Wananchi wakapokea kauli hizo kwa furaha na matumaini makubwa ya kukomboka na umasikini ambao umewagubika kwa miaka mingi, ingawa wamekuwa wakizalisha korosho zinazoliingizia taifa mamilioni ya fedha.

Wakaaminishwa na wanasiasa hao kuwa kule kuwepo tu kwa mtambo huo mkoani Mtwara ni fedha tosha kwa sababu nyingi za msingi.

Kwa imani hiyo, wananchi wakafurahia jambo hili na kwa mujibu wa maelezo ya wengi, wakatoa ushirikiano tangu kupisha eneo litakalojengwa mtambo huo, na kule bomba litakapopita.


Kiini cha vurugu

Kwa mujibu wa uchunguzi wa Tanzania Daima Jumamosi, kiini cha vurugu za sasa kina mikondo miwili.
Kwanza ni kampeni za vyama vya siasa ambavyo viliwataka wakazi wa Mtwara kusimama imara na kuhakikisha kuwa ahadi walizopewa na watawala zinatekelezwa kikamilifu.

Vyama hivyo, vikawahamasisha wananchi kusimama imara na kuwataka watambue kuwa sehemu yoyote duniani, wakazi wa eneo husika inapotoka rasilimali wananufaika na kupata maendeleo makubwa na si kuambulia mateso, adha na umasikini kama ambavyo imetokea katika baadhi ya maeneo ya nchi ambako kumepatikana madini na rasilimali nyingine.

Vyama vya siasa ‘vikawaamsha’ wananchi wasilewe maneno yaliyojaa ahadi na wawe na ujasiri wa kuhoji watawala kile walichowaahidi.

Hamasa hii iliwaingia vema wananchi wengi. Wakakumbuka namna ambavyo wameahidiwa mambo mengi hasa katika ujenzi wa barabara na bei ya zao la korosho kwa miaka mingi bila mafanikio.

Pili, vurugu hizi zimechangiwa kwa kiwango kikubwa na kutotekelezwa kwa ahadi walizopewa wananchi hawa na wanasiasa wakati wa kampeni. Kutotimizwa kwa yale waliyoambiwa hususan katika mradi huu wa gesi.

Kauli ya serikali ya kujenga bomba la kusafirisha gesi, na kuachana ama kukaa kwake kimya kuhusu kujengwa kwa kinu cha kuchakata gesi mkoani Mtwara, yawezwa kusema waziwazi kuwa kiini na msingi mkubwa wa ‘hasira kali’ ya wananchi ambao katika hali ya kukata tamaa ya maisha, wameamua kufanya walichokiona kinawafaa. Wakafanya vurugu!

0 comments