Friday, 31 May 2013

UWALIMU WITO; Walimu wapya Sumbawanga waishi kwa hisani

Na Sammy Kisika, Tanzania Daima

WALIMU 75 walioajiriwa Machi mwaka huu na kupangiwa vituo katika wilaya ya Sumbawanga na Kalambo, mkoani Rukwa, wanaishi kwa kutegemea hisani ya wasamaria wema kutokana na ugumu wa maisha unaowakabili.

Katibu wa Chama cha Walimu (CWT) Wilaya za Sumbawanga na Kalambo, Vicent Ndewele, alibainisha hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari akielezea hatma ya walimu hao katika vituo vyao vya kazi.

Ndewele alisema walimu hao wana namba ya malipo ya mshahara, lakini kitu cha kushangaza kwenye orodha ya malipo ya mishahara (payroll) majina yao hayapo.

Alisema kuwepo kwa tatizo hilo kumekuwa kukisababisha wasipate mishahara, hali inayowasababishia ugumu wa maisha.

Ndewele alisema kuwa walimu hao wamefikia hali mbaya huku baadhi yao wakionekana kukata tamaa na wako tayari kuacha kazi, kwani wamedai kuwa wamechoka.

Alitoa wito kwa serikali kuhakikisha walimu hao wanalipwa mwisho wa Juni huku akiwataka wakurugenzi wa halmashauri hizo kutatua matatizo ya walimu hao na kuacha majibu yasiyo na ufumbuzi.

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri hizo, Chrispine Luanda, alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kuongeza kuwa halmashauri haina makosa, kwani wao walifuata taratibu zote ndiyo maana walimu hao walipata namba ya malipo.

“Sisi tumetimiza wajibu wetu, ila tatizo ni Idara Kuu ya Utumishi na Hazina huko Dar es Salaam wao ndio wanawacheleweshea hao walimu,” alisema Luanda.

0 comments