Saturday 8 June 2013

Mtwara: Hatujazuia gesi, tunataka haki - 2

Na  Charles Misango


ITAKUMBUKWA kuwa katika toleo la wiki jana hatukuweza kuendelea na makala hii kutokana na tatizo lililokuwa nje ya uwezo wetu kama tulivyolianza katika toleo la wiki juzi.

Leo tunaendelea kueleza kauli na msimamo halisi wa wana-Mtwara wanaopinga shutuma zinazoelekezwa kwao kuhusu sakata la gesi.

Kampeni za uchaguzi za mwaka 2010 zikachukua nafasi kubwa za kutoa ahadi nono kwa wakazi wa Mtwara kutoka kwa wagombea wa CCM. Hao wakawaambia kuwa kupatikana kwa gesi mkoani humo, kutalenga kwanza kuwanufaisha wakazi wa mkoa huo, na Watanzania wengine kwa ujumla wake.

Matamshi haya yakapokelewa kwa ushabiki mkubwa ikikumbukwa kwamba wakazi karibu wote wa mkoa huo na wale wa Lindi wanategemea zaidi zao la korosho ambalo hata hivyo halijawaletea maendeleo yoyote.

Ramadhan Sharif mkazi wa Magomeni, anasema kuwa walipopata maneno haya awali hawakuyashangilia sana kwa sababu kadhaa.

Anasema moja iliyo kubwa ni tabia ya watendaji wa serikali ya kutoa ahadi nono wakati wa kampeni, lakini mara tu wanapopata madaraka kila kitu kinakwisha.

Anatoa mfano wa kutokamilika kwa ujenzi wa barabara kiwango cha lami kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, na kila ufikapo wakati wa uchaguzi, lugha za waomba kura zimekuwa ni zilezile za kukamilisha kipande kidogo ndani ya muda mfupi.

“Kwa hiyo, tukajaribu sana kuhoji tutanufaikaje. Wakasema kuwa mpango wa serikali ni kutujengea kinu cha kuchakata hapahapa na kitakachosafirishwa kwenda Dar es Salaam ni gesi iliyo tayari kwa matumizi tu.

“Kwa maana nyingine walichotueleza na sisi tukaamini kuwa kitakuwa mkombozi kwetu, ni kwamba kila kitu kitafanyika hapa hapa, na kwamba matokeo ya hatua hii ni kwanza kuwepo kwa ajira zaidi ya 100 kwa watu watakaoajiriwa katika mitambo hiyo. Lakini lililo kubwa ni kule kuanzishwa kwa viwanda vitakavyotokana na uwepo wa mitambo hii.

“Sasa tunachoambiwa kwa sasa, ni kwamba eti itasafirishwa na mitambo hii haijengwi hapa inasukumwa kule Dar es Salaam na Bagamoyo. Hiki ndicho chatukera ati. Kwanini walitudanganya?” anasema Sharif.

Wakazi wa Mtwara wanakiri kuudhiwa zaidi na kupindishwa kwa maneno, kwamba wanashawishiwa na kuwa mgogoro una mkono wa wanasiasa.

“Wanachokifanya wale wa upinzani ni kutukumbusha ambacho CCM ilituahidi. Lakini hata kama hawatusemei, kwani siye majuha kiasi kwamba tuko wepesi wa kusahau haraka?” anauliza mkazi mwingine, Hashimu Baraka wa Shangani West.

Kukinzana kwa kauli za viongozi wa serikali na wale wa CCM kuhusu suala hilo kunawakera sio wana-Mtwara tu, bali hata vyama vya upinzani, hususan CHADEMA ambao wanasingiziwa kuwa nyuma ya vurugu za kila wakati.

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) anapinga hatua za viongozi wa taifa kutoa kauli zisizokuwa za ufumbuzi wa mgogoro wa gesi asilia mkoani Mtwara, hususan kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuwa chanzo cha mgogoro unaoendelea Mtwara ni wanasiasa.

Kupinga kwake kunatokana na kauli ya hivi karibuni ya Rais Kikwete, akisema kuwa chokochoko hizo zinasababishwa na baadhi ya wanasiasa wanaotaka kujipatia umaarufu kupitia mgogoro huo.

Akifafanua zaidi, Mnyika anasema kwa mara ya kwanza Rais Kikwete aliyasema hayo Januari mwaka huu katika baadhi ya hotuba zake za kila mwisho wa mwezi, mara baada ya vurugu hizo zilipoanza kupinga mradi huo.

“Rais ni mkuu wa nchi, kiongozi wa serikali na amiri jeshi mkuu. Nilitarajia rais na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wangewataja kwa majina hao wanasiasa na kutueleza hatua walizochukua,” anasema Mnyika.

Anasema kama mgogoro huo una mikono ya ndani na nje ya nchi na kwamba wanawasaka wachochezi hao ndani na nje ya nchi, hiyo inadhihirisha wazi kuwa hadi sasa serikali haina hakika na kile inachodai.

Anaongeza kuwa badala ya kuhangaika kuwasaka hao wanasiasa na watu wa nje, ni vema akawasaka kwanza wale walioko ndani ya serikali na CCM ambako vyombo hivyo anaviongoza, ili kubaini chanzo badala ya kushughulikia matokeo.

“Rais Kikwete anakumbuka kwamba mwaka 2005 alikwenda Mtwara na kuahidi umeme wa gesi wa MW 300 kuzalishwa kabla ya mwaka 2010, hata hivyo hakutimiza ahadi yake hiyo,” anasema.

Mnyika anasema ieleweke kwamba suala hili si la wakazi wa Mtwara peke yake, bali ni kilio cha wananchi katika mikoa mingi yenye rasilimali na maliasili.

“Umwagaji damu sio suluhisho kwa pande zote, lakini serikali inapaswa kusoma alama za nyakati na kujielekeza katika kushughulikia vyanzo vya migogoro zaidi ya kukabiliana kwa kimabavu,” anasema.

Malalamiko ya gesi yapo pia mkoani Lindi ambako tangu gesi, ianzwe kuvunwa mwaka 2004 na bomba lake kujengwa hadi jijini Dar es Salaam chini ya Songas, yamekuwepo malalamiko ya ufisadi wa mikataba mibovu ambayo yana athari kwa wananchi wa maeneo husika na taifa kwa ujumla.

“Rais Kikwete, Waziri Nchimbi na serikali kwa ujumla warejee mapendekezo tuliyotoa hivi karibuni kwenye hotuba ya kambi rasmi ya upinzani bungeni,” anasema Mnyika.

Mnyika anabainisha kuwa serikali inapaswa kuweka wazi mikataba yote ya uendelezaji wa gesi asilia, kuanzia ya utafutaji hadi ya ujenzi wa bomba la gesi.

“Manufaa ya kuambiwa tu na kuonyeshwa michoro inawafanya wananchi wakose imani kwa kuwa walishawahi kuambiwa kwa miaka mingi bila utekelezaki,” anasema.

Serikali isifunge milango ya majadiliano na wananchi wake kwa kuwa mwisho wa siku kwa mujibu wa katiba ya nchi ibara ya 8 mamlaka na madaraka yote ni ya serikali itawajibika kwa umma ambako lengo la serikali ni kuleta ustawi wa umma na si vinginevyo.

Maoni ya kambi rasmi ya upinzani bungeni ya mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2012/13 na makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2013/14, ni muhimu yakazingatiwa na kutekelzwa na serikali.

Utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi (upstream); shughuli zote za utafutaji wa mafuta na gesi nchini unatawaliwa na Sheria ya Utafutaji na Uzalishaji Mafuta ya mwaka 1980 (The Exploration Act, 1980).

Shughuli ya usafirishaji na uuzaji (down stream) hii hutawaliwa na sheria ya EWURA sura ya 414 kwa kuwa kwa sasa sheria ya gesi nchini haipo. Hivyo basi, makubaliano katika mkataba baina ya wadau hutakiwa kuwasilishwa EWURA kwa mapitio tu, na baada ya kujiridhisha EWURA hupanga bei za gesi.

Mkataba wa ubia ndiyo mwongozo mkuu wa mahusiano yote yanayohusu uzalishaji na ugawanaji wa mapato ya gesi baina ya TPDC na mbia yeyote. Lakini kwa makusudi wabia na TPDC wamekuwa hawafuati matakwa yaliyomo kwenye PSA na mfano mzuri ni Pan African Energy2.

Mapendekezo ya kamati ndogo iliyoundwa na Bunge toka kwenye iliyokuwa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini ilipendekeza na Bunge kukubali kudurusu Sera ya Nishati, kuandaa muswada wa gesi asili wenye kutoa majibu ya maswali magumu ya Watanzania wa leo na wa miaka 50 ijayo.

Majukumu kati ya asasi moja na asasi nyingine yaainishwe bayana na kutenganishwa kwa lengo la kuleta ufanisi na kuongeza tija.

Aidha, mipango mkakati na kabambe iandaliwe ili kuibua miradi ya miundombinu na mahitaji ya rasilimali.

Taifa likichelewa kuweka nyenzo hizi muhimu, likaruhusu majadiliano na mikataba kuchukuwa nafasi, kipindi si kirefu yatashuhudiwa manung’uniko kuwa nchi imeuzwa na mivutano kati ya wananchi na wawekezaji na ya wananchi na serikali yao itajitokeza kwa nguvu sana jambo ambalo ni vyema likaepukwa mapema.

Mapendekezo haya yalitolewa bungeni Novemba 17, 2011 na kupitishwa kuwa azimio la bunge. Kwa bahati mbaya ama kwa kuzembea, sasa ni mwaka mzima na miezi sita imepita bila utekelezaji na taifa limeshuhudia maandamano na malalamiko ya wazi toka maeneo ambapo gesi asili imegunduliwa.

Licha ya ukweli kwamba gesi asili ilianza kutafutwa toka mwaka 1952, ikiwa imegunduliwa kwa mara ya kwanza nchini mwaka 1974 na baadae mwaka 1982, wakati wote huo hakukuwa na sera mahususi ya gesi hadi mwishoni mwa mwaka 2012 zaidi ya miaka 30 baadae ndipo serikali imeanzisha mchakato wa kutunga sera ya taifa ya gesi asili.

Mikataba kadhaa ya uchimbaji na utafutaji wa gesi imeshatiwa saini kati ya serikali na wawekezaji bila kuwa na sera wala sheria inayotoa mwongozo juu ya namna taifa linavyopaswa kudhibiti rasilimali hii adhimu.

Uwepo wa sera na sheria ya gesi asilia ungetoa mwelekeo juu ya namna gani serikali ingeshirikiana na wakazi wa maeneo yaliyogunduliwa gesi, pamoja na wadau wengine katika kutafuta, kugundua na kuvuna, kusafirisha, kununua na kutumia gesi hiyo asilia. Kukwepa hoja hizi na kubandika zisizokuwepo, ndio kiini cha hasira ya wanaMtwara.

SOURCE: TANZANIA DAIMA

0 comments