Thursday, 3 October 2013

MADHARA YA CHOO CHA KUKALIA

Nyumba nyingi mijini na ofisi mbalimbali zinazojengwa hivi sasa, huwekewa vyoo vya kukaa. Hata zile za zamani zinakarabatiwa na kubadilishwa kwa kuwekewa hivi ambavyo vinaonekana vya ‘kisasa’.

Mgunduzi wa vyoo vya aina hii, Thomas Crapper anasema kwa mtazamo wake aliona kukaa wakati wa kujisaidia ni utambulisho wa ustaarabu na maendeleo.

Hata hivyo, madaktari wanapingana naye wakisema kujisaidia katika vyoo vya kukaa kuna madhara kiafya kwa kuwa mkao huo unaweza kuleta matokeo mbalimbali ndani ya mwili.

Utafiti uliofanywa na mtandao wa ‘naturesplatform’ umegundua kuwa matumizi ya choo cha kukaa huweza kusababisha matatizo mbalimbali ikiwemo kansa ya utumbo mkubwa.

Kwa mujibu wa Mtaalamu wa afya wa gazeti la MWANANCHI , Samwel Shita anasema, madhara ya vyoo vya kukaa ni makubwa kwani wakati mwingine yanaweza kuwa chanzo cha saratani ya utumbo mkubwa kutokana na haja kubwa kubaki kwa muda mrefu katika utumbo huo.

Shita anasema mtu anapojisaidia haja kubwa katika choo cha kuchuchumaa, kinasaidia haja yote kutoka kwa sababu ya msukumo unaosababishwa na mkao huo.

“Unapokaa unakuwa umekaa katika choo mwili unakuwa umelegea, hivyo inabidi utumie nguvu kubwa kujikamua kutoa haja, tofauti na unapochuchumaa,” anasema Shita na kuongeza:

“Matatizo huanza hapo, unapojisaidia ukiwa umekaa na kulazimisha kujikamua unaweza kusababisha vimishipa vidogo katika utumbo mpana sehemu ya haja kubwa ya ndani na ya nje kuvimba na maumivu makali husababishwa na ugonjwa unaojulikana kama ‘hemorrhoid,” anasema.

Anasema ‘hemorrhoid’ ni ugonjwa ambao pia huitwa bawasiri. Mgonjwa hupata uvimbe katika njia ya haja kubwa na hivyo kupata maumivu wakati wa kujisaidia na haja yake mara nyingine huambatana na damu.

0 comments