Kumekuwa na kelele za waumini nchini Ujerumani wakishinikiza askofu huyo afukuzwe kwa kukiuka taratibu.
Vatican City. Makao Makuu ya Kanisa Katoliki Duniani (Vatican) yamemsimamisha kazi Askofu wa Jimbo la Limburg, Ujerumani Franz-Peter Tebartz-van Elst anayekabiliwa na kashfa ya matumizi mabaya ya fedha kwa shughuli za kifahari.
Vatican ilieleza jana kuwa uamuzi huo umechukuliwa baada ya kuridhika kuwa Askofu van Elst amekiuka maadili yaliyowekwa na Papa Francis kwa viongozi walioko chini yake akiwataka waishi maisha ya uchaji, umaskini.
Hadi sasa, kumekuwa na kelele nyingi miongoni mwa waumini nchini Ujerumani wakitaka askofu huyo afukuzwe kazi.
Miongoni mwa matumizi yake makubwa ni ujenzi wa makazi yake binafsi yaliyogharimu Euro 2.9 milioni (Dola 3.9 milioni), ukumbi wa chakula wenye mita za mraba 63 ambao ni pamoja na mesi na bafu yenye thamani ya Euro 15,000.
Askofu van Elst (53) amekuwa akituhumiwa kuendesha miradi hiyo kwenye mji wa kihistoria wa Limburg, ikiwamo makumbusho, kumbi za mikutano, kanisa dogo na nyumba ya makazi yake binafsi.
Fedha hizo zinatokana na mapato ambayo ni misamaha ya kodi kwa vikundi vya kidini nchini Ujerumani kwa mujibu wa sheria.
“Baada ya uchunguzi wa awali, Vatican imeamua kuchukua hatua kumsimamisha na kumwondoa kwenye usimamizi wa jimbo,” ilieleza taarifa hiyo.
“Baba Mtakatifu (Francis) amekuwa akifuatilia kwa karibu mambo yote yanayoendelea katika Jimbo la Limbuerg,” iliongeza taarifa hiyo.
“Hali hiyo imefikia mahali ambako kiongozi huyu hawezi kuendelea kusimamia kazi zake za kitume kama askofu wa jimbo.”
Hata hivyo, taarifa hiyo haikueleza ni kwa muda gani Askofu van Elst amesimamishwa kazi, ila iliongeza kuwa itategemea na kukamilika kwa uchunguzi, tathmini ya hali ya fedha ya jimbo na mambo mengine.
Wiki iliyopita, Askofu van Elst alisafiri hadi mjini Rome, Italia kwa ndege ya shirika la gharama nafuu, Ryanair kujieleza mbele ya Papa Francis – kutokana na madai kuwa alisafiri mwaka jana kwa ndege ya daraja la kwanza kwenda India na pia kutumia vibaya fedha.
Taarifa za matumizi hayo makubwa ya kiongozi huyo zimelitikisa
Kanisa Katoliki la Ujerumani huku wengi wakitaka uwazi katika matumizi
ya fedha -- mageuzi ambayo Papa Francis amekuwa akiyapigia kelele na
kutaka kanisa maskini kwa watu maskini. Miradi hiyo kwa pamoja ambayo
iliidhinishwa na mtangulizi wake awali ilikadiriwa kutumia Euro 5.5
milioni, lakini iliongezeka kwa kiasi cha kutisha na kufikia Euro 31
milioni ikiwamo bustani yenye thamani ya Euro 783,000.
Pia, Askofu Tebartz-van Elst anatuhumiwa kwa kutoa taarifa za uongo mahakamani kuhusu safari yake ya India kutembelea familia maskini.
Waendesha mashtaka wa Serikali wanaeleza kuwa askofu huyo alitoa taarifa za uongo chini ya kiapo kwenye mahakama ya mjini Hamburg dhidi ya gazeti la kila wiki, Der Spiegel akikana safari ya India anakodaiwa kutumia daraja la kwanza. Matumizi makubwa ya askofu huyo yameudhi walipa kodi wa Ujerumani wakidai kwamba wanakamuliwa huku fedha zikitumiwa vibaya na wengi wao kuandamana nje ya makazi ya askofu huyo.
Kansela Angela Merkel, binti wa kiongozi wa zamani wa Kipentekoste amesema kupitia msemaji wake, Steffen Seibert kwamba ana matumaini Kanisa Katoliki litamaliza tatizo hilo kwa jina la Yesu. Askofu Tebartz-van Elst hata hivyo ametetea miradi yote akieleza inalenga kudumisha mila na historia ya eneo hilo.
Tangu kuingia madarakani kwa Papa Francis, kumekuwa na kasi ya mabadiliko ndani ya kanisa.
CHANZO: MWANANCHI
0 comments