Monday, 21 October 2013

Wamiliki shule binafsi waiangukia serikali

WAMILIKI wa shule binafsi wameiomba serikali kuwapunguzia gharama mbalimbali ili kuwapunguzia mzigo wazazi katika kusomesha watoto wao.

Ombi hilo lilitolewa juzi na Mkurugenzi Mkuu wa Shule za Filbert Bayi, Anna Bayi, wakati wa mahafali ya nane ya kidato cha nne yaliyofanyika Mkuza-Kibaha, mkoani Pwani, ambako mgeni rasmi alikuwa Katibu Tawala Mkoa, Beatha Swai.

Bayi alisema pamoja na juhudi nzuri wanazozionyesha katika kusukuma gurudumu la maendeleo kwenye nyanja ya elimu, wanakabiliwa na baadhi ya matatizo na vikwazo kama vile kulipia ukaguzi wa vifaa vya kuzima moto kati ya sh milioni 2 hadi milioni 2.5, mabango ya shule, kodi ya majengo, gharama za ukaguzi huku hawakaguliwi na mitihani ya ‘Mock’ shule za msingi ngazi ya kata, wilaya, mkoa na kanda.

“Ufanyaji wa mitihani hii inayoanza Machi ngazi ya kata, ina kasoro nyingi kama vile, kwa mwezi huo mtoto anakuwa hajafundishwa hata kufikia nusu silabasi, mitihani haina ubora katika utungaji na hatimaye uchakachuaji wa matokeo kwa makusudi, ili kuonyesha shule za kata kwamba ndizo zinafanya vizuri.

Alieleza kuwa shule binafsi zina shirikisho lao (TAMONGSCO), la wamiliki wa shule/vyuo vya binafsi ambapo huwa zinajitungia mitihani ya majaribio kwa gharama zao zenyewe, hivyo zinapoongezeka za ziada inawabidi wambebeshe mzazi.

“Katika utafiti uliofanywa na mtafiti mchumi wa Benki ya Dunia kitengo cha Elimu, Stevele, kuhusu elimu ya Tanzania, aligundua gharama za kumsomesha mwanafunzi wa sekondari ya serikali kwa mwaka ni zaidi ya sh 3,000,000.

“Pia Katibu Mkuu wa Tamongsco, Nkonya, aliwahi kufanya utafiti kwenye shule za Tambaza, Mpwapwa na Tosamaganga na kugundua ni kweli gharama ni hiyo hiyo na shule za msingi ni kati ya sh 700,000 hadi milioni moja na fedha hizi hulipwa na serikali. Je serikali haioni ili kumsaidia mzazi ambaye pia ameshalipishwa kodi mbalimbali atokako ni kuondoa gharama zisizo za lazima kama kodi ya mapato, majengo ya shule, ukaguzi, mabango, Osha na zinamamoto,” alifafanua Bayi.

Akijibu risala jiyo, Swai mbali na kupongeza jitihada za shule hiyo, aliahidi kufikisha sehemu husika changamoto zilizoainishwa.

Katika hatua nyingine, Bayi alisema kutokana na maombi ya wazazi wengi, wameona ni vema kuibadilisha shule hiyo kuwa ya wasichana pekee kuanzia mwaka huu ili kuongeza idadi ya shule za wasichana mkoa wa Pwani.

0 comments