Mzee Bakari (mwenye shati ya bluu) wa Kijiji cha Madanga
wilaya ya Pangani, akipongeza Kituo cha Redio cha Pangani FM kuendeleza
Kiswahili kupitia kipindi cha Lugha ya Kiswahili.
Na.Mwandishi
wetu,
Kikundi cha Wazee
cha MWEHU katika kijiji cha Madanga wilayani Pangani kimeipongeza redio ya
Pangani FM kwa kueleza Kiswahili kupitia kipindi kinachorushwa hewani na
kituo hicho.
Wakichangia
majadiliano ya kikundi kufuatilia usikivu wa vipindi vya kituo hicho, zoezi
linalofanywa kwa pamoja na Redio Pangani FM kwa kushirkiana na Shirika la
Kimataifa la UNESCO, wazee hao wamesema wanafurahishwa sana na kipindi cha
LUGHA YA KISWAHILI kinachorushwa hewani kila Alhamisi jioni na kurudiwa
Jumamosi mchana.
"Kile kipindi cha
Kiswahili kinanikosha sana kwa sababu Kiswahili kinachozungumzwa na vijana
wa sasa sio Kiswahili kizuri kwa mfano 'kasheshe, mkwara'... tofauti na
Kiswahili tulichosoma cha Hekaya za Abunuwasi kinapendeza sana. Nakipenda
kipindi cha Kiswahili kiendelee sana kwa sababu kinaendeleza utashi wa
lugha ya taifa", alisema mzee aliyejitaja kwa jina moja la Mzee
Bakari.
Wamesema Kiswahili
kinachozungumzwa hivi sasa na kizazi kipya kinapotosha kwa kuingiza na
kuondoa baadhi ya maneno, matamshi mabaya kiasi kwamba kinaondoa maana
nzima ya kukuza Kiswahili na kuienzi kama lugha ya
taifa.
Mzee Mwehu (koti la suti) wa kikundi cha wazee cha MWEHU
kijiji cha Madanga, Pangani akitoa mapendekezo yake ya kuanzishwa kipindi
cha wazee chenye lengo la kuibua matatizo
yanayowasibu.
Pamoja na kukisifu
kipindi cha Kiswahili, wazee hao pia wamempongeza mtayarishaji wa kipindi
hicho kwa kusema kwamba yuko makini na umahiri mkubwa katika utayarishaji
na utangazaji wake.
Vipindi vingine
visivyosifiwa ni pamoja na kipindi cha Urithi wa Pangani, Muziki, Michezo
na Taarifa ya Habari.
Zoezi la
ufuatiliaji na tathmini ni miongoni mwa utekelezaji wa mradi wa kuzipa
uwezo Redio 9 za Jamii za kutumia TEHAMA kutayarisha vipindi vya afya,
kilimo na elimu ili kutoa taarifa ya maeneo hayo kwa urahisi na wingi,
unaotekelezwa na UNESCO kwa msaada wa Shirika la Maendeleo la Sweden
(SIDA).
Hata hivyo wazee
hao wamependekeza kuanzishwa kwa kipindi cha wazee jambo ambalo wanasema
kuonekana kusahaulika kwa kuwa wana urithi wa mambo mengi yenye busara
ambayo ni hazina kwa maendeleo ya wanajamii wa Pangani.
"Mimi masikitiko
yangu ni kutokosekana kwa kipindi cha wazee. Tuna matatizo yetu mengi
yanayotusibu lakini hakuna pa kuyasemea. Kwa mfano tuna tatizo la maji
hapa, tumefuatilia kwa viongozi lakini tunazungushwa tu.
Laiti
tungeyazungumza haya kupitia kipindi chetu, tungefikisha ujumbe", alisema
mzee maarufu kwa jina la MWEHU.
Mzee Hadhrina Hatibu Msiagi wa kijiji cha Madanga
akizungumza na Mtangazaji wa Pangani FM, Bi. Maajabu Ali kuhusu umuhimu wa
kuwa na msemaji mahiri wa historia za kale za Pangani wakati wa zoezi la
ufuatiliaji na tathmini lilioendeshwa kwa pamoja na Redio Pangani na UNESCO
hivi karibuni.
Kwa upande wa
kipindi cha Urithi wa Pangani, wamependekeza kuboreshwa kwa kipindi hicho
kwa kumtafuta msemaji anayeijua kwa kina historia ya kale ya Pangani
kinyume cha ilivyo sasa.
Wamesema Pangani
ina utajiri wa historia ya kale lakini anayekiendesha kuzungumzia historia
ya kale ya jana hivyo kuwanyima wanajamii haki ya kujua na ukweli wa
chimbuko lao.
"Kuna mambo mengi
ya kale ya Pangani, lakini siyo yanayozungumzwa, yanayozungumzwa ni ya jana
kwa hiyo tunataka wapatikane watu wazee wanaozijua habari hizo", alisema
Mzee Hadhrina Hatibu Msiagi.
Kijiji cha Madanga
ni miongoni mwa vijiji kongwe vya kwanza kuanzishwa ndani ya wilaya ya
Pangani, kilichoanzishwa karne ya 17. Vijiji vingine ni Mwera, Pangani na
Bushiri.
Kikundi cha Wazee cha MWEHU wakiwa katika picha ya pamoja
na wanaoendesha zoezi la ufuatiliaji na tathmini ya vipindi vya Pangani FM
kijijini Madanga.
Zainul A. Mzige,
Operation Manager,
MO BLOG,
0 comments