
Saudi Arabia imetoa orodha ya majina takriban 50 ambayo imeagiza wasipewe watoto wanaozaliwa nchini humo.
Miongoni mwa majina hayo ni Rama, Amir, Linda, Alice, Maya, Binyamin, na Sandy.
Wizara ya masuala ya ndani nchini humo ilisema marufuku hiyo ilitokana na hali kwamba majina hayo baadhi yanaenda kinyume na utamaduni na dini ya taifa hilo, ni ya kigeni, au ‘hayafai’.
Benjamin ni Binyamin kwa Kiarabu, ambalo ndilo jina la Waziri Mkuu wa Israel ambaye huitwa Benjamin Netanyahu.
Gazeti la Gulf News limesema majina yaliyopigwa marufuku ni ya makundi matatu.
Yale ambayo yanaibua chuki kidini, yale ambayo yanahusiana na ufalme na yale ambayo asili yake si ya Kiarabu au Kiislamu.
Baadhi ya majina ambayo yamo orodhani na hayaonekani kuwa kwenye makundi hayo ni Benjamin na Abdul Naser.
Binyamin katika Uislamu ndiye mwana wa Nabii Yakubu na Kaka yake Nabii Yusufu.
Abdul (au Abdel) Naser, nalo ni jina la kiongozi msifika wa Misri miaka ya 1960 ambaye hakuwa akisikizana na Saudi Arabia.
Majina kama vile Abdul Nabi na Abdul Hussain, ambayo ni ya kawaida katika Washia na baadhi ya Wasuni yana utata kwani yanaweza kufasiriwa kwa njia nyingi tofauti.
Abdul kwa Kiarabu maana yake ni ‘mwabudu wa’ au ‘mtumwa wa’, au 'mja' nalo Nabi maana yake ni ‘nabii’.
Wanaopinga jina Abdul wanasema ‘mwabudu wa’ halifai kwani ni Mungu pekee anaweza kuabudiwa.
Majina mengi ya Kiislamu yenye Abdul huwa yameongezwa mojayapo ya majina 99 ya Mungu kwa mfano Abdul Rahman.
Baadhi ya majina ambayo yamepigwa marufuku yanahusiana na ufalme, mfano Sumuw (muadhama), Malek (mfalme), Malika (malkia) na Al Mamlaka (ufalme).
Baadhi ya majina yaliyo kwenye orodha hiyo hupatikana sana miongoni mwa Waarabu kwa mfano Malak (malaika), Amir (mwanamfalme), Abdul Naser na Jibreel (Gabriel).
0 comments