Tuesday, 11 March 2014

WANAWAKE WAWILI WAFUNGWA JELA BAADA YA KUVAA SKETI FUPI MAHAKAMANI UGANDA

By    
 
Wanawake wawili waliofika mahakamani wakiwa wamevalia sketi fupi (mini skirt) wamefungwa gerezani baada ya jaji kusema mavazi yao yalitatiza mahakama.

Bi Prosy Nasuna alikuwa amemshtaki mwanamke mwingine kuhusu deni la Sh103,182.

Stakabadhi za mahakama zinaonyesha Bi Nasuna alimpeleka Bi Jane Nabukenya mahakamani kwa kwenda kinyume na makubaliano yao alipokosa kumlipa deni lake.

Hata hivyo, alipoenda Bukomansimbi kusikiliza kesi yake wiki iliyopita, yeye pamoja na mshtakiwa walijikuta wakiishia gerezani.

Awali, kulikuwepo manung’uniko na kelele wakati watu waliposema mavazi yao yalipigwa marufuku kwenye sheria ya kukabiliana na ponografia iliyopitishwa hivi majuzi.

Sheria hiyo inasema ponografia inahusu mbinu yoyote ya kuonyesha sehemu nyeti za binadamu hasa kwa minajili ya kutamanisha.

Hali hii ilimpelekea Hakimu Mkuu Catherine Baguma kuagiza wakamatwe kwa kutoheshimu mahakama.

Alisema mahakama haingeweza kuendelea na kesi hiyo ikiwa wawili hao walikuwa wamevaa minisketi.

Bi Baguma aliwahukumu wawili hao kifungo cha masaa matatu gerezani na kuahirisha kesi yao hadi Machi 13.

Mnamo Desemba mwaka jana, bunge la Uganda lilipitisha sheria ya kuharamisha minisketi ambayo inalenga kuweka wazi kosa la ponografia kwenye sheria za nchi hiyo.

Huku baadhi ya wabunge wakidai mswada huo ulikiuka haki za kibinadamu, wengi waliunga mkono Serikali na kuupitisha.


CHANZO: AHBAABUR RASUL

0 comments