MAMLAKA ya Usafirishaji Majini na Nchi Kavu (Sumatra), imetangaza kurejesha safari za daladala kwenda Kivukoni mwishoni mwa mwezi huu.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam juzi, Ofisa Mfawidhi Kanda ya Mashariki, Conrad Shio, alisema daladala zote ambazo zilikuwa zimesitishwa kutoa huduma za usafiri zitaanza kufanya hivyo kutokana na ujenzi wa barabara kumalizika.
Shio alisema wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake ambao muda mrefu walikuwa wakipata adha ya usafiri, hususani waliokuwa wakienda Kigamboni, watakuwa wameepukana na adha hiyo.
Mamlaka hiyo ilisitisha daladala kutoa huduma za usafirishaji abiria wanaokwenda Posta na Kivukoni Septemba 30, mwaka jana, kabla ya kuja kuliruhusu Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (UDA) kutoa huduma maeneo hayo, hali iliyosababisha malalamiko kutoka kwa wamiliki wa daladala, wakidai shirika hilo linapendelewa na mamlaka hiyo.
CHANZO: TANZANIA DAIMA
0 comments