Sunday, 28 September 2014

ARTETA: FA LIMEMBEBA WENGER

KIUNGO wa Arsenal, Mikel Arteta amesema kutwaa Kombe la FA kumesaidia kocha Arsene Wenger kubaki kazini. Wenger alikaa na klabu hiyo ya London Kaskazini kwa miaka tisa bila taji kabla ya kutwaa Kombe la FA na kurudisha hali ya utulivu kwa mashabiki.

Arsenal ilifungwa mabao 2-0 na Hull City katika dakika za kawaida kabla ya kuibuka na kushinda mabao 3-2 katika dakika za nyongeza kwenye mechi hiyo ya fainali.

“Hakuwa na uhakika na hatima yake,” alisema Arteta alipozungumza na Daily Mail.

“Mara zote huwa anasema anataka kubaki lakini hajasaini mkataba, kwenye nusu fainali, hatukujua kitu gani kingetokea.

“Kama tungefungwa na Hull, habari ingekuwa nyingine. “Ilikuwa mechi kubwa katika historia ya Arsenal, tulishinda kombe la kwanza baada ya miaka tisa”.

Alex Oxlade-Chamberlain alionekana katika mechi tano za Arsenal za Ligi Kuu msimu wa mwaka 2013-14, na Arteta alisema mchezaji huyo wa kimataifa wa England alifanya makubwa Emirates.

“Kiwango alicho nacho ni kikubwa, kama ataongeza jitihada, anaweza kufika mbali sana,” alisema Arteta.

“Ana kasi na uwezo wa kuwa winga bora, lakini ana mpango wa kuwa kiungo, na hilo ni gumu sana kulifanikisha".

Arteta pia alimzunguzmia kiungo Mesut Ozil, aliyejiunga na klabu hiyo katika msimu wa ligi wa mwaka 2013-14 ambapo alionekana kumtetea.

Kiungo huyo wa Ujerumani aliigharimu Arsenal pauni milioni 42.4 lakini mchezaji huyo wa zamani wa Everton alisema bingwa huyo wa kombe la dunia ni msanii.

“Unapokuwa na mchezaji kama Ozil pamoja na mambo yote, watu wanaweza kumpenda ama kumchukia,” alisema Arteta.

“Unapokuwa msanii huwezi kucheza zaidi ya mechi 10 kila wiki, ni ngumu kwa mchezaji mbunifu kucheza hivyo”.

0 comments