kUTOKA hABARI LEO
JUKWAA la Katiba Tanzania (Jukata)
limesema Watanzania waachwe huru kwa ajili ya kuijadili
Katiba
Inayopendekezwa ili muda wa kura ya maoni utakapofika waweze kufanya
uamuzi sahihi bila ya kushawishiwa na vyama vya siasa au makundi ya
kidini.
Akizungumza na gazeti hili jana,
Mwenyekiti wa Jukata Deus Kibamba, alisema vyama vya siasa visiingilie
jambo hilo, kwani kuendelea kupiga kampeni kutawafanya Watanzania kupiga
kura ya maoni kwa shinikizo la vyama vya siasa na madhehebu ya dini.
"Sisi msimamo wetu tunataka wananchi
wenyewe waisome katiba hiyo, waielewe halafu waamue kupitia sanduku la
kura," alisema Kibamba.
Kibamba alisema dalili zilivyo sasa ni
wazi kuwa wakati wa upigaji wa kura ya maoni utajaa mvutano kutokana na
wanasiasa na vyama siasa kugawanyika na kuanza kupiga kampeni ya ndio na
hapana dhidi ya Katiba hiyo Inayopendekezwa.
"Nakwambia kutachimbika wakati wa kupiga
kura ya maoni, kama wanasiasa wataendelea na lugha zao za kuipigia debe
na wengine kuibeza," alisema Kibamba na kuongeza kuwa ndio maana
wanampongeza Rais Jakaya Kikwete na vyama vingine vya siasa jambo hilo
lipigiwe kura baada ya Uchaguzi Mkuu.
Alisema jambo hilo likifanyika kabla ya
uchaguzi au wakati wa uchaguzi mkuu, wanasiasa watachanganya wananchi na
akasisitiza kuwa ni vyema Watanzania waachwe waisome Katiba hiyo
inayopendekezwa.
Jukata pia kupitia kwa jarida lao la
robo mwaka, imedai kuwa kauli zilizotolewa na baadhi ya viongozi mara
baada ya Katiba inayopendekezwa kupitishwa zinaweza kuwa na athari kubwa
katiba mchakato wa kupata katiba mpya.
Taarifa hiyo ilisema ni wakati sasa wa
kuachwa kwanza huru kwa Watanzania wenyewe waijadili Katiba
Inayopendekezwa ili waweze kutoa uamuzi sahihi.
“Katiba ni yetu sote hakuna mwenye haki
ya kuandika Katiba kuliko wengine hivyo dhana ya maridhiano na muafaka
ipewe kipaumbele,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Tangu kupitishwa kwa katiba hiyo, baadhi
ya viongozi wa vyama vya siasa wamenukuliwa wakitoa matamko mbalimbali
wengine wakitaka wananchi waikatae katiba hiyo na wengine wakieleza kuwa
inawajali wananchi hivyo waikubali.
Jarida hilo la Jukata lilitoa Kauli ya
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ya kutamani kura ya maoni ifanyike kabla ya
uchaguzi mkuu au pamoja na uchaguzi mkuu kuwa inakwenda kinyume na
makubaliano yaliyofikiwa kati ya Rais Jakaya Kikwete na Kituo cha
Demokrasia Tanzania ya kusitisha mchakato huo hadi uchaguzi mkuu upite.
Aidha, ilisema kauli ya kuomba makundi
maalumu kama vile wafugaji, wakulima na wanawake kuwakumbuka kwa kuwa
masuala yao yamewekwa kwenye Katiba pendekezi ni kauli ambazo tafsiri
yake ni kupiga kampeni kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa na
Serikali Kuu.
Jukata pia imetaja tukio la kutaka
kupigwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman na baadhi
ya wajumbe wa BMK kutoka Zanzibar baada ya kupiga kura ya hapana kuwa
ni jambo la aibu.
Wakati huohuo, Viongozi Wakuu wa Nchi,
Viongozi wakuu wastaafu, Mabalozi, viongozi wa madhehebu ya dini na
viongozi kutoka nje ya nchi wametajwa kuhudhuria sherehe kubwa ya
kihistoria ya kukabidhiwa Rais katiba inayopendekezwa na Bunge Maalumu
la Katiba.
Tukio hilo la kukabidhi rasimu ya Katiba
litafanywa na Rais Kikwete na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Katika mkutano wake na waandishi wa
habari jana, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk Rehema Nchimbi alisema tukio hilo
litafanyika kesho katika uwanja wa Jamhuri na kuwataka wananchi
kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo la kihistoria.
Alisema ni jambo la kumshukuru Mungu
kuona mchakato wa katiba umefanyika kwa amani na utulivu mkubwa bila
vurugu wala kumwaga damu kama ilivyo kwa nchi nyingine.
“Ni jambo la kumshukuru Mungu kwa kubaki
salama kwa kipindi chote cha mchakato wa katiba tofauti na
yanayojitokeza nchi nyingine wakati wa mchakato kama huo,” alisema.
Alisema viongozi wakuu wa kitaifa,
viongozi wa dini, viongozi wakuu wastaafu wa Tanzania bara na Zanzibar,
mabalozi na viongozi wakuu wote watahudhuria katika tukio hilo kubwa la
kihistoria.
Dk Nchimbi alisema sherehe hizo
zitafanyika kuanzia saa sita mchana, lakini milango ya Uwanja wa Jamhuri
itakuwa wazi kuanzia saa 12 asubuhi.
“Wananchi wote wanaalikwa kuhudhuria
shughuli hiyo na kushuhudia tukio hilo kubwa na la kihistoria ambalo
halijawahi kutokea, wananchi wa mkoa wa Dodoma tuna haki na wajibu wa
kuonesha furaha yetu kwa bunge hili la kihistoria limefanyika mkoani
Dodoma pekee na si mahali pengine,” alisema.
Alisema Bunge lilifanyika kwa amani na
utulivu na wananchi kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Jamhuri ni
njia mojawapo ya kuonesha furaha na shukrani kwa Mungu.
Pia alisema kutakuwepo na makundi
mbalimbali kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar na makundi hayo ni
pamoja na wafugaji, wakulima, wavuvi, wanawake, vijana wazee, wachimbaji
madini wadogo, walemavu na wasanii, wananchi na wote ambao katiba
iliyopendekezwa imewagusa.
“Serikali ya mkoa wa Dodoma inatoa mwito
kwa wananchi wote na mikoa ya jirani kuhudhuria kwa wingi ili
kushuhudia tukio hilo kubwa,” alisema.
Alisema tukio hilo kubwa na la
kihistoria litatanguliwa na tukio muhimu na maalumu la kuomba dua na
shukrani kwa kukamilika salama kwa shughuli za Bunge Maalum la Katiba
Mkoani hapa. Alisema dua na shukrani itakafanyika leo katika viwanja vya
Mwalimu Nyerere kuanzia saa 10 jioni.
Alisema viongozi wa Serikali na taasisi zisizo za kiserikali, viongozi na waumini wa dini mbalimbali watahudhuria.
Aidha, alisema kutakuwa na ulinzi wa
kutosha na miundombinu ya usalama ya kitaifa itakuwa Dodoma kuhakikisha
sherehe hizo zinafanyika kwa usalama na utulivu mkubwa.
Pia alisema tukio kama hilo linategemewa kufanyika huko Zanzibar.
Alipohojiwa na waandishi wa habari kwa
nini makabidhiano hayo yanafanyika Uwanja wa Jamhuri na si Ikulu ya Rais
iliyopo Chamwino, Dk Nchimbi alisema hilo limetokana na unyeti wa tukio
hilo ambalo limeonesha watu wengi wanahitaji kuhudhuria na kushuhudia
rasimu hiyo ikikabidhiwa.
Pia alipohojiwa ni viongozi gani kutoka nje ya nchi watakaohudhuria makabidhiano hayo alisema bado hana taarifa kamili.
“Kama watakuwepo mtawaona siku ya tukio bado sina taarifa kamili juu ya viongozi wan chi za nje au wawakilishi wao,” alisema.
Waislamu waaswa wasiandamane Wakati huo
huo,Waislamu nchini wametakiwa kutowasikiliza baadhi ya watu
wanaowashawishi kuandamana juu ya suala la Mahakama ya Kadhi kwani jambo
hilo linafanyiwa kazi ambapo Waziri Mkuu Mizengo Pinda amewaahidi
kuhakikisha mambo yao yanaingizwa kwenye katiba.
Akizungumza wakati sikukuu ya
Idd-ul-Adha mkoa wa Pwani iliyofanyika mjini Kibaha, Mbunge wa Jimbo la
Mafia Abdulkarim Shah ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye Baraza la Idd
alisema Waislamu wasikubali kuingia kwenye mtego huo wa maandamano
kupinga katiba.
Shah alisema kuwa serikali ni sikivu na
kupitia kiongozi wake mkubwa haiwezi kwenda kinyume na makubaliano
waliyokubaliana ambapo Waziri Mkuu alisema suala lao linashughulikiwa
hivyo ni vema Waislamu wakawa na subira.
“Msikubali kutumika kwani kuna baadhi ya
watu wanataka kutumia suala la Kadhi kufanya maandamano jambo ambalo
linaweza kuleta uvunjifu wa amani ya nchi na wanapaswa kuheshimu kauli
zinazotolewa na viongozi wao za kudumisha amani,” alisema Shah.
Alisema kuwa kupitia viongozi wao wa
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) waumini wa dini hiyo wanapaswa
kupeleka hoja zao na si kwenda kinyume, ikiwa ni pamoja na kuandamana
kwani kila jambo lina wakati wake.
Imeandikwa na Shadrack Sagati, Sifa Lubasi na John Gagarini.
0 comments