Profesa Jay, ambaye alikuwa akisaidiana na msanii mwenzake Mbunge wa Mbyea Mjini Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, walikuwa wakitambulisha nyimbo yao inayokwenda kwa jina la M4C, ambayo wataiimbia katika ziara iliyopewa jina la M4C Tour itakayoanza hivi karibuni.
Viongozi, wanachama na waalikwa wengine, walianza kushangilia mara tu mshehereshaji wa uzinduzi wa CHADEMA Mtandao, Ester Wasira alipowataka Profesa Jay na Sugu wapande jukwaani kutumbuiza kidogo na kuelezea namna watakavyofanya ziara yao ya nchi nzima.
Kelele za kushangilia na kuonyesha vidole vitatu zilisikika wakati wasanii hao wakichana mistari ya kuwataka Watanzania na wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kutekeleza yale waliyokubaliana katika muungano wao Oktoba 26 mwaka huu pale Jangwaji jijini Dar es Salaam.
“Kama nilivyopiga katika ‘movement’ ya Antvirus nitakuwa balozi tena kwenye ‘movement’ hii itakayokwenda nchi nzima kuhamasisha vijana kujiandikisha kwenye ‘BVR’ pamoja na kuikataa katiba ya vijisenti … hii ni zaidi ya tamasha la muziki ‘stay tuned’ inaanza ‘soon’ tu,” alisema Sugu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe, Programu ya CHADEMA Mtandao, imelenga kuwawezesha Watanzania kujiunga na chama hicho kwa njia ya mtandao ili waweze kupata habari na kuchangia kwa ajili ya mabadiliko.
Uzinduzi wa CHADEMA Mtandao, ulirushwa moja kwa moja na televisheni ya ITV katika ukumbi wa Serena Inn jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na uwakilishi wote wa vyama vya siasa vinavyounda UKAWA ambavyo ni NLD, CUF na NCCR-Mageuzi.
0 comments