Sunday, 5 July 2015

BASATA WAMTEMBELEA BANZA STONE

By    
WA T E N D A J I wa Baraza la Sanaa la Taifa ( B A S A T A ) wakiongozwa na Kaimu Katibu Mtendaji, Vivian Shalua jana walimtembelea msanii na mwimbaji wa muziki wa bendi, Ramadhan Masanja ‘Banza Stone’ ambaye kwa muda sasa amekuwa akiugua nyumbani kwao maeneo ya Sinza jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya Basata kwa vyombo vya habari jana ilisema kuwa lengo la ziara hiyo ilikuwa kumjulia hali msanii huyo mahiri wa bendi na kushauriana na familia yake juu ya namna bora ya kusaidia matibabu yake na kuhakikisha anapata huduma zote stahiki kulingana na maelekezo ya daktari wake.

Katika ziara hiyo, kwa mujibu wa Basata, watendaji hao wakiwa na Mkurugenzi wa Kampuni ya African Stars Entertainment (ASET) Asha Baraka, walipata wasaa wa kufanya mazungumzo na familia ya mwanamuziki huyo ili kupata maendeleo ya afya yake, matibabu na mwenendo wake.

Wanafamilia hao Banza Stone wakiongozwa na kaka yake, Khamis Ally Masanja walieleza kwamba hali ya mgonjwa huyo imekuwa ikibadilika mara kwa mara na kwamba amekuwa akipata matibabu katika Hospitali ya Palestina iliyoko Sinza jijini Dar es Salaam.

Aidha amekuwa akipelekwa hospitali mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam ikiwemo ya Manispaa ya Kinondoni, Mwananyamala ambako anaendelea kutibiwa kwa sasa.

Baada ya kupata taarifa ya kina kuhusu afya ya msanii Banza Stone, watendaji wa Basata kwa kushauriana na wanafamilia hao walifunga ziara kwenda Hospitali ya Palestina, Sinza ambayo pia amekuwa akitibiwa na kufanya utaratibu wa matibabu ili kuhakikisha anapewa huduma stahiki na kuhakikisha afya yake inaimarika.

Akizungumza hospitalini hapo, Kaimu Katibu Mtendaji wa Basata, Shalua alitoa mwito kwa wadau wa sanaa na wasanii kwa ujumla kumwombea Banza Stone na kujitolea kwa hali na mali katika kuhakikisha anarejea katika hali yake ya zamani na hatimaye kurudi kwenye majukwaa ya maonesho.

chanzo: habari leo

0 comments