Tuesday, 18 August 2015

CC YA CCM YATHIBITISHA ANGUKO LA MAWAZIRI

By    
Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye
KAMATI Kuu (CC) ya CCM jana ilikamilisha uteuzi wa wagombea ubunge katika majimbo 11 yaliyokuwa na dosari ambapo sasa wabunge wa zamani, Profesa Peter Msolla, Dk Binilith Mahenge, Dk Seif Rashid, Vita Kawawa, Gaudence Kayombo na Dk Titus Kamani wamekwama katika kutetea nafasi hiyo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM iliamuru kurejewa kwa kura za maoni katika majimbo hayo 11 kutokana na dosari mbalimbali zilizojitokeza wakati wa kura hizo zilizopigwa na wanachama wa CCM matawini katika majimbo Agosti mosi mwaka huu.

Katika kura hizo za marudio, wabunge hao wa zamani walishindwa kufurukuta baada ya kushindwa na wagombea wenzao na sasa hatima yao ilibaki kwa Kamati Kuu ambayo ilikutana jana katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete.

Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye aliwaambia waandishi wa habari jana saa 9.30 alasiri kuwa kikao hicho kingeendelea baada ya wakati huo kuwa mapumziko, lakini kilikuwa kimefanya uteuzi katika majimbo tisa kati ya hayo 11, huku majimbo ya Kiteto mkoani Manyara na Singida Mashariki mkoani Singida yakitarajiwa kufanyiwa uteuzi baadaye jana kwa kuwa wakati huo mambo yake yalikuwa hajakaa vizuri.

Aliwataja waliongoza kura za maoni na kupitishwa na Kamati Kuu jana ni Jerry Silaa (Ukonga, Dar es Salaam), Edward Mwalongo (Njombe Kusini, Njombe), Venance Mwamoto (Kilolo, Iringa), Dk Raphael Chegeni (Busega, Simiyu), Edward Ngonyani (Namtumbo, Ruvuma), Mohamed Mchengerwa (Rufiji, Pwani), Dk Norman Sigalla (Makete, Njombe), Martin Msuha (Mbinga Vijijini, Ruvuma) na Joel Mwaka (Chilonwa, Dodoma).

Katika kinyang’anyiro hicho, Silaa ambaye pia ni Meya wa Ilala na Mjumbe wa Kamati Kuu, alimshinda mfanyabiashara maarufu wa Dar es Salaam, Ramesh Patel, Mwamoto alimshinda Profesa Msolla, Ngonyani akambwaga Vita Kawawa, Dk Rashid ambaye ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii akang’olewa na Mchengerwa na Dk Sigalla akamshinda Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Mahenge.

Aidha, Msuha alimshinda Kayombo wakati Dk Chegeni alimshinda Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Mwenyekiti wake wa CCM Mkoa wa Simiyu, Dk Kamani ambaye inaelezwa kuwa marudio hayo ya kura za maoni yaligubikwa na fujo zilizoanzishwa na wafuasi wa waziri huyo aliyewania urais kupitia CCM mwaka huu.

Dk Chegeni jana alikuwapo katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu wakati kikao cha Kamati Kuu kikiendelea, na pia walikuwapo viongozi wengine wa CCM wa Kiteto na Manyara wakiwamo Mbunge wa Kiteto, Benedict ole Nangoro, Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Umbulla na Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka.

Nape alisema baada ya uteuzi wa majimbo ya Kiteto na Singida Mashariki ambalo mchakato wake wa awali ulifutwa na kutangazwa upya, Kamati Kuu ingeingia katika ajenda nyingine za kuelekea Uchaguzi Mkuu ambao kampeni zake zinaanza Jumamosi hii hadi Oktoba 24, siku moja kabla ya Watanzania kupiga kura kumchagua Rais wa Awamu ya Tano, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani.

Aidha, Nape alisema CCM itafanya tathmini ya mchakato wa kura za maoni baada ya Uchaguzi Mkuu kuona mchakato huo ulivyokwenda kwani imekuwa ikifanya hivyo kila wakati wa uchaguzi na haitakurupuka sasa kutoa tathmini ambayo haijafanyiwa kazi kwani wanahitaji muda zaidi.

Chanzo: Habari Leo

0 comments