Sunday, 16 August 2015

TET YAPUNGUZA IDADI YA MASOMO SHULE MSINGI

By    
Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imetangaza kuboresha mitaala kuanzia darasa la tatu na la sita  na kupunguza idadi ya masomo kutoka 11 kufikia saba.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TET ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ubunifu na Ukuzaji wa Mitaala, Dk. Wilberforce Meena, aliwaambia waandishi wa habari wakati akizungumzia majukumu ya Taasisi hiyo na mafanikio katika kuandaa na kuboresha mitaala nchini.

Alisema kuwa mtaala huo utapunguza masomo na maudhuu yaliyopo kwenye masomo ili kumuwezesha mwanafunzi kufanya vizuri darasani.

Aliyataja masomo hayo saba kuwa ni Kiswahili, Kingereza, Hisabati, Sayansi na Teknolojia, maarifa na jamii, Uraia na maadili pamoja na dini. Alieleza kuwa kutakuwa na somo la michezo ambalo litatumika kama kuibua vipaji vya wanafunzi katika shule. 

Alisema maboresho hayo ya mitaala wameyafanya kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa elimu   295 wakiwemo walimu, maafisa elimu, wanafunzi, watunga sera na bado wanaendelea kupokea maoni kuhakikisha mtaala unakidhi mahitaji.

Meena alisema yalitokea malalamiko ya wanafunzi kujiunga na kidato cha kwanza bila kujua kusoma ama kumaliza elimu ya msingi bila kujua kusoma wakafanya utafiti na hatimaye kubadili mitaala. 

Meena alisema kwa shule ambazo zinafundisha kwa Kiingereza wanatakiwa kufuata mitaala  waliyowaandalia licha ya kudaiwa kufundisha mambo mengi.

Alisema tayari wametoa mafunzo kwa walimu 32,000 kuhusiana na mitaala hiyo kwani ya awali walishindwa kuitekeleza kwa kuwa hawakuwa na uelewa.

Hata hivyo, Meena alisema vitabu vya kiada na ziada ambavyo vilikuwa vinalalamikiwa kuwapo na matatizo ni kuwa wapo katika mchakato wa kuvikusanya   shuleni na kuviangalia ubora wake.

Alisema vitabu hivyo vingi vipo masokoni vilivyolalamikiwa  kuviondoa vyote sokoni kwa haraka hawataweza, hivyo baada ya muda vitaondolewa. 

Aliwashauri watungaji wa vitabu kuhakikisha wanaanda vitabu vyenye ubora ili viuzike na nje ya nchi na sio kuishia kwenye soko la ndani.


CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

0 comments