Tuesday, 13 October 2015

DANGOTE 'KUFUMUA' BANDARI YA MTWARA

By    

UWEZO wa bandari ya Mtwara unatarajiwa kuongezeka mara dufu kufuatia kufunguliwa rasmi kwa kiwanda cha saruji cha Dangote ambacho ni kikubwa kuliko vyote Afrika Mashariki.

Kiwanda hicho kilichojengwa kwa thamani ya dola za Kimarekani milioni 600 (Sh trilioni 1.2) na tajiri namba moja katika bara la Afrika, Alhaji Aliko Dangote, kitatumia bandari ya Mtwara katika kusafirisha saruji yake kwa mauzo ya nje na pia kuingiza baadhi ya malighafi zitakazotakiwa katika uzalishaji wa saruji, miongoni mwa bidhaa nyingine zitakazokuwa zinapita bandarini hapo.

Ili kufanikisha hilo, tayari Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imeshakabidhi kiasi cha hekta 26 kwa kiwanda cha Dangote kwa ajili ya ujenzi wa gati litakalohudumia shehena hiyo katika kijiji cha Mgao, wilayani Mtwara.

Hatua hiyo ni moja ya mipango ya kupanua bandari hiyo ambapo pia magati mengine manne yatajengwa. Wakati gati la Mgao litajengwa na Dangote, magati mengine manne yatajengwa na serikali ya Tanzania.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadh Massawe alisema jana kuwa ujenzi wa magati hayo manne utafanywa kwa awamu kuanzia mwaka huu wa fedha. Wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho kitakachokuwa kinazalisha tani milioni 3 za saruji kwa mwaka, Rais Jakaya Kikwete alisema njia bora ya kukuza uchumi ni kwa uwekezaji kama huo ambao unafungua milango ya kuzalisha ajira mpya na kuongeza uwigo wa kodi.

Rais Kikwete alisema kuwa uwekezaji huo unakuja wakati muafaka sana ambapo mahitaji ya saruji yanaongezeka kwa kasi kubwa nchini na katika nchi jirani kutokana na kukua kwa kasi kwa sekta ya ujenzi.

Ukuaji wa sekta ya ujenzi ulikuwa kwa asilimia 7 mwaka 2005/2006 hadi 12.5 mwaka 2014/2015 hapa nchini. Katika hotuba yake, Alhaji Dangote alishukuru TPA na taasisi nyingine za serikali kwa kufanikisha uwekezaji huo ndani ya miaka miwili baada ya kuwekwa jiwe la msingi.

Chanzo: Habari leo

0 comments