Monday 12 October 2015

TAMASHA LA MTOTO KIKE LAFANA, LATOA KAULI NZITO

By    

Mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Kike Duniani Mkurugenzi wa watoto kutoka Wizara ya Jamii, Jinsia na Watoto Bi. Margaret Sawe Mussai akiwaasa watoto wa kike kuzingatia elimu kwani ndio nguzo ya msingi katika maisha yao wakati w siku ya Mtoto wa Kike Duniani iliyofanyika katika viwanja vya shule ya Tandale jijini Dar. (Picha na Geofrey Adroph wa Pamoja Blog).
Na Mwandishi wetu
WAKATI serikali imekiri kwamba pamoja na kuwa na sheria kali za kuzuia ukatili kwa watoto bado kuna matukio mengi yanayowanyima watoto uhuru na haki zao msingi,wadau mbalimbali walioshiriki tamasha la mtoto msichana wamewataka wasichana kutimiza ndoto zao.
Katika tamasha hilo lililofanyika katika shule ya msingi Tandale, wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es salaam kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa nane vipaji mbalimbali vya watoto vilioneshwa na watoto nao kutoa kauli zao za kutaka haki na ustawi wao kwani wao ni taifa la sasa.
Pamoja na watoto hao kutoa ushuhuda na kuonesha njia ya kusaidiwa, Mkurugenzi wa watoto kutoka wizara ya maendeleo ya jamii , jinsia na watoto Margaret Sawe Mussai pamoja na kuwaambia watoto na jamii kutumia simu 119 kuelezea ukatili, ametaka madawati yaliyopo Polisi kutumika vilivyo kukabiliana na vitendo hivyo.
Alisema lazima wazazi na walezi wawajibike katika kulinda watoto kwani taarifa zilizopo sasa haziridhishi hata kidogo.
Alisema taarifa zilizopo watoto wa kike asilimia 29 na wavulana asilimia 13 wamenyanyaswa kijinsia wakati wasichana asilimia 14 na wavulana asilimia 6 wamekabiliwa na tatizo la kujaribiwa kuvurugwa kijinsia.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) Bi. Natalia Kanem akizungumza jambo kwenye siku ya Mtoto wa Kike Duniani iliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Tandale jijini Dar.
Akizungumzia suala la mimba za utotoni alisema kwamba wizara imeandaa program za kukabiliana na mimba na ndoa za utotoni huku akisema kwamba sheria ya ndoa ya mwaka 1971 iko mbioni kubadilishwa ili kupandisha umri wa kuolewa kuwa miaka 18.
Aidha alisema serikali na wadau wengine wanaendesha mafunzo ya kuwatoa watoto katika mazingira hatarishi pamoja na kusaidia wazazi vijana ambao walikatisha shule kutokana na ujauzito.
Mkurugenzi huyo pamoja na kueleza changamoto za malezi na ulinzi kwa watoto amesema sera zilizopo zinaendelea kuboreshwa ili kutoa ulinzi zaidi katika kuhakikisha taifa linakua na watoto wenye uhakika wa usalama.
Naye Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu UNFPA Dk. Natalia Kanem alisema mtoto msichana anahitaji kushikilia ndoto yake pamoja na changamoto zinazojitokeza.
Alisema pamoja na kuwepo kwa vikwazo vya mawasiliano , mtoto wa kike anastahili kupewa taarifa mbalimbali zinazomweka huru katika mambo ambayo yanamhusu yeye na jamii yake.
Alisema pamoja na haja ya kuwepo kwa usawa wa kijinsia, mtoto wa kike ni lazima apate haki yake ya kusoma,kutodhuriwa na utamaduni uliopitwa na wakati ambao ni kandamizi kama kukeketwa na ndoa za utotoni na kutobaguliwa.
Msaidizi wa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) nchini Tanzania Bi. Hashina Begum akisoma risala kwenye siku ya Mtoto wa Kike Duniani iliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Tandale jijini Dar. Aliwataka watoto wa kike kuhakikisha kwamba wanasoma kwa kuwa elimu ni kila kitu na wakishakuwa na elimu watajiamini na kujitambua. Alisema ipo haja ya kuimarisha mfumo wa ulinzi kwa watoto wa kike ili kupata nafasi ya kusonga mbele na wale ambao wamekatishwa masomo kwa sababu mbalimbali kurejea darasani ili kupata elimu na uwezo wa kuendelea mbele. Alisema kw akuunganisha nguvu kati ya serikali, mashirika ya umoja wa mataifa na wadau mbalimbali wa maendeleo na mtoto wa kike,watoto wa kike watapata nafasi kubwa ya kusonge mbele. Aliwataka watoto wa kike kujitambua kwamba wao ni wazuri lakini wanapaswa kujiheshimu na kuwaheshimu wengine kwa ajili ya mustakabali wa maendeleo yao. “Wale wanaoapata mimba, wale wanaokatishwa masomo ni lazima wapate njia ya kujiendeleza tena” alisema Dk Natalia.
Angel Benedicto ambaye alikuwa ni mfanyakazi wa ndani akieleza alipotokea mpaka kufika alipo sasa wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike yaliyofanyika siku ya Jumamosi. Katika tamasha hilo wasichana wawili walitoa ushuhuda, Binti mdogo Eva Tolage ambaye alimwandikia barua Rais Barak Obama akihoji Marekani na yeye binafsi rais Obama na viongozi wa dunia watafanya nini kumsaidia mtoto wa kike anayekabiliwa na changamoto nyingi hasa wale wa vijijini. Eva alimwambia Barack Obama kwamba anataka kutimiza ndoto yake ya kuwa askari kusaidia jamii, lakini atafikiaje ndoto hiyo wakati kuna changamoto ya umeme na huku baba yake kazi anazofanya hazimpi kipato cha kutosha. Msichana huyo ambaye aliandika barua kwa ujasiri mkubwa akihoji maendeleo endelevu yasiyompita binti mdogo alijibiwa na Rais Obama na kutajwa katika hotuba yake kwenye Umoja wa Mataifa kwamba viongozi wa dunia akiwemo Barack Obama mwenyewe wamemsikia na watahakikisha tatizo la wasichana wa Afrika na kwingine kokote linaondolewa na na wanapata nafasi ya kushiriki katika maendeleo.
Eva Tolage aliyeandika barua kwa rais Barack Obama wa Marekani na barua yake kusomwa katika mkutano wa viongozi wa dunia makao makuu ya Umoja wa Mataifa alitumia mkutano huo kusoma machache aliyoandika. Katika barua hiyo, Eva mwenye umri wa miaka 15, alielezea jinsi ambavyo bado mazingira mtoto ni mabovu na hatarishi kiasi cha kumfanya ashindwe kupata elimu bora, pia kuwa katika hatari ya kukumbwa na vitendo vya kikatili ikiwa ni pamoja na ubakaji. Aidha binti mwingine Angela Benedicto ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Wote sawa alisimulia matatizo ya wasichana wa kazi,adha zao kutoka kwa wanaume na watoto wa kiume wanakofanyia kazi. Alisema kwamba mateso wanayoyapata wasichana wa kazi yanastahili kukoma na kwamba ipo haja ya kuwekwa kwa mfumo unawalinda. Alisema serikali ina wajibu wa kuwatetea wasichana kupata haki zao, sio tu kusema shule bure, lakini pia kujenga kujiamini kwa wasichana katika kutimiza ndoto zao. Alisema sababu za kuwepo kwa wasichana wengi wakazi za ndani ni dhuluma inayoambatana na umaskini katika familia na tamaduni zinazomweka nyuma mtoto wa kike kiasi cha kulazimika kutafuta kazi za ndani ambazo waajiri wanakuwa hawana staha. Katika tamasha hilo kulikuwa na shughuli mbalimbali zikiwemo za kuangalia hali ya afya ya uzazi, elimu ya afya ya uzazi, kupimwa maambukizi ya UKIMWI na kukaguliwa kwa saratani ya matiti na kizazi pamoja na elimu yake. Pia kulikuwa na michezo ya kuigiza na sarakasi na mwanamuziki wa kike mwasiti alichombeza kwa nyimbo zake za uadilifu. Siku ya Mssichana duniani huadhimkishwa Oktoba 11 lakini kwa Tanzania iliadhimishwa Oktoba 10.
Mgeni rasmi pamoja na vingozi wengine wakiwa kwenye picha ya pamoja na wasichana wenye ulemavu wa ngozi katoka maadhimisho ya siku wa mtoto wa kike.
Watoto wakiwa na hali ya furaha wakati wa maadhimisho hayo yaliyofanyika katika shule ya msingi Tandale.
Watoto wa kike wakionesha vipaji katika mpira wa miguu wakati wa siku ya mtoto wa kike Duniani.

Mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Kike Duniani Mkurugenzi wa watoto kutoka Wizara ya Jamii, Jinsia na Watoto Bi. Margaret Sawe Mussai (wa kwanza kulia) akivuta kamba pamoja na wanafunzi wa kike huku Msaidizi wa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) nchini Tanzania Bi. Hashina Begum (wa kwanza kushoto) akiungana na timu ya wanaume ambapo timu ya wasichana iliibuka kidedea.
Msanii wa muziki wa kizazi kipya nchini Mwasiti akitoa burudani wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Tandale.
Vijana wa Temeke wakiendelea kutoa burudani.
Wanafunzi wa kike kutoka shule mbalimbali wakipatiwa elimu ya afya na uzazi katika mabanda yaliyopo kwenye maadhimisho hayo.
Sehemu ya wanafunzi kutoka shule mbalimbali walioshiriki maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani.
Elimu mbalimbali zikitolewa uwanjani hapo.
Burudani ya nyimbo kutoka kwa wanafunzi.
Wanafunzi wakipitia kumbukumbu mbalimbali kwenye madaftari yao.
Mmoja wa wanafunzi akijibu swali.
DSC_0524
Picha ya pamoja katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Tandale.
Mgeni rasmi na Mwakilishi wa Shirika la UNFPA pamoja na wadau wanaotetea masuala ya haki ya mtoto wa kike kwenye picha ya pamoja katika bango maalum.
Maagizo mbalimbali yanayoonyesha unyanyasaji kwa mtoto wa kike.
Wasanii wakifikisha ujumbe kwa njia ya maigizo.
Umati wa wanafunzi waliohudhuria siku ya mtoto wa kike duniani.
Wanafunzi wakifuatilia matukio mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea kwenye siku ya mtoto wa kike duniani.
Baadhi ya wanafunzi wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa maadhimisho hayo.
Mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Kike Duniani Mkurugenzi wa watoto kutoka Wizara ya Jamii, Jinsia na Watoto Bi. Margaret Sawe Mussai (kushoto) na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) Bi. Natalia Kanem ( wa pili kushoto) katika picha ya pamoja na watoa huduma katika mabanda yaliyokuwepo kwenye maadhimisho hayo.
Mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Kike Duniani Mkurugenzi wa watoto kutoka Wizara ya Jamii, Jinsia na Watoto Bi. Margaret Sawe Mussai pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) Bi. Natalia Kanem wakisaini vitabu vya wageni kwenye banda mojawapo walilotembelea.
Mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Kike Duniani Mkurugenzi wa watoto kutoka Wizara ya Jamii, Jinsia na Watoto Bi. Margaret Sawe Mussai pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) Bi. Natalia Kanem wakipata maeleozo na kukagua shughuli mbalimbali zinazoifanywa na vijana wa Restless wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike Duniani.
Mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Kike Duniani Mkurugenzi wa watoto kutoka Wizara ya Jamii, Jinsia na Watoto Bi. Margaret Sawe Mussai (wa pili kutoka kulia) akipata maelezo kutoka kwa wasichana wajasiriamali alipokuwa anatembelea mabanda.
Burudani nayo haikuwa mbali katika kusherehesha siku ya mtoto wa kike duniani.

0 comments