Thursday, 1 October 2015

UKAWA WADAI KUSHTUKIA GOLI LA MKONO NEC

By    
Mkurugenzi wa NEC, Ramadhani Kailima.
Siku moja tu baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva, kuvitaka vyama vya siasa kuacha kuituhumu, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umeibuka na kudai umeshtukia kuwapo kwa dalili za kuhujumiwa kwa kura za wagombea wao katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika (pichani), alisema dalili za kuwapo kwa vitendo hivyo alivyoviita ni ‘bao la mkono’ lililowahi kutajwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kitendo cha NEC kutowapa wao na vyama vingine nakala ya Daftari la Kudumu la Wapigakura wakati zikiwa zimebaki wiki tatu tu kabla ya uchaguzi na pia wao (vyama shiriki) kutojua mfumo wa kupokea na kutangaza matokeo ya urais utakavyofanya kazi.

Ukawa unaoundwa na Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, umemsimamisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuwa mgombea wao wa urais atakayechuana na Dk. Magufuli wa Chadema.

Mnyika aliitaka NEC iunde kamati maalum ya watalaam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kutoka vyama vya siasa ili wakaangalie namna kanzidata (Database) ya tume hiyo itakavyofanya kazi kwani kuendelea kuficha kunalenga kubariki hujuma dhidi yao.

Kadhalika, alisema uhakiki wa daftari umeshafungwa lakini hadi sasa NEC haijaeleza kuna watu wangapi watakaopiga kura Oktoba 25.

KAULI YA NEC
Akizungumzia tuhuma hizo za Ukawa, Mkurugenzi wa NEC, Ramadhani Kailima, alisema miaka yote tume imekuwa wazi na hakuna sababu ya vyama kuwa na hofu.

Alisema NEC itatoa nakala ya Daftari la Kudumu la Wapiga kura kwa vyama vyote vya siasa na pia alikubali ombi la Chadema kutaka wapeleke watalaamu wao wa Tehama ili kuangalia mfumo wa kupokea na kutangaza matokeo unavyofanya kazi.

CHANZO: NIPASHE

0 comments