Sunday, 3 January 2016

MAMBO 10 YATAKAYO TAWALA VICHWA VYA HABARI AFRIKA MWAKA 2016

By    

Mwaka 2016 unatarajiwa kushuhudia mambo mengi kuanzia katika siasa, ambapo nchi nyingi zitafanya uchaguzi, hadi michezoni.

Mwandishi wa BBC Abdinoor Aden ameandaa orodha ya mambo 10 makuu yanayotarajiwa kuteka vichwa vya habari barani mwaka huu.

1. Uchaguzi mkuu Uganda


Raia nchini Uganda watashiriki kwenye uchaguzi mkuu 18 Februari. Rais Yoweri Museveni, ambaye ameongoza taifa hilo tangu 1986, atawania akilenga kuongoza kwa muhula mwingine. Wapinzani wake ni kiongozi wa muda mrefu wa upinzani Kizza Besigye na aliyekuwa waziri mkuu Amama Mbabazi.

2. ‘Fagia fagia’ ya Magufuli Tanzania


Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli amekuwa madarakani kwa miezi miwili tu na katika kipindi hicho amebadilisha mambo mengi.

Magufuli ameanza uongozini wake kwa kubadilisha mambo mengi na kutengua uteuzi wa maafisa wa mashirika ya serikali

Tarehe 1 Januari, aliwaapisha makatibu wakuu wa wizara na kukamilisha serikali yake hivyo basi mwaka huu serikali yake inatarajiwa ‘kufanya kazi’. Tayari ametoa mwelekeo tofauti kuhusi matumizi ya pesa za serikali na utendaji kazi wa watumishi wa umma. Mambo yatabadilika? Bila shaka yeye ni mmoja wa watakaotupiwa macho sana mwaka huu.

3. FIFA kuongozwa na rais kutoka Afrika?


Bw Sexwale ndiye Mwafrika pekee anayewania kumrithi Sepp Blatter
Raia wa afrika kusini, Tokyo Sexwale, ni mmoja wa waliooidhinishwa kuwania urais wa shirikisho la soka duniani FIFA. Wengine ni Ali Al Hussein (Jordan), Sheikh Salman Bin Ebrahim Al Khalifa (Bahrain), Jérôme Champagne (Mfaransa), Gianni Infantino (Mwitaliano/Mswizi). Uchaguzi utafanyika tarehe 26 Februari. Atafanikiwa?

4. Uchaguzi Somalia, Gambia, Niger, DR Congo


Macho yote yataelekezwa nchini Somalia ambapo ifikapo mwezi Septemba, Serikali ya Rais Hassan Sheikh Mohamud itakamilisha muhula wake. Mwisho wa muhula wake wa kwanza utakuwa ni mwanzo wa uchaguzi nchini humo. Uchaguzi huo utakuwa ni muundo tofauti na njia ya wapigaji kura inayotumika na raia wa mataifa wengine Afrika. Mazungumzo yanaendelea kuamua mfumo utakaotumika. Kando na Somalia, kutakuwepo pia na uchaguzi Gambia na Niger. Rais wa Gambia Yahya Jammeh atawania tena?

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, uchaguzi mkuu pia unatarajiwa Novemba lakini kumekuwepo na wasiwasi kutokana na maandalizi. Je, utafanyika au utaahirishwa?

5. Mazungumzo ya Burundi


Hali nchini Burundi imekuwa tete kutokana na machafuko yaliyoanza baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza angewania urais kwa muhula mwingine, na baadaye jaribio la mapinduzi lililofeli. Watu zaidi ya 300 waliuawa kufikia Desemba na jamii ya kimataifa ikaelezea wasiwasi wa kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe au hata mauaji ya kimbari. Viongozi wa kanda wamefufua juhudi za kutafuta amani na chini ya uongozi wa Rais Museveni, wahusika walikutana Uganda. Iliafikiwa mazungumzo kamili yafanyike mjini Arusha, Tanzania tarehe 6 Januari. Upande wa serikali umepinga hilo. Wengi watasubiri kuona yatakayojiri.

Rais Museveni ndiyo anayeongoza mashauriano ya kutafuta amani Burundi

6. Waafrika mahakamani ICC


Mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC inatarajiwa kuendelea na kesi tofauti za uhalifu wa kivita dhidi ya Waafrika kadha. Miongoni mwao ni Naibu rais wa Kenya, William Ruto na mwanahabari, Joshua Arap Sang. Tarehe 18 Januari, kiongozi wa zamani wa waasi Germain Katanga anatarajiwa kujua hatima yake kwani siku hiyo itakuwa ya mwisho ya kifungo chake.

Kiongozi wa zamani wa Ivory Coast Laurent Gbagbo ni miongoni mwa wanaotarajia kesi zao zianze ICC mwaka huu.

7. Mgogoro wa kisiasa Libya


Mwezi mmoja baada ya mikakati ya upatanishi kuzaa matunda, dunia nzima itakuwa inaangalia iwapo Libya itaweza kuwa na mwaka usio na vurugu. Hii ni baada ya nchi hiyo kupata kaimu waziri mkuu Faez Sarraj. Faez aliteuliwa baada ya mazungumzo ya amani.

Taifa hilo limezama kwenye fujo tangu kuondolewa kwa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, marehemu Muammar Gadhafi mnamo mwaka wa 2011.

Wajumbe kutoka Libya waliafikiana baada ya mazungumzo yaliyofanikishwa na UN yaliyofanyika nchini Morocco

8. Nigeria na Boko Haram?


Aprili mwaka huu, itakuwa ni miaka miwili tangu kutekwa nyara kwa wasichana wa shule eneo la Chibok, Nigeria na wapiganaji wa Boko Haram. Kampeni ya kutetea kukombolewa kwao ilivumisha kitambulisha mada #BringBackOurGirls mtandao lakini hadi sasa wasichana hao zaidi ya 200 hawajakombolewa. Rais Muhammadu Buhari amezidisha juhudi dhidi ya Boko Haram lakini atafanikiwa kuwakomboa wasichana hao?

Tukiwa Nigeria bado, Rais Buhari aliahidi kukabiliana na ufisadi na anapokamilisha mwaka mmoja uongozini, wengi watakuwa wakitathmini mafanikio atakayoyapata, ikizingatiwa kwamba aliamua kusimamia Wizara ya Fedha.

9. Mzozo wa kisiasa Sudan Kusini


Agosti mwaka 2015, kulitiwa saini Mkataba wa Amani uliotarajiwa kurejesha amani katika taifa hilo changa zaidi duniani. Lakini mapigano yaliendelea kuripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini humo na bado wahusika wote hawajaafikiana kuhusu utekelezaji kamili wa mkataba huo. Macho yataelekezwa Juba kuona iwapo Rais Salva Kiir na Dkt Riek Machar wataafikiana na kufanikisha amani huko.

10. Mzozo wa uchaguzi Zanzibar


Kuhitimisha orodha hii, nchini Tanzania baada ya uchaguzi 25 Oktoba, matokeo ya urais visiwani Zanzibar yalifutiliwa mbali na hadi sasa mshindi hajulikani. Kumekuwepo na mashauriano ya kutafuta suluhu lakini hadi sasa bado hakuna ufumbuzi. Majuzi Chama Cha Mapinduzi CCM kiliwahimiza wafuasi wake wajiandae kwa marudio ya uchaguzi, hatua ambayo haikupokelewa vyema na Chama cha Wananchi CUF. Chama hicho cha CUF tayari kimetangaza hakitashiriki sherehe za Mapinduzi. Suluhu itapatikana vipi?

Chanzo: BBC Swahilia

0 comments