Friday, 8 January 2016

Prof. Ndalichako kufumua viwango ufaulu mitihani

By    
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, ametoa siku saba kwa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kutoa sababu zilizofanya wakabadili mfumo wa madaraja ya ufaulu, vinginevyo antachukua hatua.

Prof. Ndalichako aliyasema hayo jana alipokutana na uongozi wa Necta na kuuweka kitimoto kwa dakika 42, huku wakijikanyaga juu ya sababu zilizofanya kubadili mfumo wa ufaulu kutoka kwenye ule wa jumla ya alama (Division) kwenda kwenye  mfumo wa wastani (GPA).

Mkutano huo uliofanyika kwenye kituo cha usahihishaji wa mitihani cha Necta kilicho Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam, ulianza kuonekana mwiba kwa,Katibu Mtendaji wa Necta,  Dk. Charles Msonde pale Prof. Ndalichako alipomwambia kuwa, kwa muda mfupi aliokaa wizarani (Prof. Ndalinacho) tangu kuapishwa Desemba 28, mwaka jana amekuwa akipokea malalamiko juu ya mfumo unaotumika kupanga madaraja hivyo anataka kupata ufafanuzi.

Katika majibu yake, Dk. Msonde alisema, mabadiliko ya kutoka kwenye Division kwenda kwenye GPA yalitokana na mahitaji ya kisera ya uendeshaji wa serikali kwa mfumo wa mtandao (E-Government), ambao unaelekeza mifumo yote ya kompyuta ya taasisi mbalimbali ibadilike.

“Pia tulihuwisha ili mifumo yetu iweze kuendana na ile ya TCU (Tume ya Vyuo Vikuu), watahiniwa wetu ambao wanaomba kutahiniwa kwenye vyuo vikuu na vile vya (Nacte) hawalazimiki tena kupeleka vyeti vyao ili kudahiliwa, sasa hivi unaomba tu hata kwa simu na mifumo inaongea yenyewe,” alisema na kuongeza:
“Wakati tukiwa kwenye mfumo wa Division tukisema A ni moja, vyuo vikuu vinasema A ni tano, kwa hiyo kulitakiwa kuwe na uwiano, mfumo huu wa wastani wa pointi (GPA), haujabadilisha chochote kwenye alama za ufaulu (Division I, II, III, IV), tulichofanya ni kutafuta wastani wa pointi tu.”
Dk. Msonde alisema mfumo wa sasa unaeleweka zaidi kuliko ule wa zamani ambao ulikuwa ukiwachanganya wazazi.

Baada ya majibu hayo, Prof. Ndalichako alimtaka Dk. Msonde kutoa sababu mahususi za kitaalamu, haswa akijikita kueleza hasara iliyotokana na kutumia Division na faida iliyopatikana kwenye GPA kwani wadau wakiwamo wazazi na watu wa shule binafsi wanaulalamikia.

“Labda kwa kukufafanulia zaidi, elimu ya juu hawatumii Division wala GPA, hapa tuna katibu mkuu ambaye alikuwa huko, wanaangalia alama alizopata mwanafunzi mmoja mmoja na wanaziwekea alama tofauti kabisa,” alisema Prof. Ndalichako na kuongeza:

“Hata mambo ya E-Government ilikuwa haiangalii hayo uliyoyasema, labda useme tu kwa namna ambayo itakuwa rahisi kwa Watanzania wakuelewe tofauti na walivyo sasa.”

Prof. Ndalichako alikuwa Katibu Mtendaji wa Necta kwa miaka tisa kabla ya kujiuzulu mwaka 2013 alipokumbwa na shinikizo la kisiasa akitakiwa kubadilisha matokeo ya mtihani wa kidato cha nne wa mwaka 2012 ambao asilimia 60 ya wahitimu walapata sifuri.
Waziri huyo alimtaka Dk. Msonde kueleza sababu ambazo zingetokana na mifumo hiyo kutoendana.

Dk. Msonde alijibu alisema: “Niseme kwamba, mfumo huu unaleta faida kwa wanafunzi kuelewa kwa ngazi zote, pia unasaidia kurahisisha udahili wa vyuo vikuu,” alisema.

Baada ya kauli hiyo, Prof. Ndalichako alimkatisha Dk. Msonde na kumsimamisha Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia elimu ya Juu, Prof. Simon Msanjila, aliyesema mfumo wa udahili wa vyuo vikuu hauangalii GPA, bali unajikita kwenye fani mtu anayotaka kusomea.

“Kama mtu anaenda kusoma ualimu unaangalia kapata nini kwenye masomo yake, yawezekana kapata B, B na 0, watachukua hayo masomo na kumpangia, suala la GPA hapa halipo,” alisema Prof.  Msanjila.

Baada ya maelezo hayo, Dk. Msonde alisema waziri akienda kusoma kijitaabu alichompa atajua msingi wa kubadilika kwa madaraja hayo na wapi maelezo yalipotoka.

Baada ya kauli hiyo, Prof. Ndalichako alimtaka Dk. Msonde kuwa  wazi kwenye maelezo yake kwani hakuna siri na Watanzania wanataka kuelewa.

Baada ya kauli hiyo, Dk. Msonde bila kutaja jina, alisema baraza lilipata maagizo kutoka kwenye viongozi wa wizara husika.

“Humu ndani ya kitabu utakuta kuna maelezo hayo ya waziri na katibu mkuu, ambayo bodi iliyafanyia kazi na kuja na GPA badala ya Division,  kama nilivyosema mfumo huu haujawekwa utumike miaka yote na utafanyiwa tathimini yale yasiyo na tija yatatolewa,” alisema Dk. Msonde.

Alisema pia kuwa, kwenye maelezo waliyopewa waliambiwa tu wabadili mfumo na wasiathiri viwango vya ufaulu.

Kutokana na kauli hiyo, Prof. Ndalichako alimwambia kwamba, kati ya malalamiko ya wamili wa shule binafsi ni kupunguzwa kwa alama za ufaulu.
“Wanasema A ilipokuwa inaanzia wakati wa Division sipo ilipo leo,” alisema Prof. Ndalichako na kumpa siku saba Dk. Msonde  kutoa ufafanuzi wa kitaalamu juu ya mabadiliko hayo na wadau walivyoshirikishwa kwenye kuubadili.

WATIHANIWA BINAFSI

Baada ya kupata maelezo hayo, Prof. Ndalichako alitaka pia kupewa maelezo ya kwa nini baraza hilo lilianzisha mtihani wa maendeleo (Continues assessment-CA) kwa wanafunzi wanaorudia mitihani ya taifa ya sekondari.

Alisema kwa kawaida, wanafunzi hao huonekana tu wakati wakitaka kufanya mitihani, hivyo hakuna namna yoyote ya kuwapima kabla ya kufanya mtihani huo wa mwisho.

Prof. Ndalichako alisema mtihani huo ulianzishwa kwa azimio la Musoma lililotaka badala ya kumpima mwanafunzi aliyesoma kwa miaka saba ama minne kwa mtihani wa siku moja, ni vyema kukawa na mitihani hiyo ya katikati ambayo alama zake zitajumuishwa na ule wa taifa.
Alisema wakati yeye akiwa Katibu Mtendaji wa Necta, alitakiwa kuanzisha mitihani hiyo lakini alikataa kwa sababu kitaalamu hilo ni jambo lisilowezekana.
“Sasa nyie mtuambie kitaalamu mkiwa mnatunga hii mitihani ni misingi gani mnatumia kusema huu utakuwa CA na huu mtihani,” alisema Prof. Ndalichako.
Kwenye maelezo yake, Dk. Msonde alisema wizara ndiyo ilielekeza mabadiliko hayo kwa maelezo kwamba, watahiniwa binafsi wanafeli sana kwa sababu wanatahiniwa kwa mtihani mmoja tofauti na wale wa shule ambao wana alama za CA.

Alisema kwa dhana hiyo ndipo walipoanzisha mtihani wa pili kwa watahiniwa binafsi (somo moja wanafanya mitihani miwili), ili ule mmoja uwe CA na mwingine mtihani wa mwisho.

Baada ya maelezo hayo, Prof. Ndalichako alisema, Necta ndiyo yenye wataalamu wanaotakiwa kufikiri na kuishauri wizara kwani mantiki ya CA ni upimaji endelevu hivyo haiwezekani kumpa mtihaniwa binafsi mtihani huo kwa kuwa anaonekana siku ya mtihani wa mwisho.

Dk. Ndalichako pia aliitaka Necta kuandika sababu za kitaalamu zilizofanya kuanzishwa mitihani hiyo miwili kwa watahiniwa binafsi na kutoa mifano ya nchi nyingine zinazotumia mfumo huo.

Alisema wasipokuwa na sababu hizo, kuanzia mwaka huu watahiniwa binafsi wafanye mtihani mmoja kama ilivyokuwa awali.

Aliwataka kucha usanii kwenye elimu na kuhakikisha uamuzi wowote wanaofanya uzingatie weledi na taaluma na siyo kufuata shinikizo.

Alisema Necta ikiyumbishwa kwenye kuchukua uamuzi, elimu nchini itayumba na kwamba kiu yake ni kujua upungufu uliopo kwenye sekta ya elimu na kuufanyia kazi.

“Mimi siangalii tu wangapi wamefaulu, nataka nijue tatizo la wanafunzi na walimu kwa sababu ukikuta labda darasa zima limepata F lazima hapo kuna tatizo, au ukikuta wengine wamechora mazombi vitu vingine hapo kuna tatizo.”

“Nitataka mchambue nijue upungufu kama huo ili nifuatilie kwa nini hali iko hivyo, kwa sababu naamini kila mtoto anafundishika,” alisema Prof. Ndalichako.

Waandishi wa habari walipotaka kujua hatua ambazo Prof. Ndalichako atachukua asiporidhika na maelezo ya kubadilishwa kwa alama hizo na kuanzishwa kwa mtihani huo wa watahiniwa binafsi, alisema: “Msiwe na haraka, muda ukifika mtajua, msitake nivuke daraja kabla sijalifikia.”

CHANZO: NIPASHE

0 comments