Friday, 31 May 2013

MAJIRA; Ufaulu IV-2012 waongezeka

Na  Grace Ndossa na Goodluck Hongo, Majira


 KIWANGO cha ufaulu kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka 2012, kimeongezeka kwa asilimia 43.8 tofauti na yale yaliyotangazwa awali ambayo ni asilimia 34.5.
Matokeo hayo yametangazwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa ambaye alisema kuwa, kati ya wanafunzi 397,138, waliofaulu ni 159,609.

Kati ya wanafunzi hao, wavulana 98,858, wasichana ni 60,751, sawa na asilimia 43.8 tofauti na matokeo ya awali.

Alisema waliofaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu ni 35,349 ambapo kati yao, wavulana ni 24,425, wasichana ni 10,924, sawa na asilimia 9.55. Waliopata daraja la
nne ni 124,260 sawa na asilimia 33.54 ambapo jumla ya watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani huo mwaka 2012, walikuwa 480,029 katika vituo 5,058 vilivyosajiliwa.

Aliongeza kuwa, wanafunzi 210,846 walipata sifuri sawa na asilimia 56.2. Dkt. Kawambwa alisisitiza kuwa, matokeo hayo ni halali na hayajachakaliwa.

“Matokeo yaliyofutwa yalikuwa yamechakatwa kwa kutumia utaratibu wa “fixed grade ranges”, ambapo viwango vya aina moja hutumika kuchakata matokeo kwa masomo bila kujali kiwango cha ufaulu wa masomo husika.

“Matokeo ya sasa yamefanywa vivyo hivyo, lakini yamefanyiwa Standardlization (kuongezwa) ambapo kimataifa kuna aina kuu mbili za kuchakata matokeo ya mtihani,” alisema Dkt. Kawambwa.

Aliongeza kuwa, kwa miaka mingi Baraza la Mitihani limekuwa likitumia mfumo wa “flexible grade ranges” ambapo mwaka 2012 mfumo wa “fixed grade ranges”, ulitumika kuchakata matokeo kwa mara ya kwanza.
Hata hivyo, Dkt. Kawambwa alisema kuanzia mwaka huu, wataanza kuchakata matokeo kwa mfumo wa “fixed grade ranges” kuanzia kidato cha nne hadi sita kama nchi nyingine zinavyofanya.

Alisema ubora wa shule umepangwa kwa kutumia kigezo cha daraja la kwanza hadi la mwisho na shule zimegawanywa katika makundi mawili la kwanza ni zile zenye wanafunzi zaidi ya 40 na nyingine zenye wanafunzi chini ya 40 kulingana na idadi ya wanafunzi.

Shule 10 bora katika kundi la shule zenye watahiniwa 40 na zaidi zilizoongoza ni St. Francis Girls (Mbeya), Marian Boys (Pwani), Feza Boys (Dar es Salaam), Marian Girls (Pwani), Canossa, Fedha Girls zote za (Dar es Salaam), Rosmini (Tanga), Anwarite Girls (Kilimanjaro), St. Mary Mazinde Juu (Tanga) na Jude Mushono Arusha.

Alizitaja shule 10 za mwisho zenye watahiniwa 40 na zaidi, Mibuyuni (Lindi), Mamndimkongo (Pwani), Chitekete (Mtwara), Kikale (Pwani), Zirai (Tanga), Matanda (Lindi), Kwamndolwa (Tanga), Chuno na Mbembaleo zote za (Mtwara) pamoja na Maendeleo ya Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa baraza hilo, Dkt. Charles Msonde, alisema baraza lilipewa jukumu hilo na kulifanyia kazi ambapo wanafunzi 10 bora wa mwanzo, wataonekana kwenye tovuti za baraza hilo.

Februari 18,2013 wakati Dkt. Kawambwa akitangaza matokeo hayo, alisema watahiniwa 23,520 walifaulu katika daraja la kwanza hadi tatu kati yao wasichana 7,178, wavulana 16,342

Alisema waliopata sifuri 240,903m, kati yao wavulana 120,664, wasichana 120,239 na waliopata daraja la nne 103,327.

0 comments