Thursday, 30 May 2013

WAKATI VIWANGO VINAPANDISHWA; WALIMU 40 HAWAJARIPOTI KASULU

MBUNGE wa Kasulu Vijijini, Agripina Buyogera (NCCR), amesema walimu 40 waliopangiwa katika wilaya hiyo wameshindwa kuripoti kazini kutokana na mazingira magumu ya mikoa ya pembezoni.

Buyogera alieleza hayo bungeni jana wakati alipokuwa akiuliza swali la nyongeza.

“Tatizo la ukosefu wa walimu mikoa ya pembezoni lipo katika maeneo mengi nchini na linatokana na ukosefu wa miundombinu je, serikali haioni umuhimu wa kuweka posho maalumu kwa walimu hao ili waweze kukaa kwenye maeneo hayo?” alihoji.

Pia mbunge huyo alitaka kujua kama naibu waziri atakuwa tayari kuambatana naye baada ya mkutano wa Bunge kwenda Kasulu, ili akatatue tatizo la ukosefu mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi.

“Kasulu Vijijini kuna shule 15 za sekondari lakini hakuna hata shule moja yenye walimu wanaofundisha masomo ya sayansi,” alisema mbunge huyo.

Katika swali la msingi, mbunge huyo alitaka kujua kama serikali ipo tayari kuboresha huduma na mazingira na kuweka nyongeza ya fedha za kujikimu kwa walimu wanaopangiwa vijijini.

Akijibu maswali hayo, naibu waziri huyo alisema uko mpango wa serikali wa kupita katika maeneo ya pembezoni katika kada zote.

Mwanri alitoa rai kwa watumishi wanaoajiriwa katika maeneo ya pembezoni kuwa na moyo wa uzalendo, licha ya kuwepo kwa mazingira magumu.

Akizungumzia tatizo la walimu wa sayansi, alisema lipo nchini nzima na si Kasulu pekee na kuongeza kuwa yuko tayari kwenda Kasulu kuangalia tatizo hilo.

Akijibu swali la msingi, alisema serikali kupitia Bodi ya Mishahara na masilahi kwa watumishi inaendelea kufanya uchambuzi kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kazi ya watumishi wote nchini katika maeneo ya mishahara, posho, mazingira ya kuishi na viendea kazi.

Aidha, alisema serikali inayo dhamira ya dhati ya kukabiliana na changamoto zilizopo katika maeneo yenye mazingira magumu nchini.

Mwanri alisema katika kutekeleza azima hiyo, mwaka 2013/14, serikali imetenga sh bilioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi katika halmashauri 40 zilizobainishwa kuwa na mazingira magumu na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu imetengewa sh milioni 500.
source: Tanzania Daima

0 comments