Na Muislam WA Jihad kutoka WASIKILIZAJI WA REDIO IMAAN
Tarehe 27 Aprili, 1985 Julius Kambarage Nyerere, sasa akijulikana kama
Baba wa Taifa, katika sherehe kubwa katika viwanja vya Ikulu, alitoa
jumla ya medali 3979 kwa Watanzania waliochangia katika maendeleo ya
taifa. Kati ya wale ambao walipewa medali hizo alikuwa Sheikh Abdallah
Chaurembo.
Wazalendo waliotajwa ndani ya kitabu hiki ambao
walipigania uhuru wa Tanganyika, hakuna hata mmoja wao aliyekuwa katika
orodha ile ya heshima. Baada ya siku chache kupita, Nyerere kama mtu
aliyegutuka alimualika Dossa Aziz Ikulu.
Dossa Aziz, wakati wa
kudai uhuru wa Tanganyika alikuwa mtu maarufu, mwenye nafasi, na
kujiweza sana. Sasa Dossa baada ya miaka kupita hakuwa akifahamika tena
na ule umaarufu na utajiri wake ulikuwa umetoweka. Alikuwa akiishi
maisha ya kawaida kijijini Mlandege, maili chache nje ya Dar es Salaam.
Katika sherehe ya faragha Nyerere alimtunukia medali Dossa Aziz, rafiki
yake wa zamani. 295
Ule Mkutano wa Tabora ulikuwa umeacha kovu
lake katika historia ya uhuru wa Tanganyika. Huenda kama si yale
masharti ya uchaguzi wa kura tatu, historia ya TANU na kwa hakika ile ya
ukoloni Tanganyika isingekuwa hivi ilivyo sasa. Yamkini kusingekuwepo
na mgawanyiko katika TANU wala Zuberi Mtemvu asingeunda ANC, na Mashado
Plantan - AMNUT; wala suala la udini katika siasa za Tanganyika
lisingewekwa katika agenda, jambo ambalo kwa miongo mitatu baada ya
uhuru ngurumo zake bado zinasikika na zinatishia utengemano na uthabiti
wa nchi. Waislam wanamlaumu Nyerere na Wakristo waliokabidhiwa madaraka
ya kutawala nchi kwa msaada mkubwa wa Waislam. Waislam wanadai kuwa
wamesalitiwa. Kwa hivi sasa Waislam wako katika mwelekeo wa kujitambua
kwa mara ya pili na historia yao yenye mengi sana. Wanaamini majibu ya
baadhi ya matatizo yao ya hivi sasa yamo katika historia yao ya zamani.
Mjini Dar es Salaam katika msikiti wa Kitumbini hafla husomwa kila
mwaka katika mwezi wa Oktoba kumkumbuka Abdulwahid Kleist Sykes. Hii ni
hafla ya kifamilia ikihudhuriwa hasa na wana-ndugu. Ukiachia mbali ule
wajibu wa Waislam kurehemiana kama ilivyo kawaida katika Uislam,
Abdulwahid hufanyiwa hafla hii pale msikitini kwa sababu nyingine.
Katika umri wake mfupi, Abdulwahid alikuwa akiswali pale msikitini na
katika msikiti ule ndipo aliposwaliwa swala yake ya mwisho kabla ya
kupelekwa kuzikwa. Abdulwahid alikuwa mtu mashuhuri katika jamii ya
Waislam Dar es Salaam. Alifanya shughuli nyingi chini ya Al Jamiatul
Islamiyya. Halikadhalika alikuwa katibu baadae rais wa TAA. Ingawa
historia ya Tanzania bado haijamtambua mchango wake ni wazi kuwa
Abdulwahid ndiye aliyekuwa bongo katika kuasisi TANU chama ambacho
kilikuja kuwaunganisha wananchi wa Tanganyika katika kudai uhuru wao kwa
Waingereza.
Marika ya Abdulwahid bado wa hai na baadhi yao
wanaswali pale msikitini. Huwa wanafurahishwa na kumbukumbu hii ya
kumrehemu mwenzao. Karibu walio wengi ni maveterani wa TANU ya miaka ya
1950. Hivi sasa wao ni wazee na kwa uchungu hawana haja na siasa.
Ukiacha ndugu wa marehemu Abdulwahid (sasa hivi wanajumuika na wajukuu
zake), marafiki wa karibu na wanachama wa zamani wa TANU, hakuna hata
mtu mmoja katika Chama cha Mapinduzi (chama kilichorithi nafasi ya TANU)
anaemkumbuka.
Jina la Abdulwahid halitajwi kabisa katika
historia ya kudai uhuru wa Tanganyika au katika historia ya kuasisi
TANU. Juu ya haya yote Abdulwahid ndiye aliyewasha cheche za kuanzisha
harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.
Jopo la wana-historia wa
Chama Cha Mapinduzi waliopewa jukumu la kutafiti na kuandika historia
rasmi ya TANU, hakuna hata sehemu moja waliyotaja jina la Abdulwahid
katika kitabu kizima.296 Dhana inayojaribiwa kuenezwa katika kitabu kile
ni kuwa kabla ya kutokea kwa Julius Nyerere mwezi Aprili, 1953,
alipochaguliwa kuwa rais wa TAA, chama hicho hakikuwa na mwelekeo wowote
wa siasa. Kitu cha ajabu ni kuwa kitabu hicho wala hakielezi huo urais
wa TAA, Nyerere aliupataje au aliuchukua kutoka kwa kiongozi gani wa
wakati ule.
Kitendo hiki kimeondoa hadhi na heshima ya
wazalendo wengi waliopigania nchi hii na halikadhalika kimeiondolea TAA
heshima ya kuitwa chama cha siasa. Wanahistoria wazalendo pamoja na
wanasiasa wa sasa hawataki kabisa kuipa TAA hadhi ya chama cha siasa.
Kambona aliiita African Association chama cha majadiliano:
Sasa
inakaribia mwaka mmoja toka iundwe Tanganyika African National Union na
katika kipindi hiki chama kimekua kikipata nguvu siku hadi siku, wakati
mwingine chini ya upinzani mkubwa.
Kama mnavyofahamu chama hiki ni badala ya Tanganyika African Union ambayo ilikuwa sawasawa na chama cha majadiliano.297
Ulotu anaieleza TAA kuwa ilikuwa chama cha ustawi wa jamii.298 Wengine
wameieleza TAA kama taasisi ya jamii: Nyerere (1976), halikadhalika
Japhet na Seaton (1966).300 TAA wakati mwingine inaelezwa kuwa ilikuwa
chama cha vuguvugu za upinzani dhidi ya ukoloni, lakini upinzani wake
haukuwa dhahiri: Kaniki (1974), Nyerere (1953) 302 aliieleza TAA kama
chama cha vuguvugu la siasa lakini si za dhahiri. Julius Nyerere
alipohutubia Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa, New York, tarehe 7
Machi, 1955 alisema:
Tanganyika African National Union kwa
mtazamo mmoja ni chama kipya, lakini kwa mtazamo mwingine ni chama
kikongwe. TANU imechukua nafasi ya Tanganyika African Association ambayo
ilianzishwa mwaka 1929, kama chama cha kijamii. Tanganyika African
National Union, chama kilichochukua nafasi ya African Association miezi
kumi iliyopita ni chama kipya kwa maana ni chama cha siasa, wakati TAA
ilikuwa chama cha siasa nusunusu.
Wasomi wengine wameishusha
TAA kufikia daraja la kuwa klabu: Mwenegoha (1976) anaandika: 'Mwaka
1954, baada ya miaka ishirini na tano ya kutoweza kufanya lolote,
Nyerere aliigeuza TAA kutola chama cha kijamii kuwa chama cha siasa
chenye kuogopwa kilichoitwa Tanganyika African National Union'. 303
Abdulwahid ambae alitoa mchango wa pekee katika kuunda TANU alikuwa
anaiona TAA kama chama cha siasa (1951). 304 Katika kundi la waandishi
na wasomi walioandika kuhusu African Association kisha wakabadili mawazo
yao kuhusu nini hasa chama kile kilikuwa, ni Nyerere na Hatch ndiyo
waliobadili misimamo yao ya awali. Nyerere alipoandika barua kwa Gavana
wa Tanganyika, Edward Twining tarehe 10 Agosti, 1953 alieleza kuwa TAA
ni chama cha siasa. 305
Lakini baadae alibadili msimamo na
kusema kuwa TAA kilikuwa chama cha starehe. Kauli hii ilitawala hotuba
za Nyerere na maandishi yake kwa kipindi kirefu. Katika miaka ya hivi
karibuni amesikika akisema kuwa TAA kilikuwa 'chama cha siasa
kisichokuwa na katiba ya siasa'. Hatch (1976) ameieleza TAA kama chama
cha starehe 306 sehemu moja na chama cha siasa sehemu nyingine.307 John
Kabudi ameieleza African Association kama 'chama cha watu binafsi
wananchi kilichokuwa na mwelekeo wa kitaifa'.308 Ieleweke kuwa hata
viongozi wa TAA hawathaminiwi kama wanasiasa. Kaniki, kwa kukosa neno la
kuwatambulisha waasisi wa TAA, amewaita wanasiasa na kuwawekea
quatation mark:
Nyerere, kabla ya hapo akiwa hajulikani na
'wanasiasa' wengi katika Tanganyika, alikuwa mwalimu katika shule ya
Mtakatifu Francis, Pugu, jirani na Dar es Salaam, na alikuwa
amechaguliwa rais wa (TAA) mwaka uliopita.309
Kwa mtazamo
huo wa Kaniki mzalendo kama Abdulwahid Sykes hakuwa mwanasiasa, ila
Nyerere ndiye mwanasiasa. Iliffe (1968)310 alidokeza kuwa historia ya
TANU iliyokuwa imeandikwa hadi wakati ule ilikuwa haijakamilika na
katika uchambuzi wake alisema kuwa African Association kutokana na
mwelekeo na wanachama wake ilikuwa ni chama cha siasa. Kandoro na
Japhet, 311 waasisi wa TANU walipata umaarufu wakati Abdulwahid akiwa
rais wa TAA mwaka 1952. Hawa walikuwa ndiyo waasisi pekee ambao
walifanya kazi na Abdulwahid wakati wa Mgogoro wa Ardhi ya Wameru.
Safari ya Kirilo kuja Dar es Salaam na kule kumweka Seaton kama
mwanasheria kushughulikia mgogoro ule, kazi yote hiyo ilifanywa na
Abdulwahid na uongozi wa TAA wa wakati ule. Ilikuwa Abdulwahid ndiye
aliyemhangaikia Kirilo
kupata pasi ya kusafiria baada ya kunyimwa pasi kule Arusha. Kirilo na
Seaton na halikadhalika Kandoro wamenadika kumbukumbu zao kuhusu
ukoloni, lakini cha ajabu na kusikitisha ni kuwa hakuna hata sehemu moja
waandishi hawa wametaja mchango wa Abdulwahid hata kwa kuparazia tu.
Waandishi hawa wamejaribu kumtumbukiza Nyerere kama kiongozi aliyehusika
katika Mgogoro wa Ardhi ya Wameru, wakati yeye hata kuwapo nchini
wakati ule hakuwapo. Ukweli ni kuwa wakati mgogoro wa ule ulipofikishwa
mbele ya Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa, New York, Nyerere
alikuwa masomoni Chuo Kikuu cha Edinburgh Uskochi akisomea shahada ya
pili. Mwandishi aliyejipambanua
na hawa wote kwa kutomtaja Abdulwahid ni mama wa Kiingereza Judith
Listowel (1965) 312 ambae ingawa amemtaja kijuujuu, ameandika kwenye
kitabu chake kuwa Abdulwahid alikuwa mmoja wa waasisi wa TANU.
Katika miaka hii ya karibuni kumejitokeza hamu ya kutaka kuielewa
historia ya siasa katika Tanzania na jina la Abdulwahid limekuwa
likijitokeza mara kwa mara katika majarida, 313 magazeti, 314 magazeti
ya kimataifa, 315 na katika vitabu. 316 Maandiko yote haya yanamtazama
Abdulwahid kwa sura tofauti. Yapo yanasema kuwa yeye ndiye alikuwa
kinara katika kuunda TANU na kumtia Nyerere katika siasa. Katika
maandiko haya Abdulwahid anaelezwa kama mzalendo na mwanamapinduzi.
Tandon anamweleza Abdulwahid na wazalendo wengine katika Afrika ya
Mashariki kama Chege Kibachia, Makham Singh, Fred Kubai, James Kivu,
I.K. Musazi, Erika Fiah na Gama Pinto kama 'viongozi maveterani wa watu
wa Afrika ya Mashariki ambao wanahistoria wetu wa sasa wamewasahau'. 317
Wapo waandishi wanaomuona Abdulwahid kama 'kabaila uchwara' kutokana na
kuwa alikuwa mtoto wa mfanyabiashara Mwafrika tajiri, Kleist Sykes.
Profesa Shivji anamtuhumu Abdulwahid kwa kushirikiana na wakoloni na
anamchukulia kama kabaila uchwara ambae yeye mwenyewe hatoki katika
tabaka la wafanyakazi. Akitafakari nafasi ya Abdulwahid kama kiongozi wa
makuli katika bandari ya Dar es Salaam wakati wa ukoloni Shivji ansema:
serikali ilipenyeza uongozi wa makabaila uchwara katika chama. Mwezi
February 1948 Abdul Sykes, mtoto wa mfanya biashara Mwafrika maarufu,
aliombwa na serikali awe katibu wa chama cha makuli. Abdul Sykes hakuwa
akifanyakazi bandarini wala hakuwa anatoka katika tabaka la
wafanyakazi.318
Hapa Shivji alikuwa anaeleza jinsi Abdulwahid alivyochaguliwa
kuwa katibu mkuu wa kwanza katika historia ya vyama vya wafanyakazi
Tanganyika. Kwa kutoijua vyema historia ya maisha ya Abdulwahid na
vilevile kwa hamaki za misimamo ya mrengo wa kushoto ya Ki-Marx, Shivji
ametumia vipimo visivyo sawa katika kumchambua Abdulwahid. Engels
anasema bepari uchwara ni 'tabaka la makabaila wa kisasa ambao wanahodhi
njia zote za uzalishaji mali za jamii na vilevile wanawaajiri na
kuwalipa'.319 Hata hivyo Sklar anasema kuwa dhana hiyo sasa imebadilika
kwa hiyo hata ile maana yake ya awali imebadilika:
Hivi sasa
neno hilo linatumiwa na wafuasi wa Marx kuieleza tabaka lililo juu
katika jamii ambazo zinafuata soko huria na kuachia kuhodhiwa kwa mali
kama matokeo ya mali binafsi katika uzalishaji wake.320
Kama
Shivji angeliyajua maisha ya Abdulwahid ni wazi kuwa angetumia kipimo
kingine kabisa katika kumweleza. Lakini kwa kuwa kilichotumika ni kipimo
kisicho sawa, matokeo yake hayakuweza kuwa barabara. Hakuna biashara ya
Mwafrika wakati wa ukoloni inaweza kuitwa biashara ya bepari na katika
mkumbo wa kujumuishwa katika dhana ya ubepari, kama ubepari ulivyokuwa
ukifahamika huko Ulaya. Haya ndiyo matatizo yanayoikumba historia ya
Abdulwahid na kwa kweli historia nzima ya taifa la Tanganyika.
Katika wale walioasisi TANU, ni wale tu aliokuwa makao makuu ya TAA
ndiyo wanaoweza kueleza historia ya kweli ya chama hiki. Hawa ni John
Rupia, Dossa Aziz, Tewa Said Tewa, Julius Nyerere, Dome Budohi,
Abdulwahid na Ally Sykes. Hawa ndugu wawili, Abdulwahid na Ally, wao ni
baba yao ndiye aliyekuwa muasisi wa African Association akiwa kama
katibu wake wa kwanza hapo mwaka wa 1929. Majalada ya akina Sykes kuhusu
African Association na TANU yana habari muhimu sana kwa mtafiti kuhusu
historia ya ukoloni na juhudi walizofanya waasisi wa taifa la Tanganyika
katika kujikomboa. Majalada haya yana habari muhimu na za kutosha
kuhusu Nyerere na jinsi alivyopokelewa Dar es Salaam na akina Sykes na
jinsi alivyoingizwa katika siasa. Inastaajabisha kuwa kumbukumbu hizi
zenye habari muhimu sana kuhusu Nyerere na TANU hazikuguswa kabisa
wakati watafiti wa historia ya TANU walipokuwa wakifanya utafiti wao.
Inastaajabisha vilevile kuwa, si Ally wala mdogo wake, Abbas ndugu
wawili walio hai baada ya kifo cha kaka yao Abdu.
0 comments