Saturday, 15 March 2014

WANANCHI JORDAN WAANDAMANA KUTAKA UBALOZI WA ISRAEL UFUNGWE NCHINI KWAO


Wananchi wa Jordan sanjari na kufanya maandamano makubwa mjini Amman, mji mkuu wa nchi hiyo, wamesisitiza juu ya kufukuzwa balozi wa utawala wa Israel nchini humo. 

Maandamano hayo yalifanyika hapo jana mbele ya ubalozi wa utawala huo mjini Amman, katika kulalamikia hatua ya askari wa utawala wa Kizayuni ya kumuua kadhi mmoja raia wa Jordan katika mpaka wa nchi hiyo na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. 

Washiriki wa maandamano walichoma moto bendera ya utawala huo, walilaani pia uvunjaji wa haki za Wapalestina unaofanywa na askari wa Israel kila siku.

Waandamanaji hao waliokuwa na hasira kali, walizuiliwa na polisi wa Jordan walioweka uzio kuwazuia kufika kwenye ubalozi wa utawala huo. 

Kwa upande mwingine katika kulalamikia hatua hiyo ya kupigwa risasi kadhi wa Jordan, Jumatano iliyopita bunge la nchi hiyo liliupigia kura ya ndio muswada wa kufukuzwa balozi wa utawala wa Kizayuni nchini humo. 

Kadhi huyo wa Jordan aliuawa siku ya Jumatatu kwa kupigwa risasi na askari wa utawala huo katika kivuko cha mpakani cha al-Karamah huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

0 comments