Tuesday, 29 April 2014

“TUNALAANI UKATILI MAOVU WANAYOFANYIWA WAANDISHI WA HABARI.” - TIBANYENDERA (MISA-TAN)

DSC_0085
Picha juu na chini ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN), Bw. Mohamed Tibanyendera (wa pili kushoto) akizungumza jijini Dar es Salaam jana kuhusiana maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari yatakayofanyika wiki hii duniani kote. Kushoto ni Meneja wa Maadili na Usuluhishi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Allan Lawa, Afisa Habari wa kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Bi. Usia Nkhoma Ledama (wa pili kulia) na Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa habari Tanzania (UTPC), Jane Mihanja (kulia).(Picha na Zainul Mzige).
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Zaidi ya washiriki 200 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kuhudhuria kwenye matukio ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, inayotarajiawa kuadhimishwa nchini hapa mnamo Mei 3, jijini Arusha, imeelezwa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN), Bw. Mohamed Tibanyendera, amesema kwamba maadhimisho hayo yenye lengo kuu la kulaani maovu wanayofanyiwa waandishi wa habari barani Afrika na duniani kote, yatafunguliwa na Jaji Mstaafu Mark Bomani.
Tibanyendera amesema kwamba, pamoja na mambo mengine maalum ambayo yatakuwa yameandaliwa, matukio ya mwaka huu yataambatana pia na uzinduzi wa kitabu kiitwacho “Hii Ndiyo Demokrasia, Toleo la 20”, kitachokuwa na taarifa muhimu kuhusu waandishi wa habari walionyanyaswa na kufanyiwa vitendo vilivyokiuka haki za binadamu, barani Afrika.
DSC_0053
DSC_0108
Meneja wa Maadili na Usuluhishi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Allan Lawa (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari jijini Dar kuhusu siku ya maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari itakayofanyika jijini Arusha.
“Tunategemea kuwa na wageni zaidi ya 200, kwa siku hiyo pia tuazindua kitabu kitachozungumzia waandishi walionyanyaswa na kufungwa katika maeneo mbalimbali ya Kusini mwa Afrika pamoja na hali ya vyombo vya habari na uhuru wa habari katika nchi hizo ikiwemo Tanzania,” amesema Tibanyendera.
Tibanyendera ameongeza na kusema kwamba maadhimisho hayo ya siku mbili, yatakayofanyika kuanzia Mei 2 hadi 3, yataambatana pia na utolewaji wa semina za kuwaelimisha washiriki kuhusu mambo mbalimbali ya habari na uhuru wake, kutoka kwa wataalam wakiwemo wahadhiri watakaotoka vyuo mbali mbali hapa nchini na kwingineko, ambao wameandaliwa rasmi kwa ajili ya shughuli hiyo.
Wakati huo huo, Meneja wa Maadili na Usuluhishi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) ambao pia ni moja ya taasisi zitakazoshiriki kwenye maadhimisho hayo, Bw. Allan Lawa, amesema kwamba MCT itazindua katika maadhimisho hayo machapisho matatu yatakayohusu masuala ya habari ikiwepo ripoti ya uvunjifu wa uhuru wa habari nchini ambayo yatapatikana katika ofisi zao.
DSC_0126
Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa ambao ni mmoja wa wadhamini wa siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, Bi. Usia Nkhoma Ledama (wa pili kulia), ambaye alisisitiza kwamba uhuru wa vyombo vya habari nchini ni muhimu kusaidia nchi zinazoendela kufika malengo ya milenia.
“Sisi kama MCT tumeandaa machapisho matatu ambayo yatazinduliwa siku hiyo yanayogusia hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania 2013, ripoti ya utafiti wa uvunjifu wa uhuru wa habari katika mwaka 2013, na ripoti ya ukiukwaji wa uhuru wa vyombo vya habari nchini.
“Tuna furaha kuwaambia kwamba machapisho yote haya yatapatikana siku hiyo na wote mnakaribishwa kujipatia nakala zenu,” amesema Lawa.
Akimalizia, Bw. Lawa alisema waandishi wa habari wanapaswa kufika katika ofisi za Makao Makuu ya MCT zilizopo jijini Dar es Salaam kuchukua machapisho hayo ili waweze kuyasoma kwa kina na kuweza kutambua haki zao za msingi. Alisema pia kwamba muda si mrefu, nakala za machapisho hayo zitasambazwa na kupatikana kwenye vilabu vya vyombo vya habari (Press Club) vya mikoani ili waandishi ambao wako nje ya Dar es Salaam nao waweze kunufaika na machapisho hayo.
Maadhimisho hayo yamembeba kauli mbiu ya “Uhuru wa vyombo kwa Maendeleo ya Utawala Bora”.
DSC_0144
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa habari Tanzania (UTPC), Jane Mihanja ambaye amesema mwandishi wa habari yoyote akizuiwa kuingia kwenye mkutano ambao ni wawazi anatakiwa kutoa taarifa katika juhudi za kuhamasisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.
DSC_0033
Pichani juu ni chini ni baadhi ya waandishi wa habari na wadau wa tasnia hiyo waliohudhuriwa mkutano huo.
DSC_0031

0 comments