Monday, 3 November 2014

ASKOFU AOMBA SERIKALI WATOE RUZUKU KWA SHULE ZA PRIVATE

SERIKALI imeombwa kurudisha mfumo wa zamani wa kuzipatia shule binafsi ruzuku, lengo ni kuzifanya shule hizo kupunguza ada na hivyo kusaidia kuondoa tabaka la kielimu miongoni mwa Watanzania.

Hayo yalisemwa juzi na Mhashamu Askofu Tarcius Ngalalekumtwa wakati wa sherehe za Mahafali ya Saba ya Chuo Kikuu Kishiriki Mwenge (MWUCE), mjini hapa.

Askofu Ngalalekumtwa ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini, alisema kutokuwepo kwa ruzuku ya Serikali kumesababisha kuwapo kwa viwango vikubwa vya ada, hali inayosababisha kuwapo kwa matabaka na adha kwa wazazi wasiokuwa na uwezo wa kuwapeleka watoto wao kwenye shule za taasisi.

“Ni vyema Serikali sasa ikachukua jukumu la kurejea nyuma kwa kuzipatia shule zote ruzuku ili watoto wote waweze kusoma shule yoyote…katika hili kila shule itahiji kupeleka bajeti yake,” alisema Askofu Ngalalekumtwa.

Akizungumza katika mahafali hayo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome alisema katika kukabiliana na changamoto zinazozikabili elimu nchini, tayari wizara imetazama upya suala la sera ya elimu.

Profesa Mchome alisema wizara imeangalia pia mfumo wa elimu ulivyojipanga kwa kuangalia mwelekeo wa dunia inapokwenda, pamoja na njia ya kupata elimu bora ikiwa ni kuangalia jinsi elimu inavyoangaliwa katika ngazi zote kuanzia kwenye kata hadi taifa.
Aliongeza kuwa, ni lazima wizara kuangalia upya suala la mitaala ambayo itaifanya taifa lifikie kipato cha kati, na kufikia dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2020 na 2025.

Alisema takribani wanafunzi milioni 11 wanasoma ambapo kati ya hao, jumla ya wanafunzi milioni 8.2 ni wale wanaosome shule za msingi na milioni 1.6 ni wale wanasoma sekondari, huku idadi inayobakia ni wale wanasoma vyuo vikuu na vyuo vinavyotoa taaluma mbalimbali.

Alisema kutokana na takwimu hizo, bado idadi ya wanaofika vyuo vikuu haiendani na dira ya nchi, kuelekea mabadiliko ya haraka yanayoendana na malengo ya maendeleo ya milenia.

Mahafali hayo yalienda sambamba na uzinduzi wa kukipandisha hadhi Chuo Kikuu Kishiriki Mwenge (MWUCE) na kuwa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU).



CHANZO: HABARI LEO

0 comments