MBUNIFU wa mavazi, Miss Tanzania 2006, mwanamuziki na muigizaji wa filamu, Jokate Mwegelo amesaini makubaliano yenye thamani ya Sh bilioni 8.5 na Kampuni ya Kichina, Rainbow Shell Craft Company Limited kwa ajili ya kuzalisha na kuuza bidhaa mbalimbali za lebo yake ya Kidoti.
Makubaliano hayo yalisainiwa jana Dar es Salaam baina ya Jokate na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Rainbow Shell Craft Company Limited (CEO), Deng Guoxun.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwegelo alisema makubaliano hayo ni ya kudumu na kampuni hizo mbili zitazalisha na kuuza bidhaa za kidoti Tanzania nzima na nje ya mipaka yake.
“Hii ni hatua kubwa ya maendeleo kwangu, kama unavyojua, wakati naanza kujishughulisha na masuala ya urembo, ubunifu na uanamitindo, sikutegemea kufikia hatua hii ya kuingiza bidhaa zangu kimataifa, lakini sasa, ndoto zangu zimetimia na najivunia mafanikio haya,” alisema Mwegelo.
Alisema mbali ya kutoa mitindo tofauti ya kisasa ya nguo, kampuni yake pia itazalisha aina mbalimbali za viatu, nywele ikiwamo mawigi, rasta na viatu vya wazi (sandals) ambazo kwa sasa zipo tayari kwenye soko la Tanzania.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments