Profesa Lipumba alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Morogoro wakati wa mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Ndege, Kata ya Sabasaba.
Alisema Watanzania wamekuwa maskini kutokana na mfumo mbovu uliowekwa na viongozi waliopo madarakani.
Alisema viongozi wameshindwa kuhakikisha rasilimali zilizopo zinatumiwa kwa manufaa ya wananchi na siyo watu wachache.
Alisema Tanzania imejaliwa rasilimali nyingi kama madini, mbuga za wanyama, Mlima Kilimanjaro na ardhi ambayo ingeweza kutumika kuzalishaji na kutoa ajira kwa vijana.
Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Morogoro Mjini, Abeid Mlapakolo alisema maendeleo ya kweli na kuondoa umaskini yanaweza kuletwa na wananchi wenyewe na siyo wanasiasa.
“Ninyi wananchi ndiyo mtakaoweza kujiletea maendeleo na siyo wanasiasa, kwani wao wanataka kuwatumia kama madaraja wanapokuja kuomba kura zenu na mwisho wa siku wanawaacha,” alisema Mlapakolo.
Mlapakolo alisema ili kuondokana na adha hiyo ni vizuri wananchi kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura ili kupata fursa ya kuchagua viongozi wa kweli kutoka upinzani.
Naye Mkurugenzi wa Habari Wilaya ya Morogoro Mjini, Nafuu Mbena alisema kuwa ni vizuri wananchi kutambua kuwa mwaka huu wanapaswa kufanya uamuzi mgumu wa kuiondoa CCM madarakani.
Chanzo: Mwananchi
0 comments