Tuesday, 14 July 2015

MKUTANO WA LOWASA WAZUA TAHARUKI

By    
Mkutano wa Waandishi wa habari na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, uliotakiwa kufanyika jana nyumbani kwake Masaki, jijini Dar es Salaam, umehairishwa, huku kukiwa na taharuki juu ya kile alichotarajiwa kukizungumza kwa umma na taarifa mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii zikizagaa.

 Sababu za kuahirishwa kwa mkutano huo zinaelezwa kuwa ni kutokana na kuchelewa kufika kwa Lowassa akitokea mjini Dodoma.

 Mapema asubuhi jana Waandishi wa Habari walitakiwa kufika nyumbani kwa kiongozi huyo ambaye pia ni Mbunge wa Monduli kwa tiketi ya CCM kwa ajili ya kuzungumza jambo ambalo halikuwekwa wazi.

 Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari tangu majira ya saa 3:30 asubuhi, waliwasili nje ya nyumba hiyo na kuelezwa kuwa Lowassa bado hajafika na hivyo hakuna mkutano kama ilivyokuwa imetengazwa awali.

 Taarifa mbalimbali zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook na WhatsApp zilikuwa zikieleza kuwa nyumba ya kiongozi huyo imezingirwa na watu wa usalama wa Taifa kwa lengo la kuimarisha ulinzi, huku wengine wakidai kuwa anajiandaa ‘kutimkia’ upinzani baada ya kukosa nafasi ya Urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

 Katika mitandao hiyo kuna kiu kubwa ya watumiaji wake kutaka kusikia kauli ya kiongozi huyo baada ya jina lake kuenguliwa katika mchakato huo.

 Lowassa alijizoelea umaarufu wakati akiwa Waziri Kuu, wizara alizoziongoza ikiwamo Wizara ya Maji, Maendeleo ya Mifugo, kutokana na umahiri wake wa kusimamia masuala mbalimbali ya maendeleo.

 Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, Msemaji wa Lowassa, Abubakari Liongo, alisema mkutano huo wa Waandishi wa habari ulipangwa kufanyika jana majira ya saa 5:00 asubuhi, lakini ulishindikana kutokana na kwamba walichelewa kuwasili kutoka mkoani Dodoma.

“Taarifa zinazosambaa kuwa nyumba ya Mheshimiwa imezingirwa na watu wa ulinzi siyo za kweli, na waandishi waliofika pale asubuhi waliona hilo, pia kuhusu kuhamia upinzani ni maneno ambayo watu wameamua kuyaandika na kusambaza ila hakuna ukweli wowote,” alisema.

 Alisema Lowassa atazungumza na waandishi wa habari kama alivyokuwa amepanga, lakini ni baada ya kukamilisha baadhi ya mambo na kwamba kila chombo cha habari kitajulishwa.

 Tangu kutangazwa kwa mgombea wa kupeperusha bendera ya chama hicho, Dk. John Magufuli, Julai 12, mwaka huu, Lowassa hajajitokeza mbele ya umma kuzungumza lolote, tofauti na wagombe wengine ambao tayari wametangaza kuunga mkono mgombea aliyepitishwa.

 Katika mkutano mkuu wa CCM mjini Dodoma, Dk. Magufuli alimtangaza Mgombea mwenza ambaye ni Samia Suluhu Hassan. 

 Lowassa ni kada aliyetangaza nia ya kuomba ridhaa ya CCM kupeperusha Bendera ya chama hicho, lakini jina lake lilienguliwa katika hatua za awali za Kamati Kuu ya chama hicho ambayo ilitoa majina matano.

 Baada ya Kamati Kuu kumaliza kazi yake majira ya saa 6 usiku na majina matano kujulikana, wajumbe watatu, Dk. Emmanuel Nchimbi, Adamu Kimbisa na Sophia Simba, walizungumza na waandishi wa habari kupinga maamuzi ya kamati hiyo na kwamba hawahusiki nayo.

 Aidha, Julai 11, mwaka huu, Halmashauri Kuu ya CCM, ilikutana na kutoa majina matatu, huku katika mitaa mbalimbali kukiwa na maandamano ya wafuasi wa Lowassa, wakitaka jina lake kurejeshwa na kuwa miongoni mwa wanaoomba ridhaa ya chama hicho.

 Shinikizo hilo lilisababisha majina matatu kutotajwa haraka, na Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete, alipoingia ukumbi wa mkutano alipokelewa na nyimbo za kushinikiza jina la Lowassa kurejeshwa miongoni mwa majina yanayotakiwa kupigiwa kura na wajumbe wa mkutano huo.

Kikwete alishindwa kuendelea na mkutano huo na kuahirisha kwa kile kilichoelezwa ni kutoa nafasi kwa wajumbe kwenda kupata chakula cha mchana, na waliporejea hali ilikuwa tofauti kwani hakukuwa na nyimbo zozote.

 Katika mitaa mbalimbali ya mji wa Dodoma hasa karibu na Makao Mkuu ya chama, kulikuwa na maandamano ya baadhi ya wananchama huku wengine wakitambaa barabarani, kushinikiza jina la Lowassa kurejeshwa kuwa miongoni mwa wateule.

 Maandamano hayo yaliwakusanya watu kwenye eneo la Nyerere Square wakiimba nyimbo za Lowassa kuwa ndiye raisi wao na kutawanywa na askari waliokuwa wameimarisha ulinzi mjini humo.

CHANZO: NIPASHE

0 comments