Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Rished BADE |
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imelazimika kuwapa wafanyabiashara wa Mkoa wa Mbeya namba za simu watakazotumia kutoa taarifa za watumishi wa mamlaka hiyo waliojipatia mali kwa kipindi kifupi.
Miongoni mwa namba hizo za huduma ya bure ni 0689 122515 ya kupiga, huku ya kuandika ujumbe ikiwa ni 0689 122516.
Meneja wa Idala ya Maadili wa TRA, Simon Kingu alisema mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa pia wafanyabishara hao wanaweza kuwasiliana na mameneja wa mikoa au kamishna mkuu wa mamlaka hiyo kutoa taarifa.
Kingu alisema wamechukua hatua hiyo baada ya kupokea kero nyingi za watumishi wa mamlaka yake wakati wa kujadili mwonekano wa wafanyakazi wa mamlaka hiyo katika jamii na nini kifanyike ili kuweka mambo sawa.
Mdau Devule Mwambije alisema baadhi ya watumishi wa TRA wanaogopwa kutokana na kukosa uamini, kupenda rushwa na kubambika kodi.
Mwambije alisema wapo watumishi ambao badala ya kudai kodi ya Sh400,000 kwa ajili ya mabasi ya biashara wanaomba Sh200,000 ili watoe stika zinazotumika kwa mwaka mzima sawa na zile za Sh400,000.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, wenye viwanda na Kilimo (TCCIA) Dk Lwitiko Mwakalukwa alisema wafanyabiashara hawawataki TRA kwa sababu hawatoa elimu ya kutosha kwa kuhusu mambo mapya.
Alitoa mfano kwamba mashine za kielekroniki za kutolea risiti (EFD) ni nzuri, lakini TRA ililazimisha kabla ya kutoa elimu.
Alisema ni vyema mashine hizo zipelekwe kwa wafanyabiashara wote baada ya kupatiwa elimu kama ilivyo Kenya.
Mwakalukwa alisema huko Kenya mashine hizo zinatumiwa na wafanyabiashara wote wakiwamo wa daladala, hoteli na hata wenye baa.
Kutokana na kauli hiyo, Meneja wa Maadili TRA, alisema mamlaka imeamua kuimarisha kitengo cha maadili na kwamba imeteua watalaamu kutoka Uingereza ambao kwa sasa wanafanya utafiti kujua ukweli na hatimaye watatoa taarifa ya namna ya kurekebisha kasoro za utendaji.
CHANZO: MWANANCHI
0 comments