Monday, 14 September 2015

MUFTI: MAHUJAJI WA TANZANIA WAKO SALAMA

Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakari Zuberi
LICHA ya ongezeko la vifo vya mahujaji katika mji mtakatifu wa Makka nchini Saudi Arabia, imeelezwa kuwa, hakuna taarifa za vifo vya Waislamu wa Tanzania waliokwenda kutekeleza Ibada ya Hijja nchini humo.

Hayo yameelezwa na Mufti wa Tanzania, Shekhe Abubakari Zuberi jana katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Alisema hadi sasa bado hawajapata taarifa yoyote kuhusu vifo au kujeruhiwa kwa Watanzania waliokwenda kuhiji Makka.

“Napenda kuwataarifu Watanzania wote kuwa waendelee kuwa wavumilivu na kuwaombea wenzetu walioenda kuhiji huko Makka. Hadi hivi sasa hatujapata taarifa yoyote, lakini tunaendelea na juhudi za kufuatilia kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi,” alisema Mufti.

Aidha, alisema tukio hilo ni la kusikitisha na Waislamu wote wawaombee dua kwa Mwenyezi Mungu waliopoteza maisha ili wapumzike mahala pema peponi na kwa wale waliojeruhiwa wapone mapema.

“Tukio hili lilisababishwa na kuanguka kwa winchi iliyokuwa inatumika kwa ujenzi jirani na Msikiti wa Makka na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 107 huku mamia wengine kujeruhiwa vibaya.

“Natoa wito kwa Waislamu wote nchini na misikiti yote kuwaombea dua wenzetu waliotangulia mbele ya haki ili wapumzike salama, sisi wote ni mali ya Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea,” aliongeza.

Alisema mahujaji wa Tanzania walianza kuwasili katika mji wa Makka kuanzia Septemba 9 mwaka huu na hivyo Bakwata pamoja na serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje wanafuatilia ili kujua hali zao na kadhia iliyotokea huko.

“Watanzania waendelee kuwa watulivu na wastahimilivu wakati tunaendelea kufuatilia hali za wenzetu na pindi tukipata taarifa sahihi basi tutawataarifu kupitia vyombo vya habari,” alisema Sheikh Zuberi.

Naye Ofisa Habari wa Shirikisho la Taasisi za Hija Tanzania, Hamisi Juma Tembo, alikaririwa juzi akiwa Uwanja wa Ndege ambako mahujaji wengine walikuwa wakisafiri akisema kwamba taarifa alizo nazo ni kuwa hakuna hujaji wa Tanzania aliyekufa ama kujeruhiwa katika ajali hiyo.

Hivi karibuni kulitokea mvua kubwa na upepo nchini Saudi Arabia iliyosababisha kuanguka kwa winchi hiyo iliyokuwa inatumika katika ujenzi wa kupanua eneo la Tawaf katika msikiti huo wa Makka kwa mita za mraba 400,000 ili kuweza kuchukua idadi ya waumini milioni 2.2 kwa wakati mmoja.

Kwa sasa eneo hilo lina uwezo wa kuchukua watu milioni 2. Tukio lilitokea ikiwa ni siku chache kabla ya kuanza kwa ibada ya Hija inayofanyika kila mwaka ambayo kwa Waislamu ni moja ya nguzo muhimu.

Chanzo: habarileo

0 comments