Thursday, 10 September 2015

WAGOMBEA SITA WALIO WEKEWA PINGAMIZI RUKSA KUENDELEA NA KAMPENI

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imesikiliza na kuamua rufaa sita kati ya 13 za ubunge na kuruhusu waliowekewa pingamizi kuendelea na kampeni.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mkuu wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpigakura, Gueness Aswile, alisema Nec imezikataa sababu za rufaa zote na kukubaliana na uamuzi wa wasimamizi wa uchaguzi.

Aliyataja majimbo hayo kuwa ni Tandahimba aliyekata rufaa ni Likumbo Salim (CCM) dhidi ya Katani Katani (Cuf), Mwanga aliyekata rufaa Henry Kilewo (Chadema), dhidi ya Profesa Jumanne Maghembe (CCM) na Anderson Msuya (NCCR Mageuzi).

Jimbo lingine ni Wanging’ombe rufaa ilikatwa na Lwenge Hosea (CCM, dhidi ya Dismas Luhwago (Chadema), Handeni Mjini rufaa ilikatwa na Daud Lisewa (Chadema) dhidi ya Dk. Abdallah Kigoda (CCM) na Kasulu Mjini, rufaa ilikatwa na Bunyago Boniface (NCCR Mageuzi) dhidi ya Daniel Nsanzugwanko (CCM).

“Katika majimbo yote, Tume imekataa rufaa na wagombea wote wanaendelea na kampeni za uchaguzi,” alisema.

Aswile alisema Nec imesikiliza rufaa za madiwani 70 kati ya rufaa 118 zilizokuwa hazijafanyiwa uamuzi kutokana na vielelezo vyake kutokamilika na kati ya rufaa 70 zilizoamuliwa, 14 zimekubaliwa na wagombea wamerudishwa kugombea.

“Hii ina maana kuwa Tume imetengua uamuzi wa wasimamizi wa uchaguzi na kuwarejesha wagombea katika kinyang’anyiro cha udiwani katika kata zao. Kwa rufaa 58       Nec imekataa sababu zilizotolewa na kukubali uamuzi wa wasimamizi wa uchaguzi,” alisema.

Alizitaja kata ambazo rufaa imekubaliwa kuwa ni Ushorombo (Bukombe), Rukuraijo na Nyaruzumbura (Kyerwa), Kagondo (Manispaa ya Bukoba), Mabibo (Ubungo) na Chisano (Mlimba).

CHANZO: NIPASHE

0 comments