MAKUSANYO ya mapato ya Serikali yameendelea kuongezeka, ambapo mwezi huu Serikali inatarajia kukusanya karibu Sh trilioni 1.5. Makusanyo hayo yatavunja rekodi iliyowekwa Desemba mwaka jana ya Sh trilioni 1.4.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Servacius Likwelile, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake. Alisema kuwa sasa Serikali inajivunia kugharimia miradi ya maendeleo kwa kutumia fedha za ndani, bila ya kutegemea fedha za wahisani.
Akizungumzia hali ya uchumi na mapato ya nchi, Dk Likwelile alisema Rais John Magufuli alisisitiza suala la kuongeza makusanyo ya mapato ya kodi, kwa kuwataka wale wote wanaostahili kulipa kodi walipe, ili fedha hizo zifanye kazi ya maendeleo ya Taifa.
Alisema kwa msisitizo huo, makusanyo ya mapato ni mazuri na kwamba mwelekeo wa makusanyo ya Januari mwaka huu hadi sasa ni zaidi ya Sh trilioni moja na matarajio ni kufikia Sh trilioni 1.5 na lengo hilo litafikiwa na kuvuka. Dk Likwelile alisema kutokana na mfumo mzuri uliowekwa hivi sasa, wa kubana matumizi yasiyo na tija na kuweka vipaumbele, Serikali imetumia fedha za ndani kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo na hivyo utegemezi wa wahisani umekuwa mdogo.
Alisema kwa mwezi Januari mwaka huu, Serikali imetenga Sh bilioni 318.406 fedha za ndani kwa ajili ya kutekeleza miradi yote ya maendeleo, ambayo imepewa vipaumbele. Miradi hiyo ya vipaumbele ni ya elimu, afya, maji, barabara, umeme na kulipa madeni na pensheni za wastaafu.
“Suala la kujivunia ni kwamba tunaweza kutoa fedha za ndani kwa ajili ya kutekeleza miradi yetu ya maendeleo, fedha za wahisani za nje ni kidogo sana, mfano kwa mwezi huu Januari fedha za nje ni Sh bilioni 71.2, wakati fedha za ndani ni Sh bilioni 318.4,” alisema Dk Likwelile.
Akifafanua mapato na matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo kwa mwezi Januari, Dk Likwelile alisema miradi hiyo ya vipaumbele ni kama ifuatavyo; Sekta ya elimu Katika sekta ya elimu, Dk Likwelile amesema msisitizo umewekwa katika kipaumbele cha serikali cha kuhakikisha elimu bure inatolewa kwa wanafunzi wa ngazi ya msingi na sekondari kwa shule za Serikali. Tayari Desemba mwaka 2015, Sh bilioni 18.77 zilipelekwa kwenye shule ikiwa ni za ada, chakula kwa shule za bweni na ruzuku za shule.
Aidha, kwa mwezi huu wa Januari, Serikali imepeleka fedha kiwango hicho tena ili kutekeleza mpango wa elimu bure, huku mahitaji madogo madogo ya mwanafunzi ya kujikimu yakibaki juu ya mzazi au mlezi. Sekta ya ujenzi Katika sekta ya ujenzi wa miundombinu, Dk Likwelile alisema kwa Desemba mwaka 2015 Serikali ilitoa Sh bilioni 193 kwa ajili ya kulipa madeni ya makandarasi wa barabara nchini na kwa mwezi huu Sh bilioni 130 zimetengwa kuwalipa makandarasi hao.
Aidha, Serikali kwa mwezi huu imepeleka fedha kwenye Mfuko wa Barabara Sh bilioni 47.89 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara na kwamba Benki Kuu (BoT) pia kuna akaunti ya Mfuko wa Barabara ambayo ina Sh bilioni 77.3. Aidha, Hazina imepeleka fedha za barabara kwenye halmashauri nchini, ambazo zimepokea Sh bilioni 47.5, ili zitumike kwenye miradi ya barabara kwa lengo la kuboresha miundombinu hiyo.
Sekta ya nishati Kwenye sekta ya nishati, Dk Likwelile alisema Shirika la Umeme (Tanesco), linadai madeni mengi na mwezi uliopita shirika hilo lilipewa Sh bilioni 80 ili kuwekeza kwenye mradi wa umeme wa Kinyerezi Awamu ya Pili. Kwa mwezi Januari mwaka huu, alisema Hazina imetoa Sh bilioni 40 kuipa Tanesco ili ipunguze madeni. Umeme vijijini Kwenye sekta ya nishati vijijini, serikali pia imetoa kipaumbele kwenye miradi ya umeme inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), ambapo kwa Januari Sh bilioni 21.959 zinapelekwa.
Alisema Mfuko wa Rea uliopo BoT, una fedha Sh bilioni 21.9 na Serikali itaongeza fedha nyingine kama hizo, ili mfuko utune na kutumika kutekeleza miradi mingi ya umeme vijijini. Sekta ya maji Katika sekta ya maji, Dk Likwelile alisema, Mfuko wa Maji ulioanzishwa BoT una fedha Sh bilioni 46.3 na kati ya fedha hizo, Sh bilioni 12.5 zilitolewa kuendeleza miradi ya maji na kwa Januari Serikali imeongezea katika mfuko huo Sh bilioni 7.7.
Eneo lingine lililotengewa fedha kwa mwezi huu ni Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa ajili ya pensheni za wastaafu, ambapo fedha zilizotengwa ni Sh bilioni 82.2. Wastaafu walio kwenye daftari la Mhasibu Mkuu wa Serikali, nao wametengewa Sh bilioni 33.3. Pia alisema ukiachilia mbali fedha hizo za miradi, Serikali imetenga pia fedha kwa ajili ya mishahara ya watumishi wake na taasisi zake ambazo ni Sh bilioni 538.5 kwa Januari.
Fedha zilizotengwa kwa ajili ya kulipa Deni la Taifa na wastaafu ni Sh bilioni 784.3 “Tunatenga fedha kwenye sekta zote muhimu na tunatoa fedha kulipa Deni la Taifa ili tusibaki nyuma,” amesisitiza Dk Likwelile.
TRA wanena Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Mapato (TRA), Alphayo Kidata alisema hali ya makusanyo ya mapato nchini ni nzuri na kwamba makusanyo ya Januari mwaka huu lengo lilikuwa kupata Sh trilioni 1.45, lakini hadi sasa zikiwa zimebaki siku mbili, wameshakusanya Sh trilioni 1.31.
“Tunatarajia kuvuka lengo la kukusanya hiyo trilioni 1.45 na sasa tumefika Sh trilioni 1.31 na hizi siku mbili zilizobaki kabla ya kumaliza mwezi (jana na leo) kuna kama Sh bilioni 200 tutaikusanya na kuvuka lengo,” alisema Kidata. Alisema bado ziko fedha kutoka mikoani, ambazo hawajazipokea na kwa siku mbili zilizobaki (jana na leo) na kiasi hicho kitafikiwa na kuzidi, pamoja na kuwa Januari ni mwezi mgumu wa fedha.
Akizungumzia uvumi kuhusu kushuka kwa matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam kwa watu wanaoingiza bidhaa kutoka nje, Kidata alisema hali ya utumiaji wa Bandari ya Dar es Salaam ni nzuri na waingizaji wa bidhaa wameongezeka kwa kipimo cha metriki tani bilioni 111, ikilinganishwa na takwimu za mwaka jana. “Ndio maana tunasisitiza watu wote walipe kodi, zinakusanywa na kwenda kwenye miradi ya maendeleo, wote wanaopaswa kulipa kodi walipe na tunaomba wananchi watusaidie kuwafichua wakwepa kodi,” alisema Kidata.
Kukua kwa uchumi Akizungumzia ukuaji wa uchumi wa nchi, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Beno Ndulu alisema uchumi wa Tanzania umetengemaa na umeendelea kukua kwa asilimia saba, pamoja na kuwepo kwa dhoruba za uchumi duniani. Alisema vipo viashiria vinne vinavyoonesha ukuaji uchumi wa Tanzania unakua na kuongoza uchumi wa nchi za Afrika Mashariki (EAC) na hiyo inachangiwa pia na kuibuka kwa sekta mbili za utalii na viwanda.
Profesa Ndulu alisema kwenye miezi minne ijayo, uchumi wa Tanzania utakua kwa asilimia saba na hiyo inachangiwa na kuanza uzalishaji wa kiwanda cha saruji cha Dangote kilichopo Mtwara. Akifafanua, Gavana Ndulu alisema ukuaji uchumi kwa nchi za Afrika Mashariki, ikiwemo Kenya ni asilimia tano na Uganda ni asilimia 6.2, hivyo Tanzania ndiyo inaelekea asilimia saba na kuwa kinara.
Kiashiria cha pili cha ukuaji wa uchumi, alisema ni mfumuko wa bei ambapo kwa miezi minne, mfumuko umeongezeka kwa asilimia 6.8, lakini kiwango hicho bado ni cha chini ikilinganishwa na kigezo kilichowekwa kwa nchi za Afrika Mashariki ambazo ni asilimia nane. Alisema hivi sasa mfumuko wa bei wa Uganda na Kenya, wamevuka kigezo kilichowekwa na wao wako asilimia 8.3 wakati Tanzania ni asilimia 6.8.
Amesema bidhaa muhimu za mafuta na chakula, mfumuko wa bei wa bidhaa hizo uko asilimia mbili. Maajabu ya viwanda Kiashiria kingine cha kukua kwa uchumi wa Tanzania, alisema ni kuongezeka kwa mapato ya fedha za kigeni, ambapo alisema ingawa bei ya dhahabu duniani imeshuka, Tanzania mwaka juzi ilipata dola za Marekani bilioni 2.5 kwa mauzo ya dhahabu. Alisema mwaka jana mapato hayo yameshuka hadi dola bilioni 1.3, lakini sekta ya viwanda imeziba pengo.
Kwa mujibu wa Profesa Ndulu, pamoja na kushuka huko kwa mapato ya mauzo ya dhahabu, sekta nyingine mbili zimeibuka na kuziba mapengo hayo, ambazo ni utalii iliyokuwa ikichangia kwa muda mrefu na viwanda, iliyoibuka. Kwenye utalii fedha za kigeni zimeongezeka kutoka Dola bilioni 1.5 mwaka juzi hadi kufikia Dola bilioni 2.2 mwaka jana na kwenye sekta ya viwanda hivi sasa ndio sekta ya kujivunia kuliko zote kwa kuongeza mapato.
Kwa sasa sekta hiyo ya viwanda, Profesa Ndulu alisema inaingiza Dola bilioni 1.5 ukilinganisha na awali dola bilioni moja, hali inayoonesha kwamba viwanda vya ndani vinahimili ushindani wa nje na vinaongeza fedha za kigeni. Sekta nyingine inayoongeza fedha za kigeni nchini kwa mujibu wa Gavana Ndulu, ni usafirishaji bidhaa nchi jirani.
Alisema sekta hiyo inaingizia nchi Dola bilioni moja kwa mwaka, fedha ambazo ni nyingi ikilinganishwa na fedha za mazao yote ya kilimo ambayo yanaingizia nchi Dola za Marekani milioni 900 tu kwa mwaka.
Gavana Ndulu alisema kupungua kwa bei ya mafuta duniani, kumesaidia kuimarisha uchumi wetu kwani pengo la mapato ya fedha za kigeni na matumizi yake yametoa unafuu kwa nchi. Alisema kwa mwaka 2016 hali ya uchumi itaendelea kuwa nzuri na kuimarika zaidi na hiyo itaifanya thamani ya Shilingi ya Tanzania kuimarika zaidi.
Chanzo: Habari leo
0 comments