Na Mwandishi wetu
MMILIKI wa Shule nne za Sekondari ikiwamo Mtakatifu Mathew, Marks na Ujenzi, Thadeo Mtembei amewasilisha hati ya dharura katika Mahakama ya Mwanzo Mbagala, Dar es Salaam, kuomba mahakama iamuru upya kuwa watoto watatu aliozaa na Margreth Mwangu ni wa kwake na aruhusiwe kuwalea.
Hati hiyo iliwasilishwa juzi katika mahakama hiyo mbele ya Hakimu Rajabu Tamambele baada ya kutolewa hukumu kuwa watoto watatu waliowazaa ni wa zinaa na kwamba ni wa nje ya ndoa hivyo mahakama haiwatambui.
Katika maombi hayo yaliyowasilishwa na mtoto wa Mtembei, Peter, aliiomba mahakama hiyo itengue uamuzi wake wa awali na badala yake iamuru watoto hao awalee na kuwasomesha.
Alidai kuwa watoto hao alizaa na Mwangu na kwamba aliwajengea nyumba tatu huko maeneo ya Sabasaba, Singida.
Pia hati hiyo ilidai kuwa sababu za kutowalipia watoto ni kutokana na kupata taarifa za kuuzwa kwa nyumba za watoto hao.
Awali, Hakimu Tamambele alitoa hukumu ya kesi hiyo namba 47 ya Mwaka jana, kwamba mahakama haiwatambui watoto na kwamba wazazi watafute namna ya kuwalea.
Hukumu hiyo iliyotolewa Septemba mosi mwaka jana, ilitoa sababu kwamba hakukuwa na ndoa halali bali ni mapenzi ambayo yalisababisha kuzaliwa kwa watoto hao.
Hata hivyo, Mwangu ambaye alidai mahakamani hapo kuwa hana imani na hakimu huyo hivyo hawezi kusikiliza kesi hiyo na kwamba anaendelea na rufaa aliyoikata katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke.
Pia alidai amemfungulia kesi ya jinai Mtembei ya kutelekeza watoto ambayo ipo makao Makuu ya Polisi.
Hata hivyo, mtoto wa Mtembei aliiomba mahakama hiyo kuwasikiliza ili kuwalea watoto hao ambao waliwakataa.
0 comments