Wednesday, 13 January 2016

MICHANGO YAMPONZA MKUU WA SHULE BUKOBA

By    
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Nassoro Mnambila
MKUU wa Shule ya Sekondari ya Bilele ya Mjini Bukoba, mkoani Kagera, Siasa Phocus amevuliwa madaraka kwa madai ya kuendelea na msimamo wa kutaka wazazi wenye watoto shuleni hapo, waendelee kutoa michango kinyume na agizo la serikali.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Nassoro Mnambila aliliambia gazeti hili jana mjini hapa kwamba mwalimu huyo alishapewa utaratibu wa kuzingatia sera ya utoaji elimu msingi bure, lakini alikaidi.

“Kwa mamlaka niliyonayo, nachukua hatua hii kwa kumvua mamlaka mkuu wa shule Bilele kutokana na kushindwa kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na serikali…,” alisema Mnambila.

Alisema mwalimu huyo aliendelea na msimamo wa kuwaambia baadhi ya wazazi waliofika kuuliza utaratibu wa michango, kwamba hana taarifa na miongozo ya serikali, akiwasisitiza kila mzazi kutimiza mahitaji yaliyopo kwenye fomu ya mwanafunzi.

“Mwalimu huyo aliendelea kutoa fomu kwa kila mwanafunzi iliyoainisha kila mahitaji kama ilivyokuwa hapo awali (miaka ya nyuma) huku akitaka michango ya madawati, karatasi za kuchapia mitihani na mlolongo wa gharama nyingine nyingi,”alisema Katibu Tawala.

Michango mingine ambayo wanafunzi wa sekondari wamekuwa wakitozwa kila mwaka ni ya fyekeo, ndoo, jembe, uji, chakula cha mchana na uzio.

Katibu tawala alionya walimu wakuu na wakuu wa shule, kuzingatia na kutekeleza sera ya utoaji wa elimu msingi bure, kama ilivyo kwenye taratibu za miongozo iliyotolewa kwao katika idara ya elimu.

Fedha zafika mikoani

Wakati huo huo, mikoa mbalimbali imethibitisha kupokea fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa elimu bure. Jumla ya Sh bilioni 18.77 zimetolewa na serikali kwa ajili ya shule zote za umma nchini.

Miongoni mwa mikoa iliyothibitisha kwa waandishi wa habari kupokea fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza elimu msingi bila malipo ni pamoja na Kagera, Morogo, Rukwa na Mwanza.

Ofisa Elimu wa Mkoa wa Kagera, Aloyce Kamamba alisema wamepatiwa jumla ya Sh 810,157,000 ambazo zimeshaelekezwa kwenye akaunti za shule zilizoko mkoani humo, ambapo za msingi ni 888 na sekondari 190. Kati ya hizo, 17 ni sekondari za bweni. Kiasi hicho kimetolewa na serikali kwa ajili ya kugharimia huduma mbalimbali ikiwemo chakula.

Mkoani Rukwa, Mkuu wa Mkoa, Magalula Said Magalula alisema wamepokea Sh milioni 336 ambapo Sh 143,859,000 zimepelekwa kwenye shule za msingi 360 na kiasi kilichobaki, kimepelekwa shule 105 za sekondari. Kwa mujibu wa Magalula, fedha hizo ni kwa ajili ya mwezi huu kwani kila mwezi serikali itakuwa ikitoa fedha kwa ajili ya mpango huo.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Kalangasa Manispaa ya Sumbawanga, Gabriel Hokororo, alikiri shule yake kupokea Sh milioni 1.4 kwa ajili ya Januari mwaka huu. Katika Mkoa wa Morogoro, Katibu Tawala Msaidizi wa mkoa huo anayeshughulikia elimu, Wariambora Nkya, alithibitisha kupokea Sh milioni 724.7 kwa ajili ya shule 846 za msingi na 179 za sekondari za bweni na kutwa.

Mkoa mwingine uliothibitisha kupokea fedha hizo ni Mwanza wenye shule za sekondari 197, ambazo zimepewa Sh 642,648,000 kwa ajili ya fidia ya ada za kutwa na bweni na chakula kwa shule za bweni. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo alisema upande wa Shule za Msingi, zipo 850 ambazo zimepokea Sh milioni 356,728,000.

Alisema hadi Desemba 30 mwaka jana, shule zote zilishawekewa fedha kwenye akaunti zake.

Wahadharishwa matumizi

Walimu wakuu, wakuu wa shule, bodi wamesisitizwa juu ya matumizi sahihi ya fedha hizo na wakati huo huo kuzingatia maelekezo ya serikali ya kuhakikisha elimu msingi inatolewa bure.

Licha ya wakuu wa mikoa na idara ya elimu kuhadharisha juu ya hilo, pia Wizara ya Fedha na Mipango hivi karibuni, ilionya wakuu wa shule za msingi na Sekondari watakaotumia ovyo fedha hizo zilizotolewa na serikali kutoa elimu bure, ikisema atakayebainika kuzitumia isivyo, atashughulikiwa.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango iliwataka walimu katika kuhakikisha fedha hizo zinatumika ipasavyo, waweke wazi fedha walizopokea kutoka serikalini wananchi wafahamu alichopewa na matumizi yake.

Bodi za shule zimepewa kazi ya kuhakikisha zinasimamia matumizi na kutoa taarifa. Pia wakuu wa wilaya, mikoa na wakurugenzi wamepewa wajibu wa kusimamia fedha hizo Sh bilioni 14.7, ambazo kati yake, Sh bilioni tatu zimepelekwa katika vyombo vya usimamizi wa mitihani.

CHANZO: HABARI LEO

0 comments