Saturday 1 June 2013

ZANZIBAR YAPIGA MARUFUKU NDOA ZA JINSIA MOJA


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imetunga sheria ya kupiga marufuku ndoa za watu wa jinsia moja.Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar, Bwana Abubakar Khamis Bakar, aliyasema hayo kwenye Kikao cha Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Wawi, Saleh Nassor Juma kutoka Chama cha Wananchi (CUF).

Katika swali lake, Bw. Saleh Nassor Juma alitaka kujua ni lini Serikali ya Zanzibar itatunga sheria ya kukataza ndoa hizo na kuweka adhabu kali kwa watu ambao watabainika kufanya vitendo hivyo vichafu. 
Waziri Abubakar amesema, ndoa za watu wa jinsia moja ni kinyume na utamaduni wa Zanzibar na kwamba sheria hiyo imeweka adhabu ya kifungo cha miaka saba kwa wale wote watakaopatikana na hatia hiyo. 

Pia alisema, "Sheria hii inahusu makosa mengi yakiwemo ya ubakaji, zinaa, usagaji na umalaya ambayo yote yana adhabu ya kifungo cha maisha au miaka isiyopungua 30 gerezani,".

0 comments