WADAU wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi mkoani Kilimanjaro
wameiomba serikali kufungia vibanda vinavyoonyesha picha za ngono kwani
vimekuwa kichocheo kwa watoto wenye umri chini ya miaka 18 na
kuchangia kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo.
Akisoma risala ya wadau hao wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi
Duniani, Cardiosa Peter, alisema kuwepo kwa vibanda vya video za
kulipia mitaani, pia kwa kiasi kikubwa vinachangia kumomonyoka kwa
maadili ya watoto.
“Wapo wazazi wamekuwa na tabia ya kuwaruhusu watoto kwenda kwenye
mabanda na wakati mwingine nyumbani kuangalia picha zinazochochea
ngono, na hii inachangia watoto kuanza mahusiano ya kimapenzi mapema na
kuwa kwenye hatari ya kupata ukimwi,” alisema Cardiosa.
Alisema matumizi hasi ya teknoloji ya mawasiliano ikiwemo kuwepo kwa
vibanda hivyo mitaani, ni moja ya changamoto inayokwamisha jitihada za
mapambano dhidi ya ukimwi ambazo zimekuwa zikifanywa na mashirika
mbalimbali pamoja na serikali.
Cardiosa alisema changamoto nyingine ni jamii kuendelea kufuata mila
na desturi ambazo zinachochea maambukizi ya ukimwi pamoja na kuendelea
kuwepo kwa hali ya unyanyapaa.
CHANZO: TANZANIA DAIMA
0 comments