Monday, 7 April 2014

WAISLAMU KENYA WALAANI MSAKO WA KIHOLELA WA POLISI

By    
Baadhi ya viongozi wa jamii ya Wasomali Kenya na viongozi wa Kislamu wamelaani msako mkubwa unaofanywa na polisi na kikosi maalum cha kupambana na ghasia mjini Nairobi kufuatia mashambulio na mauwaji ya hivi karibuni huko Kenya.

Viongozi hao wameituhumu serikali kwa kuwalenga Waislamu na hasa Wasomali walipofanya msakao mkubwa wa nyumba moja hadi nyingine katika mtaa wa Eastleigh mwishoni mwa wiki na kuwakamata karibu watu 500. 

Mwishoni mwa wiki katika msako mkubwa ulowahusisha karibu polisi elfu sita na wale wa kikosi maalum cha kupambana na ghasia ulifanyika ili kuwasaka mahalifu kufuatia miripuko mitatu ya bomu mjini Nairobi wiki ilyopita.

Mkuu wa wabunge walio wengi Aden Duale mwenye asili ya Kisomali alikua afisa wa kwanza kutishia siku ya Ijuma kwamba atajiondoa kutoka muungano unaotawala wa Jubilee, kutokana na kile alichokieleza ni 'kukamatwa kiholewa wakazi wa jamii yake'.

Siku ya Jumapili viongozi wa jamii ya Kislamu na Wasomali, walikutana Nairobi na  wamelaani kitendo cha polisi kuwakamata na kuwabughudhi watu wakati wa msako wa mtaa wa Eastlegh.  

Akizungumza na Sauti ya Amerika mbunge wa Mvita, Mombasa, Abdulswamad Sharif Nassir anasema, msako huo unaowalenga jamii fulani ya watu ni makosa na inazidisha chuki miongoni mwa wakazi.

Naibu Spika wa zamani wa bunge la Kenya Farah Maalim, kwa upande wake alisema, kwamba polisi wamewaibia raia na kuwabughudhi na kuwakamata wanawake na watu wasiohusika na ugaidi.

Mwambi Mwasaru, Mkurugenzi wa kundi la kutetea haki za waislamu Mombasa, Muhuri, anasema polisi wanakiuka haki za binadam na sheria za nchi wanapofanya  msako jumla na kwa njia ya kiholela.

Bw Mwasaru anasema makundi ya kutetea haki za binadam yanaitaka serikali itafute mbinu nyingine kuwasaka magaidi na wala si raia wasio na hatia.

Lakini inavyonekana hadi hivi sasa wakuu wa usalama wanatetea mbinu wanazotumia kwani kamishna wa polisi wa County ya Nairobi, Njoroge Ndirangu anasema hawajalenga Eastleigh pekee, bali ni msako uloanza mwezi Februari na utafanyika Nairobi nzima.

Kutokana na msimamo huo Mkurugenzi wa Muhuri anasema watalazimika kufikisha mashtaka mahakamani. Mbunge Sharif Nasser kwa upande wake anasema inabidi kuwepo na mazungumzo kati ya pande zote zinazohusika ili kukabiliana na tatizo jumla la usalama.


0 comments