Monday, 17 August 2015

BASATA YALIFUNGULIA SHINDANO LA MISS TANZANIA

By    

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limelifungulia shindano la urembo la Miss Tanzania baada ya mwandaaji wake Kampuni ya LINO International Agency Limited kufuata taratibu, kuomba radhi na kuyafanyia kazi baadhi ya mapungufu yaliyojitokeza na kutekeleza masharti aliyopewa.

Itakumbukwa kuwa mnano tarehe 22/12/2014 BASATA liliwaandikia barua LINO International Agency Limited ya kulisimamisha shindano la Miss Tanzania kwa miaka miwili (Mwaka 2015 na 2016) na kuwaagiza kujipanga upya na kurekebisha kasoro ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara.

Mapungufu yaliyobainishwa ni pamoja na; mosi, kutokufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za uendeshaji matukio ya Sanaa nchini, pili kutokuwasilisha nyaraka mbalimbali za shindano lake hususan mikataba ya washiriki. Tatu kutumia mawakala wasiosajiliwa na kupewa vibali vya BASATA.

Miongoni mjwa mapungufu ambayo Kampuni ya LINO imeyafanyia kazi ni kuanza mchakato wa usajili wa mawakala – BASATA na kufanyia marekebisho kanuni na taratibu za uendeshaji wa Mashindano ya Urembo ya Miss Tanzania. Aidha, LINO imewasilisha muundo wa kamati ya uendeshaji wa shindano yenye muelekeo wa kuzingatia jinsia.

Katika kuboresha na kurudisha hadhi ya shindano la Miss Tanzania, LINO International Agency Limited imepewa kibali cha muda kisichozidi miezi minne (4) kwa ajili ya maandalizi ya awali ikiwemo kukamilisha usajili wa mawakala katika ngazi zote husika.

BASATA linapenda kuwafahamisha wadau wote wa Sanaa hususan wale wa shindano la urembo la Miss Tanzania kwamba Kampuni ya LINO imetekeleza maagizo ya msingi iliyopewa kama masharti ya kufunguliwa. Na kwamba baada ya kufanyia kazi changamoto zilizokuwa zimejitokeza BASATA limeyafungulia mashindano ya Miss Tanzania kwa masharti ya kukamilisha changamoto zilizobakia.

Ni matarajio ya BASATA kwamba kampuni ya LINO itazingatia taratibu zote za uendeshaji wa matukio ya Sanaa nchini na kwamba haitarudia tena makosa yatakayopelekea kuliweka shindano hili katika hali ya kushuka hadhi na kuzua sintofahamu katika jamii.
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini

Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI

0 comments